KATIKA SIKU HIYO WATASEMA,HUYU NDIYE BWANA TULIYEMNGOJA.

KATIKA SIKU HIYO WATASEMA,HUYU NDIYE BWANA TULIYEMNGOJA.

Isaya 25:8 “Amemeza mauti hata milele; na Bwana MUNGU atafuta machozi katika nyuso zote; na aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote; maana Bwana amenena hayo.

9 Katika siku hiyo watasema, Tazama, huyu ndiye Mungu wetu, Ndiye tuliyemngoja atusaidie; Huyu ndiye Bwana tuliyemngoja, Na tushangilie na kuufurahia wokovu wake”.

Upo wakati ambao, tutamwona Kristo uso kwa uso kwa mara ya kwanza, siku hiyo ya tarehe Fulani, na mwezi Fulani na mwaka Fulani, Tutaisikia Parapanda ya Mungu.. Parapanda hiyo haitamuhusu kila mtu, hapana, bali kwa wale ambao walikuwa wanaingojea kwa subira,..siku hiyo pengine itakuwa ni asubuhi kwa upande wako, wakati jua linachomoza mapema kabisa na ndege wanalia kwenye viota vyao, pengine utakuwa unakwenda kupiga mswaki, ajiandae kwenda kanisani, ghafla, utaanza kuona mabadiliko ya tofauti angani, utaanza kusikia sauti nzuri za parapanda, ikitokea mbali sana, pengine utajiuliza jambo hili ni nini? Wakati unaendelea kushangaa shangaa hivyo, ghafla utaona makaburi mengi yanafunguka, na wafu wengi wanafufuka, utawaona unaowajua na usio wajua..

Wakati huo utakuwa unajiuliza labda unaona maono au nini.. kwasababu utakuwa ni wewe tu peke yako ndio unayeyaona hayo yote, hakuna mwingine yoyote atakayeyaona..Saa hiyo hiyo utakuwa unawaona wale wafu nao wanakuja kukufuata kwa furaha, wanakuambia..Hii ndio ile siku tuliyokuwa tunaisubiria, kwa kipindi kirefu, kwa miaka mingi sasa imetimia..

Na wakati mnafikiria hayo, kwa mshangao mkubwa wa furaha isiyo na kifani, Mtaona juu mbinguni jeshi la malaika wengi, linatokea likiambatana na Bwana,(Bwana wetu Yesu)..na ghafla muda huo huo mnaanza kuona miili yenu inabadilishwa na kuwa miili mingine ya kimbinguni, inameta meta na ya utukufu, na bila kupoteza muda mnaanza kunyanyuka mnaiacha ardhi kwa mara ya kwanza, mnaanza kwenda juu kwa kasi sana, kumkaribia YESU mwenyewe Mafalme wa wafalme,..

Kisha wote tunakutana naye pale juu akitungojea kwa tabasamu la upendo wa ajabu, embu fikiria utakuwa na furaha kiasi gani, unamwona kwa mara ya kwanza Yesu uliyekuwa unamsubiria kwa miaka mingi, uso wake unauona uliyekuwa unatamani kuuona.. ndio hili neno litatimia.

Isaya 25:9 “Katika siku hiyo watasema, Tazama, huyu ndiye Mungu wetu, Ndiye tuliyemngoja atusaidie; Huyu ndiye Bwana tuliyemngoja, Na tushangilie na kuufurahia wokovu wake”.

Kumbuka kitendo cha wewe kuyashuhudia hayo yote, kwa watu wengine huku duniani kitakuwa ni kitendo cha kufumba na kufumbua..watashangaa tu haupo, umetoweka. Hawatasikia parapanda wala hawataona makaburi yakifunguka.

Na kwa jinsi watu watakaonyakuliwa watakavyokuwa ni wachache, hata ulimwengu hautasaidiki habari hizo, watasema tu wamepotea watu kadhaa, lakini watapatikana, hivyo watu wataendelea na shughuli zao kama kawaida, wakingojea dhiki kuu ya mpinga-Kristo.

1Wathesalonike 4;15 “Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti.

16 Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza.

17 Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele”.

18 Basi, farijianeni kwa maneno hayo.

Wakati sisi tukichukuliwa na lile jeshi la malaika na kupelekwa mbinguni kwenye karama Yesu aliyotuandalia kwa zaid ya miaka 2000, mahali ambapo furaha isiyokuwa na kifani itakuwepo,.huku chini wanadamu wote watakuwa wanapita dhiki kuu, ambayo haijawahi kutokea mfano wake..

Tukose mengine yote,tusiikose siku hiyo ya unyakuo..

Unyakuo upo karibu sana ndugu, ni jambo la kushangaza, kama wewe bado mpaka leo hii, unapuuzia habari za wokovu.. Unasubiri siku ile ikujie kwa ghafla ndio uamini? Kama gonjwa hili la Corona lilivyoijia dunia kwa ghafla ndipo wakaamini kuwa dunia inaweza ikageuzwa na kuwa kitu kingine ndani ya muda mfupi?..Ndivyo unyakuo utakavyokuja na dhiki itakavyoanza!

Tubu dhambi zako sasahivi, mpokee YESU maishani mwako, ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO ili upokee kipawa cha Roho Mtakatifu, sawasawa na Matendo 2;38, uupate wokovu.. kisha uishi maisha ya kama mtu anayemngojea KRISTO..Ili siku ile na wewe uwe mmojawapo wa watakonyakuliwa na Bwana..

Hatuna muda mwingi, hapa duniani, mavuno ya dunia yamekwishakomaa (kulingana na maandiko),..siku yoyote hukumu ya Mungu itaanza kama vile tunavyoona dalili za kuanza kwake leo hii zilivyo, ikiwa bado unasubiria dalili nyingine ndio uamini basi ujue utajikuta umeingia katika dhiki kuu, na wakati upo katikati ya dhiki kuu ndio utauliza Habari za unyakuo, na utaambiwa..unyakuo ulishapita siku nyingi! Hivyo tubu leo ukabatizwe…

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

SIKU ILE NA SAA ILE.

SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!

UFANYE NINI KAMA MKRISTO WAKATI HUU WA JANGA LA CORONA?

OLE WA NCHI NA BAHARI.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments