CHUKI ULIZO NAZO KWA MAADUI ZAKO, SIZO ALIZONAZO MUNGU JUU YAO.

by Admin | 8 November 2020 08:46 pm11

Shalom, Karibu tujifunze biblia, ambayo ni Neno la Mungu.

Ni vizuri kumjua Mungu ili tuwe na Amani.. Biblia inasema hivyo katika..

Ayubu 22: 21 “Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia”.

Maana yake ni kwamba tukiyajua mapenzi ya Mungu na tabia za Mungu basi tutakuwa na AMANI,  Na ndivyo mema yatakavyotujia.

Leo kwa neema za Bwana hebu tujifunze kidogo, juu ya tabia ya Mungu.

Wengi wetu katika Maisha tunayoishi, tunakumbana na majaribu mengi yanayoletwa na wanadamu wenzetu. Yaani wapo watu wanatumika na Adui shetani, kutuumiza sisi kihisia na kimwili, na mbaya Zaidi wanafanya hayo huku wanajua kabisa. Kwa lugha iliyozoeleka sasa watu hao wanaitwa MAADUI.

Leo hii ukimwuliza mtu yeyote je! Unao maadui?.. Ni ngumu kusikia mtu akisema kwamba sina maadui kabisa!..  Ni lazima utakuta mtu anao maadui, kwa vyovyote vile.

Wengine maadui zao ni watu wanaowanyanyasa, wengine maadui zao ni watu wanaowadharau kupita kiasi, wengine maadui zao ni watu wanaojisifu juu yao, wengine maadui zao ni watu wanaowaonea wivu n.k. Na katika nyakati hizi tunazoishi, asilimia kubwa ya watu wanaomlilia Mungu, ni kutokana na vita walizonazo dhidi ya wanaowaita maadui zao.

Utakuta mtu atakwenda kanisani kuomba Mungu amnyanyue kwenye kazi yake ili azikomeshe dharau za watu Fulani wanaomdharau, mwingine utakuta yupo kwenye mfungo wa maombi apate fursa Fulani, iwafunge midomo watu Fulani (ambao kwake yeye ndio kama maadui zake). Ni wachache sana ambao utakuta wanafunga kumwomba Mungu awape kazi nzuri, au fursa Fulani ili wamtumikie yeye kupitia hiyo.

Sasa hiyo hali ya kuingia kwenye vita dhidi ya maadui, haikuanzia hapa, ilianzia tangu kwenye biblia..Leo tutajifunza mifano kadhaa ya watu waliopambana na maadui zao, na kwa kupitia mifano hiyo, na sisi pia tutapata kujua hisia za Mungu, juu ya tunaowaita maadui zetu, Pamoja na namna ya kushughulika nao.

HANA na PENINA.

Hawa walikuwa ni wanawake wawili wa mwanaume mmoja aliyejulikana kama Elkana. Penina alikuwa na watoto lakini Hana hakujaliwa kupata Watoto, na kama tunavyojua kitu gani kilifuata, Biblia inasema Penina alianza kumchokoza sana Hana kwasababu ni tasa (1Samweli 1:6). Kwa ufupi ni kwamba alikuwa anamdhihaki na kumdharau sana..kisa tu yeye ana Watoto na mwenzie hana.

Kama wewe unayesoma ujumbe huu ni mwanamke, hebu jiweke kwenye hiyo nafasi, huna mtoto, halafu mwingine aliye naye anakukebehi kebehi, anakupa kupa vijimaneno vya kukumiza na kukudhalilisha. Bila shaka tayari huyo kashakuwa adui yako.

Ndicho kilichomtokea Hana, baada ya kuzungumzwa sana na mke mwenza, uvumilivu ukamshinda ikabidi aanze kumlilia Mungu. Na baadaye kama tunavyoijua Habari, Mungu akasikia kilio chake na yeye akampa Watoto.

Lakini hebu turudi kwa upande wa Elkana, ambaye ndiye mume wa wanawake wote wawili (Hana na Penina). Wakati Hana na Penina ni maadui, Elkana alikuwa anawapenda wote. Wakati Hana anajifungua mtoto wa kwanza, haikumfanya Elkana awachukie Watoto wa Penina, wala haikumfanya amchukie Penina. Ijapokuwa Penina na Hana walikuwa ni maadui.

Ndivyo hivyo hivyo kwa Mungu wetu, Yule ambaye ni adui wako wewe, yule unayemchukia…haimaanishi kwamba Mungu naye anamchukia kama unavyomchukia wewe…yule anayekuudhi sana, haimaanishi kwamba anamuudhi Mungu kama anavyokuudhi wewe. Hivyo usichukue hasira zako ukazifanya za Mungu.

Hebu tujifunze tena mfano mwingine.. wa SARA na HAJIRI. Hawa nao walikuwa ni wanawake wawili, ambao ilifika wakati wakashiriki mume mmoja aliyeitwa IBRAHIMU. Na ikafika kipindi pia wakawa ni maadui kwasababu Hajiri alipata mtoto na Sara hakupata. Na Hajiri ambaye ni kijakazi alianza kumdharau bibi yake, kwasababu hakuwa na mtoto. Hivyo kukawa na ugomvi mkubwa wa chini kwa chini..(maadui hao wawili wamekutana). Na ulipofika wakati wa Mungu kumfungua tumbo Sara, alimfukuza Hajiri Pamoja na mwanawe Ishmaeli.

Lakini je! Jiulize chuki aliyokuwa nayo Sara dhidi ya mtoto wa kijakazi wake Hajiri (yaani Ishamaeli), je! ndiyo hiyo hiyo iliyokuwa juu ya Ibrahimu kwa Ishamaeli?.. Au chuki Hajiri aliyokuwa nayo kwa Isaka mwana wa Sara, ndiyo hiyo hiyo aliyokuwa nayo Ibrahimu kwa Isaka?.. La!..sio hiyo hiyo, Badala yake utaona Ibrahimu aliwapenda wanawe wote na wala hakuna aliyekuwa anamchukia, ijapokuwa mama zao walikuwa hawapatani.

Vivyo hivyo, huyo unayemwona ni Adui yako leo, ambaye ni mtesi wako leo, ambaye anakufanya ulie na kuhuzunika usifikiri Mungu anamchukia kama unavyomchukia wewe. Atakachofanya Mungu ni kumweka mbali na wewe, lakini usifikiri atakuwa na kinyongo naye kama ulichonacho wewe juu yake..wala usifikiri Mungu atamwua kwasababu yako wewe.. Futa hayo mawazo!…Kuanzia leo “anza kumjua Mungu ili uwe na amani”..Wala usipoteze muda wako kumwombea maombi ya kufa..kwasababu hatakufa!!..Ni sawa na Sara kumtuma Ibrahimu akamwue Ishamaeli..atakuwa anapoteza muda wake tu!.

Hali kadhalika usiogope!..Adui yako atakapokuombea shari kwa Mungu..atakuwa anapoteza muda wake tu!..Kwasababu chuki alizonazo yeye juu yako, sizo alizonazo Mungu juu yako. Ni sawa na Hajiri kumtuma Ibrahimu akamwue Isaka. Ni kitu kisichowezekana, atakuwa anapoteza muda wake tu!! Usipoteze muda wako, kufanya hivyo.

Utajifunza tena jambo kama hilo hilo kwa wake wa Yakobo.

Hivyo kwa hitimisho..Bwana wetu Yesu Kristo aliyasema maneno haya…

Mathayo 5:43  “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, UMCHUKIE ADUI YAKO;

44  lakini mimi nawaambia, WAPENDENI ADUI ZENU, WAOMBEENI WANAOWAUDHI,

45  ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.

46  Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?”

Kama unanyanyaswa..usipoteze muda kumwombe shari ndugu yako..kwasababu hayo sio mapenzi ya Mungu, wala usifurahie kuanguka kwake…je! Unadhani Elkana alikuwa anafurahishwa na ugomvi uliokuwepo kati ya Hana na Penina?..vivyo hivyo Mungu hapendezwi na sisi tunapokuwa na ugomvi na watu wanaotuchukia..na wala maombi ya magomvi hayampendezi..

Mithali 24:17 “Usifurahi, adui yako aangukapo; Wala moyo wako usishangilie ajikwaapo;

18 Bwana asije akaliona hilo, likamkasirisha; Akageuzia mbali naye hasira yake”.

Na pia usiogope! Mtu anapokuchukia au anapokufanyia ubaya..au anapokushitaki mbele za Mungu…fahamu kuwa anapoteza muda tu!..kwasababu Mungu hakuchikii kama yeye anavyokuchukia.

Bwana atubariki

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

MPENDE JIRANI YAKO KAMA NAFSI YAKO.

KWANINI NI YESU KRISTO WA NAZARETI?

HEKIMA YA KIMUNGU, INAINGIAJE MIOYONI MWETU?

MALAIKA WAPELELEZI WA HUKUMU WANAPITA SASA.

CHAPA YA MNYAMA

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/11/08/chuki-ulizo-nazo-kwa-maadui-zako-sizo-alizonazo-mungu-juu-yao/