Neema ni nini?

by Admin | 12 November 2020 08:46 am11

Neema ni nini kibiblia?


Neema ni “upendeleo usio na sababu” au kukubaliwa kusikostahili. Upo upendeleo wenye sababu na usio na sababu. Mfano wa upendeleo wenye sababu ni huu tulionao sisi wanadamu, sisi tunapendelea walio wetu, yaani watu tunaowajua au wenye manufaa katika Maisha yetu kama vile ndugu zetu, marafiki zetu n.k.

Hakuna mwanadamu yeyote anayeweza kumpendelea adui yake..Hakuna mwanadamu yeyote anayeweza kumpendelea yule mtu anayemuudhi. Hakuna mwanadamu yeyote mwenye uwezo wa kutoa huo upendeleo, isipokuwa Mungu peke yake. Ni Mungu tu ndio mwenye uwezo wa kufanya hivyo, Mungu ana uwezo wa kumpendelea yule mtu ambaye hastahili kabisa mbele zake.

Sasa ili tuielewe neema vizuri hebu soma hichi kisa..

Mathayo 20:9  “Na walipokuja wale wa saa kumi na moja, walipokea kila mtu dinari.

10  Na wale wa kwanza walipokuja, walidhani kwamba watapokea zaidi; na hao pia wakapokea kila mtu dinari.

11  Basi wakiisha kuipokea, wakamnung’unikia mwenye nyumba,

12  wakisema, Hao wa mwisho wametenda kazi saa moja tu, nawe umewasawazisha na sisi tuliostahimili taabu na hari za mchana kutwa.

13  Naye akamjibu mmoja wao, akamwambia, Rafiki, sikudhulumu; hukupatana nami kwa dinari?

14  Chukua iliyo yako, uende zako; napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe.

15  Si halali yangu kutumia vilivyo vyangu kama nipendavyo? Au jicho lako limekuwa ovu kwa sababu ya mimi kuwa mwema?

16  Vivyo hivyo wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho”.

Umeona hapo, hao waliofanya kazi lisaa limoja tu wamelipwa sawa na wale waliotaabika mchana kutwa. Ni kama vile wamependelewa, lakini hakukuwa na  sababu yeyote iliyowafanya wao walipwe sawa na wale wengine waliotaabika mchana kutwa, basi tu ni kama wamependelewa, wangepaswa walipwe kiwango kidogo Zaidi ya wenzao, na Zaidi ya yote hao ndio wangepaswa walipwe wamwisho, lakini chaajabu ndio wametangulia kulipwa…Sasa huo ndio mfano wa NEEMA.

Lakini ipo NEEMA moja kubwa sana ambayo sisi wanadamu tumepewa na Mungu. Nayo hiyo si nyingine Zaidi ya UZIMA WA MILELE. Baada ya anguko pale Edeni, hatukustahili tena tupate nafasi ya kuishi milele, Habari yetu ndio ilikuwa imeishia pale. Hatujui labda angeamua kuumba viumbe wengine, hilo hatulijui..lakini shughuli yetu ndio ilikuwa imeishia pale..

Lakini Mungu akatazama, na pasipo sababu yoyote (kama bahati tu!) ikatokea akapenda tu kutupa UZIMA WA MILELE, Wala usidhani ni kwasababu tulikuwa tunatilisha huruma sana mbele zake, ndio sababu akatuhurumia akatupa uzima wa milele..la!, wala sio sababu tulimwomba. Ni neema tu!..Ni neema tu…

Hakukuwa na sababu yoyote ya sisi kuupata tena uzima wa milele. Wala Mungu kutupoteza daima isingekuwa ni kitu kikubwa sana kwake, kwasababu kabla ya kutuumba sisi alikuwepo milele huko mamilioni na mamilioni ya miaka, alikuwepo huko peke yake pasipo sisi..Kwahiyo kamwe tusifikiri kwamba tulikuwa ni lulu sana mbele zake, ndio maana akatupa tena nafasi ya kuupata uzima wa milele.. Ni Neema tu!..Ni neema tu!..tumependelewa pasipo sababu yeyote. Angeweza kufuta na kuumba wengine na angetusahau sisi moja kwa moja…

Na alianza mpango huo wa wokovu kwa kumtuma Mwanawe mpendwa Yesu Kristo, ambaye kila amwamini huyo ATAPATA UZIMA HUO WA MILELE.

Yohana 1:14  “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; AMEJAA NEEMA NA KWELI”.

Kwahiyo hebu tutafakari kama tumeokolewa kwa neema, (maana yake tumepata upendeleo ambao hatukustahili)..tunawezaje leo kuudharau Msalaba wa Yesu?.

Biblia inasema katika…

Waebrania 2:3  “sisi je! Tutapataje kupona, TUSIPOJALI WOKOVU MKUU NAMNA HII? Ambao kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliosikia”.

Neema ya Msalaba sio kitu cha kuchezea hata kidogo. Kwasababu ndio kitu pekee kilichoificha ghadhabu ya Mungu juu yetu sasa, ikiondoka Neema hapo ndio tutajua kuwa hatukuwa watu maalumu (special) sana mbele za Mungu. Hapo ndipo tutakapojua kuwa kumbe Mungu anaweza kuishi bila sisi.

Waebrania 10:28  “Mtu aliyeidharau sheria ya Musa hufa pasipo huruma, kwa neno la mashahidi wawili au watatu.

29  Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu YULE ALIYEMKANYAGA MWANA WA MUNGU, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na KUMFANYIA JEURI ROHO WA NEEMA?”.

Ndugu tuko ukingoni kabisa mwa hii Neema kuisha, Hii nafasi tuliyopewa ya kuokoka haitakuwepo milele. Siku parapanda ya mwisho itakapolia ndio utakuwa ukomo wa hii neema. Na kwa wale watakaoukosa unyakuo ndio watahakiki nini maana ya neema maana, watakapoona kilio cha maumivu yao hayasikiwi na Mungu, wakiwa katika ziwa la moto, watakapokuwa wanaungua na kulia kwa machozi, ndipo wakiwa huko watajua kuwa hisia zao si kitu mbele za Mungu, wataona kumbe hatukuwa watu maalumu sana, mbele za Mungu kama tulivyokuwa tulikuwa tunadhani au tunahubiriwa, ndipo watajua kuwa waliichezea neema..

Ndugu mimi na wewe tusiwe miongoni mwa watakaotengwa na Mungu milele. Leo hii mpokee Kristo kama hujampokea kwa kutubu dhambi zako zote ulizokuwa unazifanya na kuziacha kabisa, Kristo yupo mlangoni mwa moyo wako sasa, anatamani aingie ili ayaokoe Maisha yako..Ikiwa upo tayari kufanya hivyo sasa na wala si kesho basi fungua hapa >> SALA YA TOBA

Neema ya Kristo ikae nasi sote.

Maran atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

FUNGUO ZA UZIMA, MAUTI NA KUZIMU.

KUZIMU NI WAPI

ITAFAKARI SIKU YA HUKUMU.

KITABU CHA UZIMA

Ni kweli mtu anaweza akafa lakini roho yake ikawa inatumika kama msukule (kumilikiwa na mtu fulani kwa wakati) mahali pengine?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/11/12/neema-maana-yake-nini/