by Admin | 19 November 2020 08:46 am11
Kitabu cha waraka wa pili wa Yohana ( 2 Yohana ) ndicho kitabu kifupi kuliko vyote katika biblia nzima, kina sura moja tu na mstari 13, kinapatikana katika agano jipya. Ili kujua ujumbe wake ni nini, fungua hapa >>> WARAKA WA PILI WA YOHANA.
Lakini tukirudi katika agano la kale, kitabu kilicho kifupi kuliko vyote ni Kitabu cha Obadia, (japo sio kifupi kuliko vyote katika biblia nzima) chenyewe kina sura moja tu na mistari 21,
Kitabu hichi kinaeleza mambo mabaya yaliyofanya nchi ya Edomu kwa ndugu zao wayahudi. Edomu ni taifa lililozaliwa na Esau yule ndugu yake Yakobo. Hivyo mataifa haya mawili yangepaswa yawe ni ndugu na kushirikiana katika shida na raha.
Lakini ilipotekea shida katika Israeli, wakati ule wanachukuliwa utumwani na Nebukdreza, na miji yao kuchomwa na kuteketezwa, hawa Waedomu huwakuja kuwasaidia ndugu zao waisraeli, badala yake walikuwa wanafurahia kwa kilichokuwa kinatendeka, Na kibaya zaidi walikuwa wanawasapoti maadui wa ndugu zao kufanya hivyo.
Obadia 1:11 “Siku ile uliposimama upande, siku ile wageni walipochukua mali zake, na watu wa kabila nyingine walipoingia katika malango yake, na kumpa kura juu ya Yerusalemu, wewe nawe ulikuwa kama mmoja wao.
12 LAKINI USIITAZAME SIKU YA NDUGU YAKO, siku ya mashaka yake, wala usisimange juu ya wana wa Yuda siku ya kuangamizwa kwao; wala usinene maneno ya kiburi katika siku ya shida yao.
Hivyo Mungu akaliona hilo ndipo akatumia kinywa cha nabii Obadia, kuitamkia hukumu Edomi, akasema nchi yao nayo itaangamizwa, na wageni wataitawala,
Obadia 1:4 “Ujapopanda juu kama tai, Ijapokuwa kioto chako kimewekwa kati ya nyota, Nitakushusha kutoka huko; asema Bwana”.
Na zaidi ya yote Mungu atawarejesha wana wa Israeli tena, na kuwamilikisha nchi hiyo. Lakini wao wataangamizwa, kwasababu hawakuona uchungu juu ya ndugu yao wa damu.
Obadia 1:17 “Bali katika mlima Sayuni watakuwako wenye kuokoka, nao utakuwa mtakatifu; na nyumba ya Yakobo watamiliki milki zao.
18 Na nyumba ya Yakobo itakuwa moto, na nyumba ya Yusufu itakuwa mwali wa moto, na nyumba ya Esau itakuwa mabua makavu, nao watawaka kati yao, na kuwateketeza; wala hatasalia mtu awaye yote katika nyumba ya Esau; kwa kuwa Bwana amesema hayo”.
Tunajifunza nini?
Tunapaswa tuoneane huruma sisi kwa sisi, na kusaidiana kinyume chake tukiwa tunafurahia mabaya yawapate wapendwa wetu, na kibaya zaidi tunashirikiana na wale wanaowaangamiza tujue kuwa Mungu anaweza kutugeuzia kibao na sisi kama alivyofanya kwa Waedomi. Atamwokoa yule ndugu yako, lakini wewe atakuangamiza.
Vilevile inatufundisha kuwasaidia wale walio wadhaifu wa imani, Ikiwa tutaona mtu fulani anashida ya kiroho, na shetani anataka kumwangamiza, na sisi, hutaki kuchukua hatua yoyote kwenda kumfundisha au kumuhubiria, hilo nalo ni kosa kama walilolifanya waedomi.
Hivyo Bwana atusaidie tuwe na moyo wa kusaidiana kama kitabu hichi Obadia kinavyotufundisha. Ni kitabu kifupi lakini kina ujumbe mzito sana kwetu.
Shalom.
Kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/11/19/kitabu-kifupi-katika-biblia-ni-kipi-na-ujumbe-wake-ni-upi/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.