USITAFUTE KUKANWA NA BWANA SIKU ILE.

by Admin | 23 Novemba 2020 08:46 um11

Kukanwa hakuna tofauti sana na kusalitiwa..Ni maneno pacha!.. Alichokifanya Yuda hakina tofauti sana na alichokifanya Petro. Tofauti ni kwamba mmoja “kamkataa Yesu” mwingine “kamuuza”..lakini wote wamemkana, na wote wamemsaliti.

Utauliza hata Petro alimsaliti Bwana?..Jibu ni ndio!.. kumkana mtu wakati wa mateso yake na dhiki yake, na siku zote mlikuwa mnatembea pamoja ni kumsaliti pia!.

Sasa kuna maneno Bwana Yesu aliyasema ambayo ndio kiini cha somo letu leo.

Tusome..

Mathayo 10:33  “Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.

34  Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja kuleta amani, bali upanga. ”

Sasa kukana maana yake ni nini?..

Mnapokubaliana na mtu, na kuwekeana nadhiri ya kwamba mtakuwa pamoja katika shida na raha, na ukatembea na huyo ndugu yako ukiamini kwamba popote mtakuwa pamoja mkisaidiana na kuteteana, halafu ghafla mnaingia kwenye tatizo, yule ndugu yako anakukataa ghafla tu, anasema hakujui, wala hamjuani! pasipo kutegemea..huko ndiko kukanwa au kusalitiwa.

Ndicho Bwana alichomaanisha hapo kwamba siku ile atawakana baadhi ya watu. Ikiwa na maana kuwa, hapa duniani ataendelea kutembea na wewe kama rafiki wa kweli kwako, ukimwomba kitu atakupa, hata ukiumwa utakuponya, utaweza kwenda kukemea pepo kwa jina lake litatoka,  utajihisi kabisa kwamba unaye rafiki wa kweli maishani mwako, na utakuwa na uhakika kwamba huwezi kupotea kamwe, yeye yupo na wewe, ukimwita atakuitikia… Lakini siku ile utashangaa amekuwaje!!..utashangaa anakuwambia sikujui…Ndipo utaanza kusema… si ni juzi tu ulinitokea kwenye ndoto ukanionyesha maono, si ni juzi tu, nilitoa pepo kwa jina lako, si ni juzi tu ulinionyesha unabii..inakuwaje leo unasema hunijui??…Huko ndio kukanwa, ambako kunaumiza sana.

Na ndio maana alisema;

Luka 13:24  “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze.

25  Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako;

26  ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu.

27  Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu.

28  Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje”.

Na pia Bwana alizungumza maneno kama hayo hayo katika kitabu cha Mathayo…

Mathayo 7:21  “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.

22  Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?

23  Ndipo nitawaambia dhahiri, SIKUWAJUA NINYI KAMWE; ONDOKENİ KWANGU, ninyi mtendao maovu”.

Leo hii watu wengi wanapumbazika na fadhili za Mungu..na huku mioyoni mwao wamemwacha Mungu, mioyoni mwao wamemkana na kumkataa, bado ni wazinzi kwa siri, bado ni wauaji, waizi, walevi, wachawi, waabudu sanamu, na watu wanaoupenda ulimwengu… Wamemkataa Yesu, na maishani mwao kwasababu wanaona Mungu anazidi kuwapa afya, wanadhani Kristo anapendezwa nao, wanaona bado wanabarikiwa katika biashara zao, wanadhani wapo mioyoni mwa Kristo, wanapomwomba Kristo, hiki au kile wanapatiwa wanajua wanatembea na mtu ambaye kamwe hawezi kuwakana…Oo inasikitisha sana siku ile ghafla yule aliyekuwa anawapa chakula, aliyekuwa anawashika mkono wakati wa shida, aliyekuwa anawaponya, aliyekuwa anawafaraji wakati wa shida, ghafla anawakana na kuwaambia SIWAJUI…Na haishii hapo, anaendelea na kusema ONDOKENI KWANGU….

Siku hiyo utasema, yule Yesu wa upendo leo hii ananifukuzaa!!!!.. Yule niliyekuwa kila siku namwona kwenye maisha yako leo hii ananifukuzaa…Hutaamini lakini ndivyo itakavyokuwa!!!

Tusitamani kukanwa siku ile. Je Kristo ameyatakasa maisha yako? Au bado unapumbazika na fadhili zake kwako?..Kumbuka yeye anasema anawanyeshea mvua waovu na wema…hivyo si jambo kubwa sana yeye kukupa wewe gari, kama anaweza kukupa nishati ya jua bure kwa miaka yote hiyo uliyoishi, na huku bado ni mlevi, hivyo ni gari atakupa pia, na nyumba (wala si shetani ambaye atakupa, ni yeye Yesu) lakini siku ile atakuambia dhahiri sikujui..Kama hujampokea Yesu, na kufanya uteule wako imara, huu ni wakati wako sasa. Tubu dhambi zako na pia tafuta ubatizo kama bado hujabatizwa, na Kristo atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu, ambaye atakuongoza kukupeleka kule anakotaka yeye.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

JE YESU AMEJIAMINISHA KWAKO?

KWANINI KRISTO AFE?

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita..

JINSI SHETANI ANAVYOZUIA MAJIBU YA MAOMBI YETU.

Kitabu kifupi katika biblia ni kipi, na ujumbe wake ni upi?

Rudi Nyumbani:

WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/11/23/usitafute-kukanwa-na-bwana-siku-ile/