JIFUNZE KUTOA KATIKA HAZINA YAKO VITU VIPYA NA VYA KALE.

by Admin | 10 December 2020 08:46 pm12

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze maandiko..

Mathayo 13:51  “Yesu aliwauliza, Mmeyafahamu hayo yote? Wakamwambia, Naam.

52  Akawaambia, Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale.

53  Ikawa Yesu alipoimaliza mifano hiyo, alitoka akaenda zake”.

Swali: unaweza kujiuliza kwanini Bwana Yesu aliufananisha ufalme wa mbinguni na mtu mwenye nyumba ambaye anatoa katika hazina yake vitu vipya na vya kale..

Siku zote mtu mwenye busara, katika nyumba yake (hususani katika store yake)..ni lazima utakuta vitu vipya na vile visivyo vipya. Na lengo la kuwepo vitu visivyo vipya ni ili kukarabati vile ambavyo si vipya wakati unaofaa.

Kwamfano utaona mtu aliyejenga nyumba..na hatimaye ikabaki misumari kadhaa, au rangi, au vikabaki vipande vya mabati, wengi huwa hawaendi kuvitupa badala yake wanaviweka stoo, kwaajili ya matumizi ya baadaye ambayo yanaweza kujitokeza.  Pengine baadaye atakuja kufikiria kutengeneza banda la mifugo yake kama kuku, na vile vipande vya mabati au mbao vilivyosalia vinaweza kumsaidia..au pengine kukatokea hitilafu kwenye nyumba yake, na hivyo itambidi afanye ukarabati, ile hazina ya rangi na misumari na mabati vinaweza kuja kumsaidia…au yeye anaweza asivihitaji lakini pengine ndugu yake mwingine atakuja kuvihitaji huko mbeleni, hivyo ni lazima vihifadhiwe…

Ndio hapo utakuta  kitu kinaweza kukaa stoo hata miaka 5 au zaidi.. kadhalika mtu mwenye busara aliyevaa viatu mpaka vikachakaa huwa haendi kuvitupa, ataviweka stoo, kwasababu anajua utakuja kufika wakati hivyo viatu vitapata matumizi aidha atapewa mtu mwingine pengine mwenye haja navyo…au vitatumika kwa shughuli zisizohitaji umaridadi, kama kazi za mashambani au ujenzi.

Na nguo ni hivyo hivyo, zikichakaa huwa watu hawazitupi badala yake wanazihifadhi kwenye makabati ya stoo kwa matumizi ya baadaye kwasababu anaweza kutokea mtu anazihitaji, au maskini, au zinaweza kutumika kama matambara ya kudekia au kusafishia vitu, hivyo hata kama vitakaa stoo miaka 5, au 10 lakini havitatupwa..Sasa mtu huyo huyo huyo wakati huo huo anazo nguo mpya katika makabati yake ndani anazozitumia kwa kutokea nje, vile vile katika stoo yake anazo nguo zilizochakaa na zisizofaa kwa kusudi maalumu. (Hiyo ni hekima).

Na katika elimu ya ufalme wa Mbinguni, na yenyewe ni hivyo hivyo, inafananishwa na mtu  mwenye nyumba…

Ipo elimu ya ulimwengu huu na ipo Elimu ya Ufalme wa Ulimwengu. Elimu ya ulimwengu huu inalenga l katika kumfundisha mtu kuishi jinsi ulimwengu unavyotaka ili afanikiwe. Na kadhalika Elimu ya Ufalme wa mbinguni inalenga kumfundisha mtu, mambo ya kimbinguni ili afanikiwe.

Lakini Bwana Yesu alisema hapo juu Mtu mwenye elimu ya ufalme wa Mbinguni amefanana na na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale..

Maana yake ni kwamba, Mtu mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni (yaani muhubiri yeyote yule, awe Mchungaji, Muinjilisti, nabii, Mwalimu, au yoyote yule), anapaswa awe anajua na kuelewa jinsi ya kulichambua na kulitumia Neno la Mungu kama lilivyogawanyika katika pande zote mbili, (yaani Agano la Kale na Agano jipya).

Huwezi kusema tunalitumia tu agano jipya na wala hatulihitaji agano la kale, Kadhalika huwezi kulifanya agano la kale, lifae kwa sehemu ya agano jipya, na wala huwezi kufanya agano jipya lifae sehemu ya agano la kale….Ni sawa utumie nguo zisizofaa ulizoziweka stoo uanze kuzifanya nguo rasmi za kutokea. Lakini unaweza kuzifanya zile zilizopo store ziwe za kuzikarabati hizi mpya,..unaweza kutumia kipande cha nguo za kale kufutia vumbi katika kiatu chako..Lakini huwezi kutumia suti yako kabatini kufutia vumbi kiatu kilichopo stoo, unachokitumia kuendea shamba.

Marko 2:21  “Hakuna mtu ashonaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; ikiwa ashona, kile kipya kilichotiwa huliharibu lile vazi kuukuu, na pale palipotatuka huzidi”

Vivyo hivyo agano la kale ni kwaajili ya kulipamba agano jipya na kulifanya lieleweke zaidi..

Kwamfano huwezi kuichukua sabato ya agano la kale, na kuilazimisha iwe ni agizo la agano jipya…Lakini unaweza kuitumia sabato ya Agano la kale, kuizungumzia sabato halisi ya Agano jipya ambayo ndio hilo pumziko tunalolipata baada ya kumpokea Kristo (Mathayo 11:28). Na hilo pumziko tunalipata baada ya kumpokea Kristo ambaye ndiye Bwana wa Sabato.

Kwahiyo maagano yote mawili yana umuhimu, na ni wajibu wetu kila siku kutafuta kujua hekima ya kuyatumia maneno ya Mungu ipasavyo. Ndege hawezi kupaa kwa bawa moja tu, atayahitaji yote mawili. Vivyo hivyo na sisi.

2Timotheo 2:15 “Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kwel”

Maran atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/12/10/jifunze-kutoa-katika-hazina-yako-vitu-vipya-na-vya-kale/