Wale mamajusi walikuwa ni wakina nani?

by Admin | 28 December 2020 08:46 pm12

Jibu: Tofauti na inavyodhaniwa na wengi kuwa wale mamajusi walikuwa ni wasoma nyota au watu wenye elimu na nyota (wanajimu)..lakini ukweli ni kwamba hawakuwa wanajimu wala wachawi, wala wasoma nyota.

Mamajusi ni watu ambao hawakuwa wayahudi (yaani waisraeli) biblia inasema walitoka Mashariki,. Katika Nyakati za biblia, likizungumzwa neno mashariki lilikuwa linalenga maeneo ya Babeli au mbali zaidi ya hapo mpaka maeneno ya Hindi, hivyo hawakuwa Wayahudi, bali watu kutoka nchi ya Mashariki.

Lakini pamoja na hayo, walikuwa na juhudi nyingi sana za kumjua Mungu wa Israeli. Ni sawa na yule Malkia wa Sheba aliyetoka mbali sana huko Kushi, kwenda kuisikiliza hekima ya Sulemani,(Mathayo 12:42), au ni sawa na yule Towashi,mkushi aliyetoka huko Kushi kupanda Yerusalemu kumwabudu Mungu wa Israeli.(Matendo 8:26-40).

Hivyo na hawa mamajusi walikuwa ni hivyo hivyo. Hawakuwa waisraeli, lakini walitoka mbali kumtafuta Mungu wa Israeli.

Sasa ni kawaida ya Mungu kuwapa ishara mbali mbali na za ajabu watu wale wanaomtafuta hususani wale ambao sio wa uzao wa Israeli.  Kwamfano utaona huyu mkushi  (yani Mu-Ethiopia), alitoka huko Afrika akasafiri kwenda Yerusalemu, yeye alikuwa anaijua tu torati na vitabu baadhi vya manabii wa Israeli, na wakati anasoma vitabu hivyo akafika kwenye kitabu cha Nabii Isaya, mlango ule wa 53, ambao unazungumzia kuhusu unabii wa ujio wa Masihi (yaani Yesu). Lakini kwasababu hajui chochote, Mungu akamhurumia akamtumia mtumishi wake Filipo aweze kumfafanulia unabii huo, na baada ya kufafanuliwa ili Mungu alithibitishe neno lake ndipo akamwonyesha huyo towashi ishara ile ya KUTOWEKA ghafla kwa Filipo.

Tusome..

Matendo 8:26 “ Malaika wa Bwana akasema na Filipo, akamwambia, Ondoka ukaende upande wa kusini hata njia ile itelemkayo kutoka Yerusalemu kwenda Gaza; nayo ni jangwa.

27  Naye akaondoka, akaenda; mara akamwona mtu wa Kushi, towashi, mwenye mamlaka chini ya Kandake malkia wa Kushi, aliyewekwa juu ya hazina yake yote; naye alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu,

28  akawa akirejea, ameketi garini mwake akisoma chuo cha nabii Isaya.

29  Roho akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo.

30  Basi Filipo akaenda mbio, akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, Je! Yamekuelea haya unayosoma?

31  Akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye.

32  Na fungu la Maandiko alilokuwa akilisoma ni hili, Aliongozwa kwenda machinjoni kama kondoo, Na kama vile mwana-kondoo alivyo kimya mbele yake amkataye manyoya, Vivyo hivyo yeye naye hafunui kinywa chake.

33  Katika kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa. Ni nani atakayeeleza kizazi chake? Kwa maana uzima wake umeondolewa katika nchi.

34  Yule towashi akamjibu Filipo, akasema, Nakuomba, nabii huyu; asema maneno haya kwa habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za mtu mwingine?

35  Filipo akafunua kinywa chake, naye, akianza kwa andiko lilo hilo, akamhubiri habari njema za Yesu.

36  Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?

37  Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.] 8.38  Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza. 8.39  Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi.

40  Lakini Filipo akaonekana katika Azoto, na alipokuwa akipita akahubiri Injili katika miji yote, hata akafika Kaisaria”.

Sasa huyu Towashi, Mkushi hakuwa na elimu yoyote ya kuhusu “watu kutoweka”, wala hakuwa mchawi mpaka akaiona ile ishara… Hapana ni Mungu tu alipenda kumpa ile ishara ili aamini kiwepesi. Mungu angeweza kumwonyesha ishara nyingine yoyote, lakini alichagua kumwonyesha hiyo, angeweza kumpa ishara hata kama ile ya Musa mkono wake kugeuka kuwa wenye ukoma na kurudia tena hali yake, au Mungu angeweza kuchagua ishara ya jua kusimama,  lakini Mungu aliichagua hiyo ya Filipo kupotea kwa makusudi yake, ili aamini kirahisi.

Vivyo hivyo na wale mamajusi, walikuwa ni watu wa kusoma sana maandiko na vitabu vya manabii wa Israeli, hivyo wakiwa katika “njia panda” ya kutamani kumjua Masihi ni nani, ndipo Mungu akachagua kuwapa ishara ya kuwapa ili kuwathibitishia na kuwaonyesha Masihi ni nani, ndio akawapa hiyo ishara ya  “Nyota”..Wangeweza kupewa ishara ya mwezi, au bahari au chochote kile, kwasababu Mungu hana mipaka anaweza kutumia chochote kile kupitisha ujumbe wake, kipindi fulani aliweza kumtumia Punda kumwonyesha Balaamu dhambi yake, lakini Mungu akawachaguli ishara hiyo, sasa sio kwamba kwa ishara ile walikuwa ni wachawi, au wasoma nyota, la! Walikuwa ni watu wa kawaida kabisa, kama tu wale wachungaji makondeni waliotokewa na malaika na kupewa habari za kuzaliwa kwa Masihi.(Luka 2:8)

Hivyo Mungu anaweza kutumia chochote, alitumia kijiti wakati wa Musa, alitumia Punda wakati wa Balaamu, alitumia milima wakati wa wana wa Israeli jangwani, alitumia jua wakati wa Yoshua, alitumia bahari wakati wa wana wa Israeli, na anaweza kutumia chochote kile hana mipaka..

Biblia inasema katika…

 Zaburi 97: 6 “Mbingu zimetangaza haki yake, Na watu wote wameuona utukufu wake”.

Kwahiyo mamajusi hawakuwa wachawi, wala wanajimu..Walikuwa ni watu wenye kutafuta kwa bidii habari za Mungu na hivyo Mungu akazungumza nao kwa ishara ya kipekee kama ile.

Hivyo na sisi leo Mungu anaweza kuzungumza na sisi kwa ishara yoyote ile aipendayo, lakini ishara hiyo ni lazima iturudishe kwa Yesu na si kwa mwingine yeyote. Ikitupeleka kwa mwingine hiyo ni ishara kutoka kwa yule adui yetu shetani.

Na pia ni muhimu kujua kuwa Leo hii kuna mafundisho ya kusoma nyota kwa kigezo cha hawa mamajusi, hayo ni mafundisho ya Adui, ni vizuri kuwa nayo makini, ni mafundisho ya mashetani, ndani yake kuna roho zidanganyazo na za kuwafunga watu badala ya kuwafungua.

Bwana azidi kutupa macho ya kuyaona hayo.

Maran atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

WAENDEE WANA WA ISAKARI, UWE SALAMA.

UFUNUO: Mlango wa 12

Je ni wanyang’anyi wawili waliomtukana Bwana Yesu au mmoja?

YESU ANA KIU NA WEWE.

KUSUDI LA MIMI KUWEPO DUNIANI NI LIPI?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/12/28/swali-wale-mamajusi-walikuwa-ni-wakina-nani/