JINSI  DHAMBI ILIVYO NA SHINIKIZO KUBWA SANA.

by Admin | 2 January 2021 08:46 pm01

Wakati mwingine kuna mambo unasoma kwenye biblia unaishia kuogopa sana, hususani pale unapoona mtu Mungu anafanya mambo ambayo hata mwenye dhambi si rahisi ayafanye. Kwamfano embu tuwaangalie hawa watu wawili, [Daudi na Yuda]. Hawa wote tunajua walikuwa ni watiwa mafuta wa Mungu, tukianzana na Daudi, tunajua alikuwa ni shujaa sana, na katika ushujaa wake, aliweza kuchagua mashujaa wake wengine 37 waaminifu ili kumsaidia katika vita, na kuipigania Israeli.

Lakini katikati ya mashujaa hao kulikuwa na mwingine ambaye alikuwa mwaminifu sana pengine hata Zaidi ya mashujaa wengine wote, na huyo aliitwa Uria. Uaminifu wake tunausoma jinsi ulivyokuwa.. hakuwa tayari kwenda kujiburudisha nafsi yake wakati kazi ya vita haijamalizika, na wenzake wapo bado mapambanoni, haijalishi kuwa ni mfalme ndiye aliyempa ruhusu ya kuondoka, hakuwa tayari kuondoka. 

2Samweli 11:8 “Daudi akamwambia Uria, Haya, shuka nyumbani kwako, ukanawe miguu yako. Basi Uria akatoka katika nyumba ya mfalme, na tunu ya vyakula ikamfuata, iliyotoka kwa mfalme.

9 Lakini Uria akalala mlangoni pa nyumba ya mfalme, pamoja na watumishi wote wa bwana wake, wala hakushuka nyumbani kwake.

10 Watu walipomwambia Daudi ya kwamba, Uria hakushuka nyumbani kwake, Daudi akamwambia Uria, Je! Hukutoka safarini? Mbona hukushuka nyumbani kwako?

11 Naye Uria akamwambia Daudi, Sanduku, na Israeli, na Yuda, wanakaa vibandani; na bwana wangu Yoabu, na watumishi wa bwana wangu, wamepiga kambi waziwazi uwandani; nami niende nyumbani kwangu, kula na kunywa, na kulala na mke wangu? Uishivyo, na kama roho yako iishivyo, mimi sitafanya jambo hili. 12 Basi Daudi akamwambia Uria, Ngoja hapa leo tena, na kesho nitakuacha kwenda zako. Basi Uria akakaa Yerusalemu siku ile, na siku ya pili yake.

13 Naye Daudi akamwalika, akala, akanywa mbele yake; naye akamlevya; hata wakati wa jioni akatoka kwenda kulala kitandani mwake pamoja na watumishi wa bwana wake, lakini hakushuka nyumbani kwake.”

Unaweza ukajiuliza, mtu kama huyu, labda ndio angependwa kipekee na Daudi, na kupewa zawadi nyingi kwa moyo wake huo wa uaminifu na Upendo, lakini kinyume chake Daudi ndio akampangia njama za kumwangamiza. Tena kumwangamiza katika huo huo uaminifu wake.. Na akafanikiwa,  akamuua kwenye vita, pale alipowaambia mashujaa wake wamwache mwenyewe auawe.

Huyo ndio Daudi mtiwa mafuta wa Bwana,  Lakini ni nini kilichompelekea afanye vile, hakufanya vile kwasababu alipenda, bali kwasababu ya shinikizo la dhambi lililokuwa nyuma yake. Na dhambi yenyewe ilianzia pale, alimuona mke wa Uria, akamtamani, kisha akamchukua alale naye, akadhani itaishia pale pale tu, hakujua kuwa madhara Zaidi yanaweza kuja, matokeo yake akapata mimba yule mwanamke, Na Daudi alipoona hivyo akataka kumbambikizia Uria mimba ambayo si yake wake,  ili tu kusitiri aibu, ndio maana akampa likizo ya ghafla, ili akalale na mkewe, lakini Uria alikuwa mwaminifu hakukwenda kulala na mke wake, alibaki kambini, ndipo Daudi ikambidi abuni mbinu nyingine ya kusitiri uovu wake, ndipo akaamua kukiua kiungo chake kiteule, kisichokuwa na hatia yoyote. Hilo ndio shinikizo la dhambi.

Mwingine ni Yuda, huyu naye alianza dhambi kidogo kidogo tu, ya wizi, hakujua tamaa hiyo itampelekea kuisaliti damu isiyokuwa na hatia, akadhani  ni mambo rahisi rahisi tu, akaendelea kuwa mwizi, mpaka ikafikia hatua ile dhambi iliyokuwa ndani yake ikamshinikiza, kupata hela nyingi Zaidi na njia pekee ambayo ingempelekea kuipata ni kwa kumsaliti Bwana wake, Mtakatifu ili wale wakuu wa makuhani wampe Hela.

Sasa usidhani kwamba kumsaliti Bwana wake ambaye alijua anampenda upeo, na kumweshimu ilikuwa ni jambo analolifurahia sana, hapana, bali lile shinikizo la dhambi, bali lile shinikizo la dhambi ndio lililompelekea kuchukua maamuzi ambayo yalimletea majuto ya milele.

Yuda alimsaliti Bwana wake, alimsaliti jemedari wake, alimsaliti mwokozi wake aliyependa, kwa dhambi ndogo tu ya kupenda fedha na wizi.

Huoni leo hii watu wanawatoa ndugu zao kafara kwa waganga wa kienyeji, unadhani hawawapendi ndugu zao, wanawapenda lakini lile shinikizo la dhambi ambalo lilianza zamani kama tamaa tu ya mali ndilo lililowafikisha mahali ambapo inawagharimu wafanye hivyo, wasipofanya ndio wamekwisha.

Huoni leo hii mabinti wengi, wanatoa mimba ovyo, kama vile si kitendo cha uuaji wanachokifanya. Usidhani hawawapendi watoto wao, lakini lile shinikizo la dhambi pengine la kukwepa aibu, kukwepa kutengwa, kukwepa kufukuzwa shule, kukwepa  majukumu, linawafanya watende vitendo hivyo vya kinyama kila kukicha.

Hata wewe leo hii usidhani huwezi kumuua mtu kwa kumpiga risasi, usidhani huwezi kufanya mambo ya ajabu kupindukia, usiseme hivyo kama ni mtendaji wa dhambi hizo ambazo unaziona za kawaida tu, unaweza kutenda tena na ukawa ni mnyama kuliko hata magaidi wenyewe, kama utaivumilia dhambi ndani yako, Haijalishi utajiita ni mtumishi wa Mungu.

Dhambi ni ya kuiogopa sana, usiseme yule ni mke wa mtu ngoja nikazini naye  leo tu basi, hakutakuwa na shida yoyote, usijaribu kufanya hivyo ndugu, usiseme ngoja niibe kile kidogo kwenye kampuni, hakitaniletea madhara yoyote, usifanye hivyo.. Dhambi inashinikizo kubwa sana, inakupeleka mahali ambapo huwezi kuchomoka mpaka ufanye kufuru mbaya sana. Laiti Daudi au Yuda angelijua tangu mwanzo kuwa watasababisha damu za zisizo na hatia  kumwagika wasingedhubutu kufanya mambo kama yale.

Lolote unaloliona ni dogo maadamu ni dhambi jiepushe nalo tu, kwa usalama wa maisha yako ya rohoni.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Je mtu anayeua anabeba dhambi zote za yule aliyemuua?

USIINGIE MKATABA NA DHAMBI.

ROHO ANENA WAZIWAZI

Swali: Kurushwa upesi kunakozungumziwa katika Danieli 9:21 ndio kupi?

IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/01/02/jinsi-dhambi-ilivyo-na-shinikizo-kubwa-sana/