Sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji zilikuwaje?

by Admin | 30 January 2021 08:46 pm01

Jibu: Katika agano la kale zilitolewa sadaka mbali mbali, na sadaka zote zilizotolewa zilikuwa ni lazima zifike madhabahuni pa Mungu, ili sadaka iitwe sadaka ni lazima ihusishe madhabahu. Isipohusisha madhabahu hiyo haiitwi tena sadaka bali mchango, au zawadi, au msaada. Lakini chochote kinachotolewa na kupelekwa kwenye madhabahu ya Mungu, hicho kinaitwa sadaka.

Sasa katika agano la kale, wana wa Israeli Bwana aliwaagiza wamtolee sadaka, kila mtu kwa hiari yake, na si kwa kulazimishwa..

Kutoka 35: 4 “Kisha Musa akanena na mkutano wote wa wana wa Israeli, akawaambia, Neno hili ndilo aliloliamuru Bwana, akisema,

5 Katwaeni kati yenu matoleo kwa Bwana; MTU AWAYE YOTE ALIYE NA MOYO WA KUPENDA, ayalete matoleo; dhahabu na fedha na shaba”

Hapo anasema Bwana anasema..“kila mwenye moyo wa kupenda” na sio kulazimishwa.. Maana yake kama mtu hajisikii kumtolea Mungu, basi halazimishwi, lakini atajipunguzia Baraka zake kutoka kwa Mungu.

Sasa katika agano la kale yalikuwepo makundi kadhaa ya sadaka, (yaani aina za sadaka watu walizokuwa wanamtolea Mungu). Zilikuwepo sadaka za Wanyama, kama vile Ng’ombe, Mbuzi, kondoo, na Njiwa, Hawa walikuwa wanaletwa Nyumbani kwa Mungu, na kuchinjwa, na kisha damu yao kutumika kufanya upatanisho, na baadhi ya viungo vya miili yao kuteketezwa juu ya madhabahu, na sehemu ya nyama iliyobakia isiyoteketezwa juu ya madhabahu, walikuwa wanapewa makuhani, pamoja na watoto wao..

Pamoja na hayo pia zilikuwepo sadaka za vyakula.. Ambapo watu walikuwa wanaleta nafaka zao kama sadaka kwa Mungu, Ndio hapo zinazaliwa sadaka za Unga na sadaka za vinywaji. Na katika makundi yote hayo ya sadaka, yote yalitolewa fungu la kumi, na malimbuko.

Sasa sadaka za unga, zilikuwa zilihusisha unga (wa ngano au shayiri) uliosagwa vizuri, na kisha kupelekwa kwenye madhabahu, huo unaweza kuwa kilo kadhaa, au au pungufu kidogo, na mtu akishaupeleka, Kuhani anachukua kiwango kidogo cha huo unga, na kuuchanganya na ubani, na kisha kuuchoma huo unga pamoja na ubani ule..Na kiwango kingine cha unga kilichobakia kisichochomwa (ambacho kinakuwa ni kingi) wanapewa makuhani, kama riziki yao.

Walawi 2:1 “Na mtu atakapomtolea Bwana matoleo ya sadaka ya unga, matoleo yake yatakuwa ya unga mwembamba; naye ataumiminia mafuta, na kutia na ubani juu yake;

2 kisha atauleta kwa wana wa Haruni, hao makuhani; naye atatwaa konzi moja katika huo unga mwembamba, na katika mafuta yake, na huo ubani wote; kisha kuhani atauteketeza kuwa ndio ukumbusho wake juu ya madhabahu, ni kafara ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana;

3 na huo uliosalia wa ile sadaka ya unga utakuwa ni wa Haruni na wanawe; ni kitu kitakatifu sana katika sadaka zilizosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto”.

Na kama mtu atapenda asilete unga, bali alete unga uliokadwa tayari na kuokwa (Yaani mkate kamili), basi yalikuwepo maagizo ya jinsi ya kuuandaa huo unga (mkate), na kuuleta madhabahuni.. kwamba huo unga uliokandwa na kuokwa haupaswi kuwekwa hamira wala asali. (Walawi 2:4-11).

Mistari mingine inayozungumzia sadaka hiyo ya unga ni pamoja na Kutoka 29:40-41, Kutoka 30:9, Kutoka 40:29, Walawi 5:13, Walawi 6:15, Walawi 9:17, Walawi 14:10.

Na pamoja na kuwepo sadaka hiyo ya unga, ilikuwepo pia sadaka ya kinywaji ambayo ilikuwa inaambatana na hii ya unga, Isipokuwa katika sadaka ya kinywaji kilichokuwa kinatolewa ni Divai, (Kwasababu ndio kinywaji kilichokuwa cha gharama na heshima, kwa enzi hizo, na kwa tamaduni za kiyahudi), Na Divai haikutumika kwa matumizi ya ulevi, wala anasa,bali kwa matumizi matakatifu. (Kutoka 29:41)

Sasa sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji (Divai) zinafananishwa na mwili na damu ya Yesu. Kristo aliutoa mwili wake na damu yake kama sadaka, kwa ajili yetu..Na Mungu aliruhusu watu wamtolee sadaka hiyo ya unga na ya kinywaji katika agano la kale, kufunua mwili wa Yesu na damu yake katika agano jipya. Na pia aliruhusu makuhani wa agano la kale washiriki sehemu ya sadaka hiyo, kufunua “ushirika wa meza ya Bwana” kwa makuhani wa agano jipya.

Mathayo 26:26 “Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu

27  Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki;

28  kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi”.

Kwahiyo kama vile makuhani walivyoshiriki sehemu ya unga(mkate) na sehemu ya divai iliyokuwa inaletwa madhabahuni, vivyo hivyo na sisi pia tunashiriki mwili na damu ya Yesu, ili tuwe na sehemu katika madhabahu ya Bwana. Kwasababu wote tuliompokea Yesu, tunafananishwa na makuhani wa Bwana.

Ufunuo 1:5  “tena zitokazo kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake,

6  NA KUTUFANYA KUWA UFALME, NA MAKUHANI KWA MUNGU, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina”.

Hivyo kuna umuhimu mkubwa sana wa kuishiriki meza ya Bwana, kwa kila aliyemwamini Yesu, na kuishi katika Neno lake.

Yohana 6:53  “Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu.

54  Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.

55  Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli”.

Kama hujajua namna ya kushiriki meza ya Bwana, na ungetamani kujua basi unaweza kutujuza kwenye box la maoni, chini kabisa mwa somo hili, ili tukutumie somo juu ya hilo kwa urefu.

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

MEZA YA BWANA, NA KUTAWADHANA MIGUU.

Je tunapaswa tushiriki Meza ya Bwana mara ngapi?

NI WAPI MAHALI SAHIHI PA KULIPA ZAKA?

JE! KUNA UMUHIMU WOWOTE WA KULIPA ZAKA?

ALIYOKUTANA NAYO YESU, YERIKO.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/01/30/sadaka-ya-unga-na-sadaka-ya-kinywaji-zilikuwaje/