JE! NI WAPI UTAPOKEA HISIA ZA KWELI ZA KI-MUNGU?

by Admin | 10 February 2021 08:46 am02

Yapo mambo mengi yasiyo ya kawaida aliyoyafanya Bwana Yesu..Lakini kuna mojawapo ningependa tujifunze leo.. Na jambo lenyewe linapatikana katika habari hii..

Marko 7:32 “Wakamletea kiziwi, naye ni mwenye utasi, wakamsihi amwekee mikono.

33 Akamtenga na mkutano faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi,

34 akatazama juu mbinguni, AKAUGUA, akamwambia, Efatha, maana yake, Funguka”.

Uponyaji wa mtu huyu, ulikuwa ni wa kitofauti sana na ponyaji nyingine zote Yesu alizozifanya.. Kwani nyingine zilihitaji Yesu kutamka tu, au kutoa maagizo Fulani machache n.k., lakini hili lilihitaji jambo lingine la kipekee sana.. Nalo ni hisia za ndani kabisa za rohoni.

Bwana alipomwita huyu mtu, na kujua tatizo lake, moja kwa moja akamwekea vidole vyake masikioni, kisha akatema mate akamgusa ulimu..Sasa hakuishia hapo tu kama alivyofanya kwa baadhi ya watu wengine aliowaponya, labda kuwapa maagizo Fulani, kama alivyofanya kwa huyu tunayemsoma katika Yohana 9:6 …

Yohana 9:6 “Alipokwisha kusema hayo, alitema mate chini, akafanya tope kwa yale mate. Akampaka kipofu tope za macho,

7 akamwambia, Nenda kanawe katika birika ya Siloamu, (maana yake, Aliyetumwa). Basi akaenda na kunawa; akarudi anaona”.

Hapana, lakini kwa huyu, ilihitaji Yesu achukue hatua nyingine Zaidi ya rohoni.. Ya kuugua, Ya kuona huruma ya kupitiliza juu ya mtu huyu ambaye alikaa katika hali hiyo ya utasi na uziwi kwa muda mrefu..Ilihitaji aihisi hali yake kwa undani Zaidi isivyokuwa kawaida.

Hivyo ili kupata hisia hizo ilimbidi sasa, ajue ni wapi atazitolea, kwasababu hivi hivi tu haziji vinginevyo atakuwa unafanya kinafki..Ndipo hapo akatazama juu mbinguni..

Alijua huruma ipo kwa Mungu tu mbinguni, alijua upendo upo juu, alijua uponyaji wa kweli unatoka kwa Baba yake juu na si kwa mwingine awaye yote..sasa kitendo cha yeye kuelekeza uso wake mbinguni, ilimsaidia kuvuta kwa haraka ile huruma ya ki-Mungu ndani yake, na hapo hapo akajikuta ANAUGUA sana moyoni..huruma ikamjaa isiyokuwa ya kawaida, na pindi aliporudisha macho yake tu chini, hakumwona yule mtu kama alivyomwona hapo mwanzo.. Bali alimwona kwa jicho la huruma nyingi sana, na ndipo saa hiyo hiyo aliposema EFATHA..yaani funguka..Na yule mtu akawa mzima kabisa.

Ni nini tunajifunza?

Hatuwezi kuwahurumia wengine, hatuwezi kuwaganga wengine mioyo, hatuwezi kuwasaidia wengine ikiwa tu hisia hizi hatuna ndani yetu, ikiwa macho yetu, wakati wote hatuyaelekezi mbinguni, tusitegemee tutaugua mioyoni mwetu kwa Kristo alivyokuwa anaugua kwa ajili yetu.

Mpaka kupelekea kuwa tayari kuuawa kwa ajili yetu sisi tulio dhambini..

Bwana Yesu alisema..

Luka 6:36 “Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma”.

Luka 7:12 “Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye.

13 Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie”.

Huruma za Yesu utazisome sehemu nyingi sana kwenye maandiko kwa muda wako unaweza kuvipitia hivi vifungu Marko 6:34, Mathayo 9:36, 20:34,

Kumbuka Upendo wa kweli, huruma ya kweli inatoka kwa Mungu tu peke yake. Ndicho Yesu alichokifanya.. hakuwatazama wanadamu ndipo kuugua kuje ndani yake, hakuitazama milima, hakuwatazama wanyama bali alitazama juu mbinguni Baba yake mwenye rehema alipo, ndipo huruma ikamjaa moyoni.

Nasi pia tuyaelekeze macho yetu mbinguni, ili tupokee hisia hizi za kweli za Mungu, hisia ambazo zitavuta uponyaji wa ki-Mungu kwa haraka sana. Hisia ambazo zitajenga kuombeana na kusaidiana, Na kuhudumiana.

Na kuelekeza macho yetu mbinguni, maana yake si kuangalia angani, hapana, bali ni kumsoma Mungu wetu kwa bidii, na kujua anataka nini kwetu, na hiyo inakuja kwa kulitafakari Neno lake, pia kwa kusali, na kufunga na kumfanyia ibada..

Hayo yote tukiyafuata itatupelekea kuzipokea hisia hizi za Kristo kwa wingi wote, na matokeo yake tutafukuza roho zote za chuki, na vinyongo, na hasira, fitina, wivu na mashindano ndani yetu.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

BWANA AYAGANGE NA MACHO YETU PIA.

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA PILI WA YOHANA.

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

Je! Kuna malaika wangapi mbinguni?

JE! HAMPOTEI KWA SABABU HII?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/02/10/je-ni-wapi-utapokea-hisia-za-kweli-za-ki-mungu/