Ni kwanini Yesu alisema “Na wakisikia wasikie, wasielewe Wasije wakaongoka?”

by Admin | 19 March 2021 08:46 am03

SWALI: Katika Marko 4:12, Bwana Yesu anasema.. “  ili wakitazama watazame, wasione; Na wakisikia wasikie, wasielewe; Wasije wakaongoka, na kusamehewa”. Swali ni kwamba, kwanini Yesu alisema hivyo kuwa acha wasisikie na kuelewa ili wasije wakaongoka na kusamehewa…na wakati kusudi lake si anataka watu watubu ili wapate kusamehewa dhambi?.


Jibu: Ukianza kusoma kuanzia juu kidogo utaona, Bwana Yesu alikuwa ameutoa ule mfano wa mpanzi mbele ya mkutano mkubwa, na baada ya kuutoa, hakutoa tafsiri yake, kwamba zile mbegu zilimaanisha nini, na lile konde maana yake nini.. Badala yake aliacha tu kama fumbo… Sasa kundi kubwa la watu waliokuwa wanamfuata Yesu, wengi wao walikuwa wanafuata miujiza tu, na si kingine… Lakini ni kundi dogo sana lililokuwa linafuata kwenda kusikia ni nini Yesu anazungumza…Kwa kuelewa zaidi pitia hapa>> Kwa wale walio nje, yote hufanywa kwa mifano.

Kwahiyo hili kundi dogo ambalo lilikuwa linafuatilia kwa makini maneno ya Yesu, ndio lililokuwa linamfuata baadaye Yesu akiwa peke yake na kumuuliza maana ya ile mifano yote aliyokuwa anaitoa. Na ndipo Yesu anawafafanulia mifano ile.

Lakini wengine wengi waliosalia, ambao hawakuwa na haja ya maneno ya uzima ya Yesu, badala yake walikuwa wanafuata miujiza tu, hawakuwa na muda wa kutaka kujua tafsiri ya ile mifano. Kwahiyo ile mifano ilipokuwa inatolewa na Yesu kwao iliishia kuwa kama hadithi tu, na wengine walikuwa wanaishia kuitafsiri wanavyojua wao. Lakini wale wengine wenye hekima walikuwa wanamfuata Yesu baadaye akiwa peke yake na kumuuliza maana ya ile mifano..

Marko 4:8  “Nyingine zikaanguka penye udongo ulio mzuri, zikazaa matunda, zikimea na kukua, na kuzaa, moja thelathini, moja sitini, na moja mia.

9  Akasema, Aliye na masikio ya kusikilia, na asikie.

10  NAYE ALIPOKUWA PEKE YAKE, wale watu waliomzunguka, na wale Thenashara, walimwuliza habari za ile mifano.

11  Akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuijua siri ya ufalme wa Mungu, bali kwa wale walio nje yote hufanywa kwa mifano,

12  ili wakitazama watazame, wasione; Na wakisikia wasikie, wasielewe; Wasije wakaongoka, na kusamehewa”.

Sasa kwanini iwe hivyo?..kwanini Yesu asitoe mfano na tafsiri yake palepale??

Ni kwasababu siku zote Mungu hamlazimishi mtu kumfuata, wala hamlazimishi mtu kusikia maneno ya uzima. Bali Yule ambaye amefungua moyo wake kutafuta kumjua ndiye anayemfunulia zaidi.

Luka 19:26 “Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang’anywa hata alicho nacho”

Kwahiyo lile kundi ambalo halikutaka kutafuta kujua maana ya ile mifano, hiyo ndio kundi lililozibwa macho lisione (maana yake lilinyang’anywa hata kile kidogo lilichokipokea), kwamba lisikie tu mifano lakini lisielewe, kwasababu limekataa kutafuta ukweli.. Kwasababu wametangulia kuyafumba macho yao, na hivyo Mungu akaongeza upofu juu yao….Utaona biblia inalifafanu hilo vizuri katika..

Matendo 28:25 “Na walipokuwa hawapatani wao kwa wao, wakaenda zao, Paulo alipokwisha kusema neno hili moja, ya kwamba, Roho Mtakatifu alinena vema na baba zetu, kwa kinywa cha nabii Isaya,

26  akisema, Enenda kwa watu hawa, ukawaambie, Kusikia, mtasikia wala hamtafahamu; Na kuona, mtaona wala hamtatambua;

27  Kwa maana mioyo ya watu hawa imepumbaa, Na masikio yao ni mazito ya kusikia, Na macho yao WAMEYAFUMBA; Wasije wakaona kwa macho yao, Na kusikia kwa masikio yao, Na kufahamu kwa mioyo yao, Na kubadili nia zao, nikawaponya”

Mstari wa 27, hapo unasema… “na macho yao WAMEYAFUMBA”.. Maana yake hayajafumbwa na mtu, bali wameyafumba wao wenyewe, ili wasisikie… wakati Bwana Yesu anatoa ile mifano, hawakutaka kwenda kutafuta kuuliza maana yake. Hiyo waliyafumba macho yao… Na hiyo sasa Mungu akaitia uzito mioyo yao ili waendelee kukaa katika hali hiyo hiyo…kama neno lake linavyosema katika…

 2Wathesalonike 2:10 “…..na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa.

11  Kwa hiyo Mungu awaletea nguvu ya upotevu, wauamini uongo;

12  ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu”.

Kwahiyo kinachotangulia kwanza ni Watu kuikataa kweli ndani ya mioyo yao, ndipo ile nguvu ya upotevu inaachiwa juu yao..

Hiyo ni tahadhari tu hata kwetu.

Kinyume na inavyodhaniwa na wengi kuwa neema ni kitu cha kuchezea, na kwamba unaweza kuchagua muda wowote wa kumgeukia Mungu, pasipo kujua kuwa kumgeukia Mungu ni neema, na kwamba saa ya wokovu ni sasa, na wakati uliokubalika ni sasa, endapo mtu ataisikia injili ikihubiriwa kwake na kuipuuzia pasipo kuzidi kutafuta ukweli, ile neema inaondolewa juu yake na nguvu ya upotevu inakuja juu yake.

Hizi ni siku za mwisho tunazoishi, na muda umekimbia sana, Kristo yupo mlangoni..na atakuja kama mwivi, kulinyakua kanisa lake, je utakuwa wapi siku hiyo? Wewe ambaye hulitilii maanani neno lake leo?..wewe ambaye ukiambiwa mavazi unayovaa ni mavazi yasiyompendeza Mungu, unadhihaki, wewe ambaye unaipuuzia sauti inayokuonya utubu ndani ya moyo wako?..

Bwana anarudi.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Biblia ina maana gani inaposema akonyezaye kwa jicho huleta masikitiko?

JE! JICHO LAKO LINAONA NINI KATIKATI YA MAJARIBU?

BWANA AYAGANGE NA MACHO YETU PIA.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/03/19/ni-kwanini-yesu-alisema-na-wakisikia-wasikie-wasielewe-wasije-wakaongoka/