by Admin | 20 March 2021 08:46 pm03
SWALI: BWANA apewe sifa mtumishi wa Mungu! Nakusalimia katika jina la YESU KIRSTO. naomba unifafanulie Mhubili 5:1 Mtumishi maana huwa sipaelewi vizuri.. Inasema.
Mhubiri 5:1 “Jitunze mguu wako uendapo nyumbani kwa Mungu; Maana ni heri kukaribia ili usikie, Kuliko kutoa kafara ya wapumbavu; Ambao hawajui kuwa wafanya mabaya”.
JIBU: Amen, jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo litukuzwe daima.
Katika vifungu hivyo, biblia inatutahadharisha jinsi ambavyo tunapaswa tuwe pale tunapotaka kwenda nyumbani mwa Mungu (Kanisani) kumfanyia ibada/ huduma. Anasema ni heri ukaribie usikie, kuliko kutoa kafara za wapumbavu. Maana yake ni kuwa si kila jambo tunaweza kulifanya katika kanisa ilimradi tu, kama tunavyoweza kufanya mahali pengine popote. Kumbuka huduma yoyote, au dua yoyote, unayoifanya au unayoipelekea kwa Mungu hiyo ni kafara.
Leo hii utaona, binti au kijana ni mzinzi, halafu bado akifika kanisani, anakuwa wa kwanza kwenda pale mbele kumwimbia Mungu kwaya, hizo ni kafara za wapumbavu. Au mtu hajaitwa na Mungu, haliishi hata Neno la Mungu lakini ni wa kwanza kwenda kufundisha kanisani kisa tu anajiona anakipaji fulani cha kuongea.Sasa hizo ni kafara za wapumbavu ambazo biblia inasema, kuwa wafanyao hayo hawajui kuwa wanatenda mabaya.. Wanafanya mambo ambayo yatawasababishia madhara wao wenyewe.
Vilevile, kuwa na maneno mengi mbele za Bwana, ambayo hayana maana, hizo nazo ni kafara za wapumbavu, kwamfano utamwona mwingine, akifika tu magotini, ni kumnung’unikia Mungu, na kulalamika mbele zake mwanzo mwisho, kama vile wana wa Israeli walivyokuwa wanafanya kule jangwani ambao mwisho wao tunajua ulikuwa ni kuangamizwa tu badala ya kuponywa.. Hizo nazo ni kafara za wapumbavu na ndio maana mistari inayofuata inasema..
Mhubiri 5:1 “Jitunze mguu wako uendapo nyumbani kwa Mungu; Maana ni heri kukaribia ili usikie, Kuliko kutoa kafara ya wapumbavu; Ambao hawajui kuwa wafanya mabaya.
2 Usiseme maneno ya ujinga kwa kinywa chako, wala moyo wako usiwe na haraka kunena mbele za Mungu; kwa maana, Mungu yuko mbinguni, na wewe upo chini, Kwa hiyo maneno yako na yawe machache”.
Unaona? Maneno yako yawe machache..Ni heri utumie muda mwingi kushukuru, na kuomba kuliko kutoa manung’uniko, au kulaani.
Pia, kafara za wapumbavu ni pamoja na kumwekea Mungu nadhiri, bila kutafakari kwanza, kwamfano utakuta mwingine anaahidi, atamfanyia Mungu kitu fulani kwenye kanisa, halafu hatimizi alichokiahidi, angali zipo katika uwezo wa mikono yao, kama walivyofanya Anania na Safira, ambao mwisho wa siku walikufa , Ukiendelea kusoma mstari wa 4 pale unasema..
Mhubiri 5:4 “Wewe ukimwekea Mungu nadhiri, usikawie kuiondoa; kwa kuwa yeye hawi radhi na wapumbavu; basi, uiondoe hiyo uliyoiweka nadhiri.
5 Ni afadhali usiweke nadhiri, Kuliko kuiweka usiiondoe”.
Pia kutoa sadaka, ambayo imetoka katika shughuli haramu, kama za ukahaba au madawa ya kulevya, usizipeleke nyumbani kwa Bwana..
Kumbukumbu 23: 18 “Usilete ujira wa kahaba, wala mshahara wa mbwa, katika nyumba ya Bwana, Mungu wako, kwa ajili ya nadhiri yo yote; kwani haya ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako, yote mawili”.
Unaona?.. Hivyo kwa kuhitimisha ni kuwa kama bado hujafahamu ni nini ambacho Mungu anakihitaji kwanza kwako, pale unapofika nyumbani mwake, ni heri usifanye chochote kabisa, ukae usikilize tu, ufundishwe mapenzi ya Mungu kwanza, na ndipo baadaye uanze kumfanyia Mungu huduma kanisani. Kuliko kukurupuka kufanyia Mungu chochote kabla hajafahamu mapenzi yake ni nini kwako.
Tunapaswa tujue Mungu, anahitaji kwanza UTAKATIFU wa maisha yetu, ndipo hayo mengine tutakapoyatoa yawe na Baraka zaidi, hatumdanganyishii Mungu kwa kutumika kwetu wakati maisha yetu yapo mbali na wokovu. Alisema mwenyewe..
1Samweli 15:22 “…Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu”.
Hivyo tujitahidi tujue kwanza mapenzi ya Mungu nini.
Shalom.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Ni kwanini Yesu alisema “Na wakisikia wasikie, wasielewe Wasije wakaongoka?”
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/03/20/nini-maana-ya-jitunze-mguu-wako-uendapo-nyumbani-kwa-mungu/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.