Alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru

by Admin | 23 March 2021 08:46 pm03

SWALI: Naomba kufahamu nini maana ya huu mstari?

Wakorintho 3:17 “Basi ‘Bwana’ ndiye Roho; walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru”.


JIBU: Kauli hiyo kinyume chake ni kuwa, kama  Roho wa Bwana hayupo basi mahali hapo hapana uhuru wowote, kwa mujibu wa biblia.

Lakini ni uhuru wa aina gani Roho Mtakatifu analeta.

kibiblia Roho Mtakatifu alikuja kuleta Uhuru wa aina mbili.

1). Tukianzana na uhuru wa kutuondoa katika utumwa wa dhambi;

Siku ile Bwana Yesu alipoanza huduma yake ya kuhubiri alisema maneno haya..

Luka 4:18 “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa,

19 Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa”.

Umeona hiyo ni kuonyesha kuwa Roho Mtakatifu aliposhuka juu ya watu wake na katika kanisa alikuwa na kazi ya kuwatoa watu katika vifungo vya dhambi na mateso ya  ibilisi, yaani waliokuwa wanasumbuliwa na mapepo, waliokuwa wanateswa na magonjwa, na hofu, na mauti, na shida  vyote hivyo vilikuja kuondolewa na Roho Mtakatifu mwenyewe,

na pia ukizidi kusoma tena katika Isaya 61:3-4 utaona unabii huo wa Roho Mtakatifu unaendelea kusema..

“…kuwafariji wote waliao; 3 kuwaagizia hao waliao katika Sayuni, wapewe taji ya maua badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya roho nzito; wapate kuitwa miti ya haki, iliyopandwa na Bwana, ili atukuzwe”.

Unaona anafanya pia kazi ya kuwatoa watu katika huzuni zao, kuwafariji,kuwapa mataji ya utukufu na sifa. huo ni Zaidi ya Uhuru, ambao hakuna mtu yeyote hapa duniani angeweza kuutoa.

2). Uhuru wa sheria;

Pia alikuja kutukomboa sisi tuliokuwa chini ya sharia, tutoke katika laana ya sheria..

Wagalatia 4:3 “Kadhalika na sisi, tulipokuwa watoto, tulikuwa tukitumikishwa na kawaida za kwanza za dunia.

4 Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria,

5 kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana.

6 Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba.

7 Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu”.

Roho Mtakatifu alikuja kututoa katika utumwa wa sheria, ili tupate kuhesabiwa haki kwa njia ya kumwamini Yesu Kristo na sio kwa matendo yetu tena. Kwasababu hapo mwanzo tulijitahidi sana kumpendeza Mungu kwa kushika sheria, lakini sheria ilituzidi nguvu, kwasababu ya udhaifu wa miili yetu. Hivyo tangu enzi za agano la kale, hakuwahi kuonekana hata mmoja aliyeweza kumpendeza Mungu kwa matendo yake mwenyewe, haijalishi walijitahidi kiasi gani.

Hivyo ili Mungu kutuokoa,  alimtuma mwanawe Yesu Kristo duniani, ili yeye peke yake atende mema, pasipo kufanya dhambi yoyote, kisha Mungu amuhesabie haki yeye peke yake kwa matendo yake, na ndipo sasa sisi  tutakaomwamini Yesu baadaye tuhesabiwa haki kama vile yeye, kwa njia ya matendo yake na sio yetu..

Kwahiyo, ikiwa wewe umemwamini Yesu, na ukampokea Roho wake, basi ujue Mungu haangalii matendo yako, kama ndio kipimo cha yeye kukubali, bali anamwangalia mwana wake YESU KRISTO uliyemwamini, na hivyo unahesabiwa haki, kama vile hujawahi kumkosea Mungu, kwasababu VAZI la Yesu linakufunika mbele yako.

Huoni kama huo ni uhuru mkubwa sana? Unahesabiwa haki kwa kumwamini tu!  Lakini ikumbukwe kuwa hiyo haimaanishi kuwa tuendelee kutenda dhambi kisa tu hatuhesabiwi haki kwa matendo yetu, hapana, hata kwa namna ya kawaida, huwezi kwenda kupeleka mkono kwenye tundu la nyoka akung’ate kila saa, kisa tu dawa ya kutibu sumu ipo, hapana, vinginevyo utakuwa mwendawazimu, bali utachukua tahadhari kubwa sana, kwa kuzidi kukaa mbali na nyoka, kwasababu unajua sumu yake sikuzote ni kifo..

Na sisi vivyo hivyo maadamu tunahesabiwa haki kwa kumwamini Yesu Kristo ni jukumu letu sote, tukae mbali na dhambi, kwa kadiri tuwezavyo, katika utakatifu wote ili tupate kumzalia Mungu matunda. Na hiyo ndio ishara ya kuamini kwetu.

Hivyo kwa kuhitimisha ni kuwa Roho Mtakatifu ametuletea uhuru mkubwa sana hapa duniani.  kiasi kwamba mtu yeyote atakayempokea, atakuwa HURU KWELI KWELI. Jambo ambalo watu wengi hawalifahamu, wakidhani kwa Mungu ni utumwa.

Swali ni je wewe umeshampokea ndani yako? Kama jibu ni la, unasubiri nini? Kumbuka Pasipo Roho Mtakatifu huwezi kwenda katika unyakuo, na haji ndani yako isipokuwa  kwanza umemwamini  Yesu Kristo, kwa kutubu dhambi zako kwa kumaanisha kabisa na kuwa tayari kuyaacha mambo yako maovu uliyokuwa unayafanya huko nyuma. Na pili kwa kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji tele, na kwa jina la YESU KRISTO sawasawa na Matendo 2:38, Na hapo ndipo Mungu atakapokupa kipawa cha Roho Mtakatifu ndani yako bure.

Hivyo ikiwa utapenda kumkaribisha Yesu maishani mwako, basi tafuta mchungaji yoyote, au mtumishi yoyote aliyesimama katika Imani, akusaidie, au wasiliana nasi kwa namba hizi: +255693036618 / +255789001312

Mungu akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

JE NI KWELI SAMAKI NGUVA YUPO?

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

UTENDAJI KAZI MWINGINE WA ROHO MTAKATIFU USIOUFAHAMU.

 Nini maana ya “Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati”

NGAZI 7 AMBAZO MKRISTO NI LAZIMA AZIPANDE KUUFIKIA UKAMILIFU.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/03/23/alipo-roho-wa-bwana-hapo-ndipo-penye-uhuru/