MUNGU HAONI SHIDA KUMUHAKIKISHIA MWOVU ULINZI.

by Admin | 11 May 2021 08:46 pm05

Baada ya Kaini kumuua ndugu yake, na Mungu, kumlaani kwa laana ile ya kwamba atakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani, utaona alimwomba Bwana ampunguzie adhabu yake, na baada ya kupunguziwa kwa kutiwa alama, haikuishia hapo,  bado Mungu alimuhakikishia usalama mwingine wa juu Zaidi.  Tusome;

Mwanzo 4:14 “Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua.

15 Bwana akamwambia, KWA SABABU HIYO YE YOTE ATAKAYEMWUA KAINI ATALIPIZWA KISASI MARA SABA. Bwana akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga”.

Unaona hapo kwenye mstari  wa 15, Bwana akimuhakikishia ulinzi wa kipekee sana. Jambo ambalo si rahisi mtu mwovu kufanyiwa na mtu yeyote, kwasababu hakuna tendo lolote la kishujaa alilotenda Kaini mpaka alipiziwe kisasi mara saba, kwa yeyote atakayemuua,ni heri ingekuwa ni mara moja, lakini mara saba, hiyo angepaswa afanyiwe mtu mwenye haki.

Tengeneza picha diktekta, ambaye ameshutumiwa kwa mauaji wa maelfu ya watu, kama vile HITLER wa ujerumani, leo hii, unasikia Mungu anasema mtu yeyote atakayemuua Hitler atalipizwa kisasi mara saba, unaweza kudhani Mungu anafurahishwa na maovu. Ndivyo ilivyokuwa kwa Kaini, Mungu haoni shida kumuhakikishia mwovu ulinzi na mafanikio. Hilo tunapaswa tulijue.

Lakini afadhali ingeishia kwa Kaini tu, Tabia yake ya uuaji iliendelea mpaka kwa uzao wake. Utaona yupo mmoja aliitwa, Lameki, yeye alikuwa muuaji kuliko hata baba yake, anasema alimuua mtu kwa kumtia jeraha tu, alimuua mtu kwa kumchubua tu, akiwa na maana mtu aliyemkosea  kwa jambo dogo sana alikuwa  radhi kumuua, bila kujali chochote.

Huku akitumia kivuli kile kile cha baba yake, cha usalama aliohakikishiwa na Mungu, tena na Zaidi, anasema kama ikitokea mtu atataka kumlipizia kisasi kwa uuaji wake, basi akumbuke kuwa Mungu atamlipizia sio tu mara saba, bali mara saba sabini.

Mwanzo 4:23 “Lameki akawaambia wake zake, Sikieni sauti yangu, Ada na Sila; Enyi wake za Lameki, sikilizeni usemi wangu; Maana nimemwua mtu kwa kunitia jeraha; Kijana kwa kunichubua;

24 Kama Kaini akilipiwa kisasi mara saba, Hakika Lameki atalipiwa mara sabini na saba”.

Unaona? Walikuwa wanajiamulia kufanya mauaji tu kama vile kuchinja kuku, kwasababu walijua hakuna laana yoyote itakayowapata,. Hiyo ndio sababu ulimwengu wa kipindi kile ulizidi kuwa mwovu kupitiliza, mpaka ikafikia hatua ya Mungu kusema, mwisho wa kila mwanadamu umefika.

Mwanzo 6:5 “Bwana akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote.

6 Bwana akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo.

7 Bwana akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewafanya…….

11 Dunia ikaharibika mbele za Mungu, dunia ikajaa dhuluma.

12 Mungu akaiona dunia, na tazama, imeharibika; maana kila mwenye mwili amejiharibia njia yake duniani.

13 Mungu akamwambia Nuhu, Mwisho wa kila mwenye mwili umekuja mbele zangu; kwa sababu wameijaza dunia dhuluma, basi nitawaharibu pamoja na dunia.

Lakini siku moja ilipofika Gharika kubwa ilishuka ikauangamiza ulimwengu wote, wakapona tu watu 8, yaani Nuhu pamoja na familia yake. Na adhabu yao haikuishia tu, pale, bado huko kuzimu walipo sasa hivi, wanaendelea na mateso makali yasiyokuwa ya kawaida.

Ndugu yangu, fahamu kuwa Mungu anaweza kukuahidia ulinzi, na usalama, na afya na amani, na furaha, angali bado upo katika dhambi zako, hilo sio jambo gumu  kwake kukupa, liweke tu akilini, angali ukiwa unafanya uchawi wako bado Mungu anaweza kukuhakikishia Maisha ya heri hapa duniani, angali unaua watu, unauza madawa ya kulevya unauza pombe, unazini nje ya ndoa.. Bado Mungu atakuhakikishia ustawi wa mambo yako.

Hivyo usishangae kwanini waovu hawakumbwi na madhara yoyote, tena Zaidi ndio wanafanikiwa na kustarehe kama ulivyokuwa uzao wa Kaini, jinsi ulivyokuwa na mafanikio makubwa duniani, kuliko hata ule uzao wa Sethi lakini mwisho wao ulikuwa ni gharika.

Huu si wakati wa kustarehe katika dhambi, kisa tu hatuoni dhara lolote mbele yetu, tujue kuwa sisi watu wa kizazi hichi ndio tupo katika hatari kubwa ya kukumbana na ghadhabu kali ya Mungu, inayokaribia kuja duniani hivi karibuni, kuliko hata vizazi vingine vya nyuma vilivyotangulia.

Kwasababu maovu tunayoyafanya sasa hivi, yamezidi hata yale ya wakati wa Nuhu, licha ya kwamba sisi tumeshaufahamu ukweli wote na kuiona njia..

Bwana Yesu alisema.

Mathayo 11:23 “Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa mpaka mbinguni? Utashushwa mpaka kuzimu; kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika katika Sodoma, ungalikuwapo mji huo hata leo.

24 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko wewe”.

Ndugu, Tubu dhambi zako, usipumbazwe na ulinzi wa Mungu, angali upo bado katika dhambi, hizi ni  siku za mwisho, mwisho wa dunia upo karibu sana, dalili zote zimeshatimia, Jiulize UNYAKUO ukipita leo, utakuwa wapi ndugu yangu? Utamweleza nini Kristo siku ile ya hukumu, utamwambia mimi sikusikia injili? Na wale wa Sodoma na Gomora ambao sasahivi wapo kuzimu waseme  nini?

Tafakari Maisha yako, duniani hapa tunapita, na vitu vyote vinapita,. Mgeukia Kristo ayabadilishe Maisha yako leo ili akufanye kuwa kiumbe kipya, kisha uishi  Maisha ya kama mtu anayemsubiria Kristo kweli kweli, na sio kama mtu wa kidunia, acha kudhani kuwa Mungu haioni maovu unayotenda.

Bwana atusaidie sote.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho

Mada Nyinginezo:

UTAKUWA MTORO NA MTU ASIYE NA KIKAO DUNIANI.

USIOMBE MAOMBI YASIYOKUWA NA MAJIBU NA WALA USIMTUKANE MUNGU.

JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.

UZAO WA NYOKA.

UFUNUO: Mlango wa 1

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/05/11/mungu-haoni-shida-kumuhakikisha-mwovu-ulinzi/