UTAKUWA MTORO NA MTU ASIYE NA KIKAO DUNIANI.

UTAKUWA MTORO NA MTU ASIYE NA KIKAO DUNIANI.

Kaini baada ya kumuua ndugu yake Habili, tunasoma pale Mungu alimlaani, na kumwambia.. “utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani”… Lakini tujiulize ni kwanini Mungu hakumrudishia Kaini mapigo ya uuwaji kama aliyoyafanya kwa ndugu yake badala yake akamwambia atakuwa mtu asiyekuwa na kikao duniani?.

Mwanzo 3:13 “Kaini akamwambia Bwana, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki.

14 Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua”.

Ndugu ni heri Mungu akuue, iishie hapo kuliko akuambie utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani..

Sasa unaweza kutafsiri kwa nje kwamba laana hiyo ilimaanisha kuwa Maisha yake yote Kaini yatakuwa ya umaskini, atakuwa mtu atakayekosa mahali pa kulala, atakuwa omba omba, atakuwa mtu wa mitaani tu, lala hoi asiyekuwa na kitu au uelekeo wowote wa maisha…

Lakini sivyo hivyo Mungu alivyomaanisha kwa Kaini, angalia vizuri utagundua kuwa baada ya kutoka tu pale Kaini ndiye aliyekuwa na mafanikio makubwa sana kuliko hata ule uzao wa Sethi uliochukua mahali pa Habili. Mwanzoni tu pale tunaona alijenga mji mkubwa akauita Henoko jina la mwanawe(Mwanzo 4:17). Na tunaona pia uzao wake baada ya hapo, ulikuwa Hodari, ndio uliokuwa na ugunduzi wa hali ya juu wa teknolojia, vitu kama chuma na shaba zilianzia kwao.. Hivyo kwa ufupi Kaini alikuwa na mafanikio makubwa kuliko hata uzao wa Sethi tukizingumzia kwa namna ya kimwili…

Lakini bado laana ile ya Bwana kuwa atakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani ilikuwa juu yake..?

Sasa kama sio hivyo basi Mungu alimaanisha nini?. Sikuzote tunajua mtu mtoro asiye na kikao(makao) ni mtu ambaye hajapata pumziko lolote maishani mwake la kudumu..na ndio maana wanasema moja ya mahitaji makuu matatu ya mtu ni pamoja na kuwa na malazi, au makazi, ukikosa mahali pa kutulia, unakuwa kama mkimbizi ambaye Maisha yake sikuzote hayana pumziko, leo hii upo hapa kesho upo kule, kila mahali kwako sio kwako, ni mgeni daima..

Hivyo Mungu alivyomwambia Kaini kuwa atakuwa mtoro na mtu asiyekuwa na makao, alikuwa anazungumzia hali yake ya rohoni jinsi itakavyokuwa, Maisha yake yote atakuwa ni mtu wa kutafuta lakini hatopata makazi ya kustarehe ya nafsi yake….hatapata pumziko la moyo wake daima..hatopata, hata atufuteje hatoona atakuwa ni huko na kule, wimbi la bahari linalochukuliwa na upepo wa kila aina ya undanganyifu … jambo ambalo halikuonekana kwa Sethi na uzao wake, wao utaona tu muda mchache baada ya kumzaa mtoto wake Jina la Mungu lilianza kuitwa kwa nguvu.

Mwanzo 4:25 “Adamu akamjua mke wake tena; akazaa mwana mwanamume, akamwita jina lake Sethi; maana alisema, Mungu ameniwekea uzao mwingine mahali pa Habili; kwa sababu Kaini alimwua.

26 Sethi naye akazaa mwana; akamwita jina lake Enoshi. Hapo ndipo watu walipoanza kuliitia Jina la Bwana”.

Unaona? Muda mfupi tu uzao wa Sethi ulitambua ni wapi pumziko lipo, na haraka sana likayaendea makao ya kudumu ya roho zao.. Lakini uzao wa Kaini uliendelea kutangatanga na ulimwenguni na humo humo ndipo uchawi ukazaliwa, uovu ukazaliwa, uvuguvugu ukazaliwa, udunia ukazaliwa..n.k.

Hata leo hii, uzao wa Kaini na Sethi unajitambulisha kabisa kwa kazi zake..makundi yote mawili yapo duniani leo hii, lipo ambalo limeshatambua makao yao ya kudumu yapo wapi..Hawa ndio wale waliompokea Yesu Kristo na kupokea lile pumziko la kweli la nafsi zao.

Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”.

Utawagundua kwa tabia zao, hata wakipitia dhiki, au shida, au misiba, au adha, hawapepesuki, kwasababu wanajua tayari yanayo makao yao ya kudumu milele mbinguni…hawana hofu ya Maisha kwasababu wanaye Kristo ndani yao….Amani ya Kristo inawatawala siku zote kwasababu walishampokea.

Lakini uzao ule mwingine wa Kaini kwasababu umeshalaaniwa ndio ule hautaki kumfuata Mungu japo unajijua kabisa unahitaji msaada wa nafsi zao..Huu upo buzy sikuzote kutafuta pumziko la nafsi zao katika kila wanachokiona, kama vile Kaini….Wana wa Kaini walioa wake wengi, na hawa wanatafuta pumziko kwa kuongeza idadi ya wake, (Mwanzo 4:19) na wakati mwingine kuacha wale walio nao na kuoa wengine. Roho zao zinazunguka zunguka kutafuta maana ya Maisha lakini haziwezi kuona kwasababu hazijui kuwa Maisha yapo katika Kristo tu peke yake..

Hawa tayari walishalaaniwa kama Kaini. Haijalishi wana mali au umaskini kiasi gani, bado wapo chini ya laana.

Swali ni je! Na wewe upo kundi lipi?. Ikiwa unasikia injili hutaki kuitii, ikiwa unahubiriwa habari za uhuru ulio katika YESU KRISTO halafu hutaki kuupokea basi fahamu kuwa Mungu hatakuua kama jinsi ambavyo hakumuua Kaini bali atakuacha uendelee na mambo yako ya kidunia ufanikiwe, uwe milionea, uwe mtu mashuhuri duniani, ujenge miji mikubwa kama ya Kaini uwe mgunduzi mpaka upokee tuzo za Nobeli lakini, rohoni uwe mtoro na mtu asiyekuwa na kikao duniani..

Utakuja kulithibitisha hilo siku ile umekufa, siku ile mwenzako wanatoka makubirini na unaowaona wanapewa miili mipya ya utukufu wanakwenda kuishi na Kristo milele katika majumba waliyoandaliwa kule mbinguni, wewe utakuwa huna kao lolote..bali mwisho wako utakuwa palepale kwenye lile ziwa la moto.

Hizi ni nyakati za mwisho mpendwa. Siku yoyote hapa paraparanda italia, mahubiri haya hatutayasikia tena, mavuno yataisha shambani, utakuwa ni wakati mwingine wa kuanza Maisha mapya ya umilele…Je utaimalizia umilele yako wapi? Jehanamu ya moto kwenye mauti ya milele au mbinguni?

Ni maombi yangu kuwa utatubu dhambi zako leo, ikiwa bado upo nje ya Kristo.. Umetanga tanga vya kutosha huu ni wakati wako sasa wa kutia nanga Kwa Kristo..kwasababu yeye ndio KAO LETU, na PUMZIKO LETU LA KWELI. Zingatia kurudi kwa Baba sawasawa na mfano ule wa mwana mpotevu Bwana alioutoa katika..(Luka 15:11-24)

Ubarikiwe sana.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

WANA WA MUNGU, NA BINTI ZA WANADAMU.

MUNGU AKIKUPITA LEO, HAIMAANISHI KUWA HAJAKUCHAGUA.

TAZAMA, MWISRAELI KWELI KWELI, HAMNA HILA NDANI YAKE!

UMUHIMU WA YESU KWETU.

MADHABAHU NI NINI?

Je! vitabu vya biblia viliwezaje kukusanywa pamoja?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments