MUNGU AKIKUPITA LEO, HAIMAANISHI KUWA HAJAKUCHAGUA.

MUNGU AKIKUPITA LEO, HAIMAANISHI KUWA HAJAKUCHAGUA.

Shalom, Jina la Mfalme mkuu Yesu Kristo libarikiwe.

Nakukaribisha katika kuyatafakari maandiko, Kama vile Paulo alivyomwambia Timotheo “Hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma..”(1Timotheo 4:13)..Nasi pia tunapaswa tuonyeshe bidii hiyo hiyo katika kusoma Neno la Mungu kwasababu kila siku yapo mambo mapya Mungu anahitaji tuyaone.

Hivyo, leo tutajifunza juu ya mtume mmoja wa kipekee kidogo anayeitwa Mathiya. Mtume huyu hatumsomi mahali pengine popote katika vitabu vya injili isipokuwa katika kitabu cha Matendo ya mitume. Mtume Huyu hakuwa miongoni mwa wale 12, lakini baadaye tunakuja kusoma alihesabiwa kuwa ni mmojawapo wa wale 12 kama wengi wetu tunavyojua, Na siri ya yeye kuhesabiwa kuwa mmojawapo wale mitume 12 wa Bwana, imeandikwa pale katika biblia, embu tusome:

Matendo 1:15 “Siku zile akasimama Petro kati ya hao ndugu (jumla ya majina ilipata mia na ishirini), akasema,

16 Ndugu, ilipasa andiko litimizwe, alilolinena Roho Mtakatifu zamani kwa kinywa cha Daudi, katika habari za Yuda aliyewaongoza wao waliomkamata Yesu;

17 kwa sababu alikuwa amehesabiwa pamoja na sisi, akapata sehemu ya huduma hii.

18 (Basi mtu huyu alinunua konde kwa ijara ya udhalimu; akaanguka kwa kasi akapasuka matumbo yake yote yakatoka.

19 Ikajulikana na watu wote wakaao Yerusalemu; hata konde lile likaitwa kwa lugha yao Akeldama, maana yake, konde la damu.)

20 Kwa maana imeandikwa katika chuo cha Zaburi, Kikao chake na kiwe ukiwa, Wala asiwepo mtu mwenye kukaa humo;

21 Basi katika watu waliofuatana nasi wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiingia na kutoka kwetu,

22 kuanza tangu ubatizo wa Yohana, hata siku ile alipochukuliwa kwetu kwenda juu, inapasa mmoja wao awe shahidi wa kufufuka kwake pamoja nasi.

23 Wakaweka wawili, Yusufu, aitwaye Barsaba, aliyekuwa na jina la pili Yusto, na Mathiya.

24 Kisha wakaomba, wakasema, Wewe, Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, tuonyeshe ni nani uliyemchagua katika hawa wawili,

25 ashike mahali katika huduma hii na utume huu, alioukosa Yuda, aende zake mahali pake mwenyewe.

26 Wakawapigia kura; kura ikamwangukia Mathiya; naye akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja”.

Unaona huo mstari wa 21 na 22, unatuambia Mathiya ni mtu aliyefuatana na mitume wa Bwana tangu siku za mwanzoni kabisa mwa huduma ya Yesu, mpaka siku ile ambayo Ananyakuliwa mbinguni. Japo kulikuwa na mabonde mengi na hatari nyingi za kuuliwa na wayahudi, lakini huyu Mathiya hakuacha kuongozana na Bwana pamoja na mitume wake, japo kuna wakati wanafunzi wengi walijitenga na Kristo na kurudi nyuma kutokana na mafundisho yake ambayo hawakuyaelewa, lakini huyu Mathiya hakurudi nyuma…Mahali ambapo wanafunzi wake waliacha kila kitu na kumfuata Yesu, Mathiya naye alifanya hivyo japo Kristo hakumuhesabia kama mmoja wa mitume wake 12.

Embu tengeneza picha siku ile Bwana YESU ametoka kusali ndio anakwenda kuwateua mitume wake 12 wa kufuatana naye, katikati ya wanafunzi wengi aliokuwa nao,..Kumbuka Huyu Mathiya naye alikuwa pale, na akamwona Bwana anampita hana habari naye anawafuata wanafunzi wengine..Ingekuwa ni wewe upo hapo ingekuwa ni rahisi kuvunjika moyo. Lakini yeye kutokuchaguliwa hakukumfanya ajione hastahili kuwa mwanafunzi wake, au asifuatane na Bwana..

Lakini hakujua kuwa kwa kujitoa kule, na kumpenda Bwana kule, kumbe tayari siku nyingi ameshaandikiwa kuwa atakuwa miongoni mwa wale mitume 12.. Lakini mpaka Bwana anaondoka hajawahi kumwambia jambo hilo.. Hilo linakuja kuthibitika kwa vinywa vya mitume wake, wakisapotiwa na maandiko haya..

Zaburi 109:8 “Siku zake na ziwe chache, Usimamizi wake na atwae mtu mwingine”.

Usimamizi wa Yuda ambaye alitiwa mafuta na Yesu mwenyewe, ambaye aliheshimiwa na Yesu, ambaye alikula meza moja na Yesu, hapa inachukuliwa na Mathiya.

Hata leo hii, huhiitaji Bwana akutokee kama ilivyokuwa kwa mitume, ili kukuthibitisha wewe unaweza kuwa ni mteule wake, huhitaji Bwana akupe maono Fulani ndio umtumikie, huhitaji upitie shule Fulani ya biblia ndio upate uthibitisho kuwa Mungu yupo na wewe..Bwana anachohitaji kwako ni uaminifu wako kwake, tangu siku ile ulipoitikia wito wa kuokoka, ili wakati wake ukifika akunyanyue kama Mathiya..

Bwana alikuwa na wanafunzi wengi sana, lakini si wote walidumu naye wakati wote, walikuwa wanakuja na kuondoka, wanakuja na kuondoka, lakini waliodumu kuanzia mwanzo hadi mwisho ni wawili tu yaani Mathiya na Yule mwingine aliyeitwa Yusufu kati ya mamia ya wanafunzi waliokuwa wanamfuata.. Kama tu vile Yoshua na Kalebu walivyoingia nchi ya ahadi wao tu kati ya mamilioni ya watu waliotoka Misri.

Na Mathiya kumbukumbu lake halitafutika milele.. Tunaposoma kitabu cha Ufunuo juu ya ule mji Mtakatifu Yerusalemu mpya ushukao kutoka mbinguni wenye misingi 12 na malango 12..Na katika misingi ile pameandikwa majina 12 ya wale mitume 12 wa Yesu, (Ufunuo 21:14) ..Sasa jina mojawapo ni la huyu Mathiya.

Lakini safari yake haikuibukia juu juu tu yaani siku ile ya kura, bali ilianzia mbali, tangu wakati wa Yohana mbatizaji..Vivyo hivyo na sisi, tumtii Kristo sasa, tuyatii maagizo yake yote anayotuelekeza hata kama hatutaona tofauti yoyote nje leo hii, lakini mwisho wa siku ataonyesha tofauti yetu tusipozimia mioyo.. Tukiokoka tusiishi kama watu ambao Mungu hawatambui, tujue kuwa siku moja ya wokovu wetu inathamani kubwa sana mbele za Mungu.

Ubarikiwe sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii 0789001312

Mada Nyinginezo:

VIFO VYA MITUME WA YESU/ JINSI MITUME WALIVYOKUFA.

JIFANYIE RAFIKI KWA MALI YA UDHALIMU.

JINSI BWANA ALIVYOWACHAGUA MITUME WAKE.

TIMAZI NI NINI

INGIENI KWA KUPITIA MLANGO ULIO MWEMBAMBA.

MIILI YA UTUKUFU ITAKUWAJE?

YONA: Mlango wa 4

TAZAMA, MWISRAELI KWELI KWELI, HAMNA HILA NDANI YAKE!

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
2 years ago

ameen