JE KUPONYWA NI UTHIBITISHO WA MUNGU KUWA NA WEWE?

JE KUPONYWA NI UTHIBITISHO WA MUNGU KUWA NA WEWE?

Shalom. Karibu tujifunze Biblia, ambalo ndio Neno la Mungu, Mwanga wa njia yetu na Taa iongozayo miguu yetu.

Biblia inasema…Mungu anawaangazia jua lake waovu na wema…(Mathayo 5:45), na anawanyeshea mvua yake wenye haki na wasio haki..Maana yake ni kwamba…Riziki Mungu anawapa watu wote…Hata mchawi akienda kupanda mbegu zake shambani kwake…Mungu atazinyeshea mvua na zitaota.

Sasa msingi wa Neno hili la “Yeye anawaangazia jua lake waovu na wema na kuwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki” ndio utakaotupa picha kamili kuelewa kwamba baraka yoyote, au upendeleo wowote tunaopokea kutoka kwa Mungu sio uthibitisho namba moja wa kuonyesha kwamba tupo sawa na Mungu au hatupo sawa na Mungu…Kwasababu kumbe baraka hizo hizo zinaweza kuwapata wote waovu na wema kwa pamoja…Ndio maana unaona leo hii hata waovu wanafanikiwa sana.

Sasa sio kwamba tuwe waovu ndio tuwe tumepata tiketi ya kubarikiwa…Hapana!..Biblia inasema..katika Zaburi 92:7 “Wasio haki wakichipuka kama majani Na wote watendao maovu wakistawi. Ni kwa kusudi waangamizwe milele”. Kwahiyo tusitafute kuwa waovu ili tufanikiwe.

Kadhalika Miaka ya watenda mabaya itafupishwa. Mtu mwovu atalifurahia jua kwa kitambo, ataifurahia neema kwa kitambo, ataufurahia wema wa Mungu kwa kitambo…lakini kifo kitamjia kwa ghafla.

Hivyo usifurahie kupata mafanikio fulani au baraka fulani, au kupata fursa fulani mbele yako baada ya kumwomba Mungu, na huku ndani ya moyo wako umemwacha Mungu ukayatafsiri mafanikio yale kama ni uthibitisho wa Mungu kupendezwa na wewe….kamwe usifanye hivyo!..kumbuka neno hili kuwa “Mungu anawanyeshea mvua waovu na wema”. Kwahiyo hata ukiwa mwovu hiyo haimzuii Mungu kukupa chakula.

Kadhalika usitafsiri majibu Mungu aliyokupa ya uponyaji..kwamba ulikuwa na ugonjwa fulani au tatizo fulani na ukamwomba Mungu naye akakuponya na wakati huo huo bado ni mlevi, mwasherati, kwamba uponyaji ulioupokea ni kwasababu Mungu amependezwa na wewe

Katika biblia kuna Mfalme mmoja ambaye alirasimisha ibada za sanamu katika Taifa la Israeli, mfalme huyo alikuwa anaitwa Yeroboamu…alitengeneza sanamu mbili za ndama akaziweka moja kaskazini mwa Israeli nyingine kusini, akawaambia Israeli wote kwamba sanamu hizo ndiyo miungu iliyowatoa wao Misri, hivyo wasiende Yerusalemu kuabudu bali wapande kwenda kuzisujudia sanamu hizo. Hivyo akawageuza mamilioni ya Wana wa Israeli mioyo na kuwafanya kuwa nusu-wachawi kwa muda mrefu kwa jinsi walivyokwenda kuziabudu sanamu hizo za ndama huko alikoziweka…

Na siku ya kuzivumbua sanamu hizo..alitengeneza madhababu juu yake na kutoa kafara…wakati anatoa kafara…akatokea nabii mmoja aliyetumwa na Mungu akatabiri mbele ya ile madhabahu kwamba siku inakuja ambayo itabomolewa na makuhani watakaohudumu katika hiyo madhabahu watachinjwa juu yake..Na huyu Mfalme alipomwona yule Nabii akanyosha mkono wake kutoa amri ya kukamatwa..Wakati anamnyooshea tu mkono wake…Ule mkono biblia unasema ukakatika …

Sasa maana yakukatika sio kwamba ulinyofoka na kuanguka chini hapana…bali maana yake ulikufa ule mkono…na ukakauka ukawa kama mkono wa maiti iliyokauka…ulikauka ukawa kama kijiti kikavu…ukawa hauna hisia hata kidogo..kama mkono uliopata kiharusi…Mfalme kuona vile akamwomba yule Nabii amwombee rehema kwa Mungu wake ili mkono wake urudi…na alipoombewa akapokea uponyaji wake siku hiyo hiyo na akaendelea na shughuli zake za kichawi…wala hakugeuka kubadilika..Na ndio Mfalme aliyefanya maovu kuliko wafalme wote waliowahi kutokea Israeli…yeye pamoja na mfalme Ahabu mumewe Yezebeli. Kasome 1Wafalme 12 na 13.

Sasa unaweza kuona huyu Mfalme alikuwa ni nusu-mchawi lakini katika uovu wake alimwomba Mungu amponye na Mungu akasikia na kumponya…na baada ya kuponywa aliendelea na Maisha yake ya ouvu…kwasababu alitaka tu apate uponyaji ili aweze kuendelea na maisha yake ya dhambi kama kawaida…… Sasa uponyaji alioupokea haukuwa uthibitisho wa kuwa Mungu amependezwa na yeye…Ni rehema za Mungu tu kwasababu yeye anawanyeshea mvua wenye haki na wasio haki…Lakini haimaanishi kuwa anapendezwa na wasio haki…Ndio maana huyu Mfalme Bwana alikuja kumwambia atakufa.

1Wafalme 14:10 “tazama, kwa hiyo mimi nitaleta mabaya juu ya nyumba yake Yeroboamu, nami nitamkatia Yeroboamu kila mwanamume, aliyefungwa na aliyeachwa katika Israeli, nami kuondoa nitawaondoa waliobaki wa nyumba yake Yeroboamu, kama mtu aondoavyo mavi, hata itakapokwisha pia”

Hiyo ndiyo imekuwa kawaida ya Mungu wetu…yeye huwanyeshea mvua waovu na wema…huwapa uponyaji makahaba na wasio makahaba endapo watamlilia, huwapa mali waovu na wasio waovu, huwanyanyua wenye haki na wasio haki..Hivyo kamwe usitumie kipimo cha wema wa Mungu juu yako kutafsiri uwepo wa Mungu katika Maisha yako…Hivyo ni vitu viwili tofauti.

Watakuwepo watu waliobarikiwa na mali kuzimu, watakuwepo watu walioponywa magonjwa yao na kuwa wazima kuzimu, watakuwepo watu kuzimu ambao waliofanyiwa mambo mengi mazuri na Mungu wakiwa duniani tena wakiwa ni waovu. Na wenye shuhuda nyingi tu, jinsi Mungu alivyowapigania katika mambo yao. N.k.

Uwepo wa Mungu juu ya Maisha yako unapimwa kwa maisha ya utakatifu unayoishi…Usifurahi umeponywa na huku bado unaendelea kuvaa vimini, Usifurahie unapata riziki kimiujiza na huku unakula rushwa, ukafikiri Bwana anapendezwa na wewe, usifurahie umetoka tu kuzini na mtu ambaye si mume wako, halafu kesho ukapata promosheni ya kupandishwa cheo kazini..ukadhani baraka hizo ni uthibitisho wa Mungu kupendezwa na wewe.

usifurahie uliombewa ukapona kansa na huku bado umemwacha mke wako au mume wako na unadhani Mungu yupo na wewe!..Usifurahie ulifunga siku kadhaa ukamwomba Mungu akupe nyumba na kweli akakupa na huku bado Maisha yako hutaki kujitakasa ukahitimisha kwa muujiza ule Mungu anapendezwa sana na wewe ndio maana akakuponya, au akakupa hiki au kile…kumbuka yeye anawanyeshea mvua waovu na wema…hivyo sio jambo kubwa sana yeye kukupa uponyaji wake angali ukiwa bado na ukahaba wako…Lakini usipotubu…Neno lake lipo pale pale..waasherati na wafiraji, na wezi, na waabudu sanamu, na wachawi, sehemu yao ni katika lile ziwa la Moto.

1Wakorintho 6:9 “Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? MSIDANGANYIKE; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,

10 wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi”.

Bwana akubariki sana…ikiwa hujamkabidhi Yesu Kristo Maisha yako..fanya hivyo leo angali tunao bado huu muda mchache…

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii 0789001312

Mada Nyinginezo:

UNAWAFAHAMU MANABII WA UONGO?

Ni sahihi kumuita Mariamu mama wa Mungu?

JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.

USIPOKUWA MWAMINIFU, NAFASI YAKO ITACHUKULIWA.

Biblia ni nini?

SAYUNI ni nini?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments