SWALI: Ninafahamu kwamba, watu waliokua wanakusanya vitabu/maandiko matakatifu kwa lengo la kuandaa BIBLIA, walikua wakiongozwa na ROHO MTAKATIFU Mwenyewe. Ili kitabu au maandishi yachaguliwe, waliangalia vigezo gani?-sababu na sikia, kuna baadhi ya vitabu havikuchukuliwa -Mfano Injili ya petro , na ya Tomaso.
JIBU: Hiyo ipo wazi kabisa kila kitabu cha biblia cha mwandishi yoyote tunayemsoma kimevuviwa na Roho Mtakatifu, hali kadhalika pia kuwepo kwa idadi ya vitabu 66 katika biblia hilo nalo ni tendo lililovuviwa na Roho Mtakatifu na wala sio wazo la kibinadamu kama wale ambao sio-wakristo wanavyofikiri. Ni mpango ambao Mungu alishaupanga kabla hata ya kuwekwa misingi ya dunia. Lakini siku zote Mungu huwa anamtumia “mtu” kutenda kazi japo sio kwamba hawezi kutenda pasipo hao hapana bali huo ni utaratibu wake tu aliojiwekea yeye(ndivyo ilivyompedeza).
Sasa tukirudi katika agano la kale, kukusanywa vitabu vile vyote 39, Mungu alitia hekima kwa wayahudi washindania Imani wakati ule,waliomcha Mungu, waliokuwa wasomi na wafuatiliaji wazuri wa unabii na historia ya taifa la Israeli kwa ujumla, hivyo kwao haikuwa kazi kubwa, kuvihakiki vitabu vya manabii waliowatangulia, Hivyo wale waliokubalika na habari zao zilithibitika kuja kutokea kweli,.Kwamfano vitabu vya torati ya Musa, ni vitabu ambavyo havikuwa na tashwishwi yoyote kwa wayahudi kwani ni vitabu vinavyoeleza chimbuko lao na vimepita kizazi hadi kizazi havijapotea tangu siku vilipoandikwa.. Vile vile Ukiangalia vitabu kama Esta,Ruthu,Wafalme, n.k. ni vitabu vya historia ambavyo vinaeleza habari zilizohalisi kabisa, vile vile vitabu vya manabii kama Isaya, Yeremia,Danieli vyote hivyo ni vitabu vilivyothibitika kuwa ni Vitabu vya wakati wote, na unabii wake ni thabiti ambao watu walikuwa wanawaona. Na kwa kuzingatia hayo ndio vikapatikana vile vitabu 39 vya Agano la kale. Lakini katika agano jipya, utaona kulikuwa pia kuna vitabu ambavyo vilishakubalika tangu kanisa la kwanza.
Kwamfano nyaraka za mtume Paulo zilikuwa zinatumiwa tayari na watakatifu wa makanisa yote yaliyokuwa Asia wakati ule kabla hata yeye hajaondoka, nyaraka zake zilikuwa zinazungushwa toka kanisa hadi kanisa..tunasoma hilo katika
Wakolosai 4:16 “Waraka huu ukiisha kusomwa kwenu fanyeni kwamba usomwe katika kanisa la Walaodikia pia; na ule wa Laodikia usomwe na ninyi”…
Kwahiyo haikuwa ngumu kuendeleza utaratibu huo mpaka kwa makanisa ya mbeleni. Vile vile utaona mtume Paulo, pia akirejea baadhi ya vifungo ambavyo vilikuwa katika vitabu vya Injili mfano Injili ile ya Luka, soma (1Timotheo 5:18b,linganisha na Luka 10:7) utalibitisha hilo kuwa kumbe hata Paulo alishapokea vitabu vya Injili kama sehemu ya maandiko matakatifu ya kurejea hiyo ni kuonyesha kuwa vitabu vya Injili vilikuwa tayari vimeshapokewa kama sehemu ya maandiko matakatifu ya wakati wote tangu kanisa la kwanza. Sasa baadaye watu kama wakina Klementi wa Rumi , Ignatusi wa Antiokia na Polikapi na wengine wakaja kutaja vitabu vingine. Na baadaye tena mabaraza kadhaa yaliitishwa ili kuthibitisha Uvuvio wa vitabu hivyo Na vigezo walivyokuwa wanatumia, ni kama vifuatavyo..
1) cha kwanza je! Mwandishi wa kitabu husika alikuwa ni mtume au alikuwa na uhusiano wa karibu na mitume.
2) Je! Kitabu husika kinakubalika na kanisa kwa ujumla.
3) Je! Kitabu kinabeba mafundisho halisi na ya msingi (kumtambua Yesu Kristo kama kiini cha Imani)?
4) Je! Kitabu hakivunji miiko na kanuni za rohoni ambazo zinathibitishwa na kazi ya Roho Mtakatifu mwenyewe?.
5) Kitabu lazima kiwe kwa sehemu Fulani kimenukuu vitabu vingine vya agano la kale..Kwamfano unaona nyaraka za Paulo nyingi zilinukuu vitabu vya Zaburi,Ayubu na Mwanzo.. Hivyo baraza la mwisho ambalo lilihitimisha kuwepo kwa vitabu 66 vya Biblia vilivyovuviwa, lilifanyika mwaka 397WK. Na ndio vitabu tulivyonavyo sasa. Lakini kumbuka kama tulivyosema kazi ya vitabu vya biblia kuwa 66 sio mwanadamu alipanga, hata ingekuwaje, kwa namna yoyote ile, kwa kupitia hatua hizo au nyingine zozote biblia ingetufikia tu kwa ukamilifu wake wote.
Ubarikiwe.
Mada Nyinginezo:
KITABU CHA YASHARI KINACHOZUNGUMZIWA KATIKA 2SAMWELI 1:17-18, NI KITABU GANI?
VITABU VYA BIBLIA: SEHEMU YA 1
NI KWA NAMNA GANI TUTASHINDA MAJARIBU?
NJIA MUNGU ALIYOIWEKA KWA KILA JAMBO:
UNAMCHUKULIA YESU KWAKO KAMA NANI?
UMEIZALIA MATUNDA MIAKA 4 YA NEEMA ULIYOPEWA?
Rudi Nyumbani:
Print this post
je kutoa fungulakumi kwenye bahasha nisawa?