SI KWA UWEZA WALA KWA NGUVU BALI KWA ROHO YANGU, ASEMA BWANA.

by Admin | 17 May 2021 08:46 pm05

Zekaria 4:6 “Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi”.

Shalom.

Yapo mambo utatumia nguvu kuyatimiza/kuyafanikisha lakini hayatatimia, vile vile yapo mambo ambayo utatumia uwezo ulionao au alionao mtu mwingine kuyatimiza lakini vile vile hayatatimia wala kufanikiwa, yatabaki kuwa changamoto kubwa sana kwako. Ukishafikia hicho kipindi/au huo wakati ni vizuri kujifunza njia nyingine sahihi na iliyo bora ya wewe kutatua matatizo yako. Na hiyo si nyingine Zaidi ya kumtumia Roho Mtakatifu.

Sasa kumtumia Roho Mtakatifu, hatumtumii kama vile tunavyotumia jina la Yesu. Hapana! Tutakuja kuona ni kwa namna gani tunamtumia Roho Mtakatifu mbele kidogo mwa somo hili, lakini sasa hebu tukisome hichi kisa ambacho kitatusaidia kuelewa vizuri kiini cha somo letu.

1Wafalme 19: 11 “Akasema, Toka, usimame mlimani mbele za Bwana. Na tazama, Bwana akapita; upepo mwingi wa nguvu ukaipasua milima, ukaivunja-vunja miamba mbele za Bwana; LAKINI BWANA HAKUWAMO KATIKA UPEPO ULE; na baada ya upepo, tetemeko la nchi; LAKINI BWANA HAKUWAMO KATIKA LILE TETEMEKO LA NCHI;

12 na baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto; LAKINI BWANA HAKUWAMO KATIKA MOTO ULE; na BAADA YA MOTO SAUTI NDOGO, YA UTULIVU.

13 Ikawa, Eliya alipoisikia, alijifunika uso wake katika mavazi yake, akatoka, akasimama mlangoni mwa pango. Na tazama, sauti ikamjia, kusema, Unafanya nini hapa, Eliya?.

Katika hatua hizo Nne ambazo Eliya alidhani atapata suluhisho la majibu yake, tunaona ni njia moja tu ya mwisho ndio uliyompatia jibu, nyingine zote hazikuwa na msaada, ingawa zilikuwa na udhihirisho mkubwa. Tunaona katika upepo mkali Bwana hakuwepo, katika tetemeko kubwa Bwana hakuwepo, katika Moto Bwana pia hakuwepo…lakini katika Sauti Ndogo ya Utulivu ya Roho Mtakatifu ndipo Mungu alipokuwepo na akazungumza na Eliya, na kumpa suluhisho la mambo yake.

Tunaloweza kujifunza hapo ni kwamba, Sauti ya Roho Mtakatifu ndani yetu ndio suluhisho la mambo yote. Na wala si misisimko na mitikisiko na matetemeko.

Roho Mtakatifu anapokuwa ndani yako.. Ndio jibu la mafumbo yote, kwa sauti yake ya utulivu ndio inayotatua matatizo yote. Ndio maana Wakati Zerubabeli anaona ni jambo zito na gumu, kumjengea Mungu nyumba katikati ya maadui, tena jambo hilo aliliona kama Mlima Mkubwa sana mbele yake…Lakini Bwana alimwambia maneno yale…

Zekaria 4:6 “ Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi.

7 Nani wewe, Ee mlima mkubwa? Mbele ya Zerubabeli utakuwa nchi tambarare; naye atalileta lile jiwe la kuwekwa juu kabisa pamoja na vigelegele vya, Neema, neema, ilikalie.”

Mlima huo Mkubwa Zerubabeli aliouona mbele yake, Bwana anasema utakuwa nchi tambarare..Lakini si kwa uwezo wala kwa nguvu, bali kwa Roho yake.

Je na wewe una mlima mkubwa mbele yako?, kiasi kwamba hujui utafanya nini?.. Suluhisho ni rahisi sana, Mpokee Roho Mtakatifu ndani yako?, huyo atakupa maelekezo sahihi ya maisha na utaona huo mlima mkubwa unageuka na kuwa nchi tambarare mbele ya macho yako. Hutahitaji kutumia nguvu nyingi kuusambaratisha huo mlima mkubwa uliopo mbele yako,bali ni vizuri utumie jitihada kumpata Roho Mtakatifu, atakayekuwezesha kulitoa tatizo lililoko mbele yako kiwepesi.

Sasa unampokeaje Roho Mtakatifu?.

Biblia imetupa jibu…

Matendo 2:37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

38 Petro akawaambia, TUBUNI MKABATIZWE KILA MMOJA KWA JINA LAKE YESU KRISTO, MPATE ONDOLEO LA DHAMBI ZENU, NANYI MTAPOKEA KIPAWA CHA ROHO MTAKATIFU.

39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”

Unapotii maagizo yake kwa kutubu, na kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi, hapo Roho Mtakatifu anaingia ndani yako kukutia muhumi (Waefeso 4:30)

Na Unapompokea Roho Mtakatifu na kumtii maagizo yake ndani yako, hapo ndipo umemtumia Roho Mtakatifu. Na hivyo hakuna mlima wowote utakaoweza kusimama mbele yako.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

Mlima Gerizimu na Ebali ni ipi, na umuhimu wao rohoni ni upi?

Mlima wa Mizeituni  unaumuhimu gani kwetu?

Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/05/17/si-kwa-uweza-wala-kwa-nguvu-bali-kwa-roho-yangu-asema-bwana/