by Admin | 20 May 2021 08:46 am05
1Wakorintho 12:3 “Kwa hiyo nawaarifu, ya kwamba hakuna mtu anenaye katika Roho wa Mungu, kusema, Yesu amelaaniwa; wala hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu.”
Katika hali ya kawaida kila mtu anaweza kusema “Yesu ni Bwana”, hata watu wa kidunia, wanaweza kulitamka hilo neno, lakini wasiwe wamemaanisha, au wamejua uzito wake, wakawa wamelitaja tu.. Lakini kwa mtu ambaye amempokea Roho Mtakatifu, na kufunuliwa kwa Roho kuwa Yesu ni nani, kwanini amekuja duniani, kwanini amwage damu yake, afe na kufufuka, na yupo wapi sasahivi?..Mtu wa namna hiyo kama akitamka “Yesu ni Bwana”,… kutamka kwake kunakuwa na maana sana na nguvu kubwa. Kwasababu amekutamka katika Roho.
Hivyo Mtu anayetaja “Yesu ni Bwana” katika Roho Mtakatifu ni lazima atakuwa ni mtakatifu, kwasababu amemjua Mungu, kadhalika atakuwa anamheshimu Mungu na kumwogopa, kutokana na ufunuo mzito alioupata kumhusu Yeye (Yesu).
Lakini Yule anayesema tu “Yesu ni Bwana” bila Roho, maana yake hamjui Yesu, hana mpango na maneno yake, hana ufunuo wowote alioupata unaomfanya yeye aseme hivyo, mtu wa namna hiyo kutamka kwake hakuna manufaa yoyote, ndio maana hapo biblia inasema.. “mtu hawezi kusema Yesu ni Bwana isipokuwa katika Roho Mtakatifu”..maana yake atakuwa anasema tu kimdomo, na si kwa kuelewa na kumaanisha.
Bwana Yesu alisema maneno haya…
Mathayo 7:21 “SI KILA MTU ANIAMBIAYE, BWANA, BWANA, ATAKAYEINGIA KATIKA UFALME WA MBINGUNI; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.
22 Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?
23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”
Umeona?.. Kusema tu “Yesu ni Bwana” bila ya kuwa na badiliko halisi la ndani, ambalo hilo linaletwa na Roho Mtakatifu mwenyewe, ni kazi bure!.. Vile vile huwezi kuwa na Roho Mtakatifu halafu useme Bwana Yesu kalaaniwa.. hilo haliwezekani.
Hivyo ili tuyafanye mapenzi ya Mungu, na maneno ya midomo yetu pamoja na sala zetu zikubalike mbele za Mungu, hatuna budi kuzaliwa mara ya pili, na kuzaliwa mara ya pili kunakuja kwa kutubu dhambi, kwa kumaanisha kuziacha, na kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi pamoja na kupokea Roho Mtakatifu.
Baada ya hapo, lolote tunalolitamka la kumwadhimisha Mungu, kumsifu, kumwomba, na kumkiri linakuwa katika Roho, na hivyo linaleta matokeo makubwa sana. Lakini kama hatutatubu kwa kumaanisha kuacha dhambi, hata sala zetu zinakuwa ni bure, hata sifa zetu kwake zinakuwa ni bure…
2Timotheo 2: 19 “Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, Bwana awajua walio wake. Na tena, Kila alitajaye jina la Bwana na auache uovu”
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Kwanini Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake wasichukue chochote isipokuwa fimbo tu?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/05/20/biblia-imemaanisha-nini-iliposema-hawezi-mtu-kusema-yesu-ni-bwana-isipokuwa-katika-roho-mtakatifu/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.