by Admin | 10 June 2021 08:46 am06
Nakusalimu katika jina kuu sana la mwokozi wetu Yesu Kristo. Karibu tuyatafakari maandiko maadamu siku ile inakaribia.
Tukitazama matukio yaliyokuwa yanaendelea pale msalabani yapo mambo kadha wa kadha tunaweza kujifunza. Kwamfano siku ile utaona walimvua nguo zake zote, wakazigawanya mafungu manne, kila askari fungu lake. Hii ikiwa na maana kuwa Bwana Yesu alisulibiwa akiwa uchi kabisa, hakutuonea haya sisi, iweje sisi tumwonee haya yeye?
Lakini wale askari walipofika kwenye Kanzu yake nayo, kwasababu ilikuwa ni ya Tano, na wenyewe walikuwa ni wanne, na kila mmoja alitaka apate sehemu ya vazi lile..Wakaona njia rahisi ni kuligawanywa, walau kila mtu apate kipande chake.
Lakini lile vazi lilikuwa ni la kitofauti sana, lilikuwa halijashonwa kwa kuunganishwa vipande mbalimbali hapana.Bali Lote tokea juu hadi chini lilikuwa ni vazi moja, kiasi kwamba kulikuwa hakuna sehemu lilikuwa na kipande kilichojitegemea kikaunganishwa nalo hapana. Unaweza kutazama mfano wa vazi hilo kwenye picha juu.
Hivyo wale askari walipotafuta walau, maungio ya vazi lile ili wawezi kukata wagawane kila mtu kipande chake hawakuona. Pengine walitafuti kwenye mikono hawakuona, kwenye kola hawakuona, kwenye mfuko hawakuona. Mwishoni wakaona ni heri walipigie tu kura, ili liwe la mmojawapo.
Yohana 19:23 “Nao askari walipomsulibisha Yesu, waliyatwaa mavazi yake, wakafanya mafungu manne, kwa kila askari fungu lake; na kanzu nayo. Basi kanzu ile haikushonwa, ilikuwa imefumwa yote pia tangu juu.
24 Basi wakaambiana, Tusiipasue, lakini tuipigie kura, iwe ya nani. Ili litimie andiko lile linenalo, Waligawanya nguo zangu, Na vazi langu wakalipigia kura. Basi ndivyo walivyofanya wale askari”.
Lakini tunaposoma habari hiyo ni jambo gani Mungu anataka tujue? Je! Ni mambo ya mavazi yake tu kupigiwa kura tu au ni nini?
Ujumbe mkuu Mungu anataka tuone hapo ni kwamba VAZI LA YESU HALIGAWANYI.. Kwasababu halija ungwaungwa, kama mengine yalivyo. Kama utalihitaji ni sharti ulichukue lote, au uliharibu kabisa, hakuna namna..
Hata sasa, mtu yeyote anayeamua kuwa mkristo, hana budi alivae vazi hili. Ambalo haliungwi ungwi.. Ndilo linalojulikana kama VAZI LA WOKOVU, Tunalolisoma katika
Isaya 61:10 “Nitafurahi sana katika Bwana, nafsi yangu itashangilia katika Mungu wangu; maana AMENIVIKA MAVAZI YA WOKOVU, AMENIFUNIKA VAZI LA HAKI, kama bwana arusi ajipambavyo kwa kilemba cha maua, na kama bibi arusi ajipambavyo kwa vyombo vya dhahabu.
Unapolivaa vazi hili ni lazima UUISHI wokovu wote, huwezi kuyakwepa maisha ya utakatifu.. Wakristo wengi wanatafuta kuligawanya vazi la wokovu wawe nalo kwa sehemu tu, hawataki kujitoa kikamilifu kwa Mungu pale wanapookoka. Wanataka waitwe wanakwaya, lakini bado waendelee na uzinzi kwa chini chini, wanataka waitwe vijana waliokoka, lakini waendelee kwenda disco, wavae vimini, na milegezo, na viduku, Wanadhani, hilo jambo linawezekana katika wokovu. Ni kweli litawezekana kwenye dini zao, na madhehebu yao, lakini kwa KWA YESU hilo jambo halipo.
Ndugu, watakaokwenda kwenye UNYAKUO, watakuwa wale tu walio tayari kulichukua vazi lote la Yesu, hao ndio wanaojulikana kama BIBI-ARUSI wa Kristo. Lakini tukijidanganya kuwa tumeokoka, halafu bado tupo nusu nusu, hatueleweki sisi ni wa upande upi, ipo wazi kuwa wakati ule tatabaki tu hapa duniani kwenye dhiki kuu ya mpinga-Kristo, na kama hutakuwa hai, basi utaendelea kubakia makaburini mpaka siku ile ya ufufuo itakapofika uhukumiwe uende motoni.
Ufunuo 19:7 “Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari.
8 Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing’arayo, safi; KWA MAANA KITANI NZURI HIYO NI MATENDO YA HAKI YA WATAKATIFU”.
Naamini utakuwa unatambua kuwa tunaishi katika kanisa la Laodikia, na uvuguvugu na tabia ya kanisa hili ni kuwa lipo Vuguvugu, tofauti na yale mengine. Hivyo Bwana atuepushe na uvuguvugu huu uliopo duniani leo.
Maran atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Nini maana ya “mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili”?
kwanini yule kijana aliitupa ile nguo ya kitani chini na kukimbia uchi?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/06/10/vazi-la-yesu-haligawanywi/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.