by Admin | 11 June 2021 08:46 am06
Kuna silaha ambazo nataka ufahamu shetani anazozitumia kwa watu ambao wanakaribia kuokoka, au waliookoka lakini bado ni wachanga katika imani. Silaha hizo, zimewafanya watu wengi waishi katika hofu, na misongo mikubwa ya mawazo, mimi nikiwa mmojawapo kabla sijaokoka.
Nataka nikuambie mawazo haya yakikujia, yakatae kwa nguvu zako zote, kwasababu ni vita vya kifikra ambavyo shetani na majeshi yake ya mapepo wanavyoleta ili kukuangusha uiche imani, au usisonge mbele. Narudia tena usiruhusu hata kidogo mawazo hayo yakutawale;
1) Umemkufuru Roho Mtakatifu:
Hii ndiyo silaha ya ibilisi ya kwanza ; Anakuletea mawazo kuwa wewe huwezi kusamehewa, kwani dhambi yako ni ya kumkufuru Roho Mtakatifu. Na anaweza kukurushia mpaka hayo mawazo ya namna hiyo ili ujione wewe tayari dhambi yako imeandikwa kwa kalamu ya chuma.
Nataka nikuambie, huo ni uongo tu, dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu haiji hivyo. Na kamwe mtu aliyemkufuru Roho hata hofu na Mungu hana ndani yake, ni mfano wa mafarisayo na masadukayo ambao walikuwa wanazipinga kazi za Roho Mtakatifu wazi wazi na kuzishuhudia hadharani kuwa ni za mapepo wakati wanaujua kabisa ukweli kwamba na Roho Mtakatifu ndiye aliyekuwa anafanya kazi zile (Mathayo 12:24-32).
Sasa jiulize wewe ni lini ulishawahi kwenda kuzipinga kazi za Roho Mtakatifu huku ukajua kabisa ndio yeye, halafu ukatoa maneno ya kufuru na kusema zile ni kazi ya mapepo..Ulishawahi kufanya jambo kama hilo mbele ya kadamnasi? Ni wazi kuwa hujawahi kufanya.. Sasa hayo mawazo ya wewe umemkufuru Roho Mtakatifu yametoka wapi kama sio kwa shetani?
Watu wengi, nimewasiliana nao, wamekuwa wakisumbuliwa na mawazo mkandamizo kama hayo, Lakini leo nataka nikuambie Usiogope, hiyo ni ishara kuwa Mungu yupo karibu na wewe sana, unachopaswa kujua ni kufahamu ile kweli, ili ikuweke huru kweli kweli.
2) Bado hujaokoka:
Unaweza ukawa umetubu kweli dhambi zako kwa kudhamiria kuziacha, na ukabatizwa katika ubatizo sahihi, na baada ya hapo ukaanza kuishi maisha yanayompendeza Mungu, Lakini kipindi fulani kikapita shetani akakuletea mawazo kwamba bado hujaokoka, wanaookoka hawawi kama wewe. Mawazo kama haya, yakatae, Bwana Yesu alisema, “Hakuna mtu anayeweza kwenda kwake, kama Baba yake hajamvuta kwake (Yohana 6:44)” Hivyo mpaka wewe umefikia hatua ya kutubu, na kubatizwa na kuanza kuonyesha bidii ya kuishi sawasawa na mapenzi yake, haikuwa kwa akili zako, bali ni Yesu mwenyewe alikuvuta.
Hivyo songa mbele, zidi kujitakasa siku baada ya siku, mpaka kuufikia ukamilifu kwasababu Yesu yupo pamoja na wewe.
3) Umeshachelewa:
Hili ni jambo lingine ambalo, limewadhoofisha wengi. Wanadhani elimu ya kidunia ni sawa na elimu ya ufalme wa mbinguni. Elimu ya kidunia, ukishakuwa mtu uzima na hujaenda shule, unaweza ukaonekana kama umeshachelewa. Duniani ukifikisha umri fulani hujaolewa, au hujapata kitu fulani umeshachelewa. Lakini kwa Mungu haiendi hivyo, maadamu pumzi ya uhai ipo ndani yako bado hujachelewa kumtumikia yeye.
Mungu anakutazama, ufanye vizuri isipokuwa tu uonyeshe bidii, ili ufanye vizuri kuliko hata wale ambao walikuwepo tangu zamani. Embu mkumbuke mtume Paulo, hakuwa miongoni mwa wale 12, wala siku ile ya Pentekoste hakuwepo. Lakini alikuja kufanya kazi kubwa kuliko wote waliomtangulia.
Ukumbuke pia ule mfano wa mwajiri na waajiriwa ambao Bwana Yesu aliutoa, akasema kulikuwa na wengine ambao walikutwa jioni kabisa hawana kazi yoyote, wakaambiwa waende shambani, na kule shambani walipomaliza shughuli yao, wakalipwa sawa sawa na wale wengine, ambao walikuwa tangu asubuhi shambani.(Mathayo 20:1-16). Na ndio maana Bwana Yesu akamalizia na kusema “wapo walio wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wale wa kwanza watakuwa wa mwisho”.
Vivyo hivyo na wewe, ikiwa umeitwa kwenye miaka ya 20, au 30 au 40 au 50 au 80. Hujachelewa popote pale. Mtumikie Bwana kwa moyo wako wote na kwa uaminifu. Na thawabu yako inaweza kuwa kubwa kama tu ile ya mitume.
4) Mungu hawezi kupendezwa na wewe:
Haya mawazo yanakuja hususani pale ambapo pengine hukutumiza wajibu wako fulani uliloambiwa na Mungu ufanye, au ulifanya dhambi fulani ambayo ilikuwa ni ya makusudi kabisa kwa Mungu, pengine ulivunja viapo vya ndoa yako ukaenda kuzini, au uliua mtu, au uliiba n.k..
Nataka nikuambie kama umetubu tayari kwa kumaanisha kutoka katika moyo wako. Basi usiruhusu tena hayo mawazo yawe ndani yako, kukutawala. Mrudie Mungu wako, mtumikie kwa bidii, kwani kumpendeza tena kunawezekana, na akawa rafiki yako, zaidi hata ya pale mwanzo kama utatii. Daudi alizini ni mke wa Uria, lakini alitubu, hata baada ya kuadhibiwa na Mungu, aliendelea kumtafuta Mungu wake, na mwisho wa siku bado akawa mtu ambaye ameupendeza moyo wa Mungu.
5) Fulani ni bora kuliko wewe mbele za Mungu:
Haya ni mawazo mengine ya ibilisi, kukukandamizi tu usipige hatua, kwamba fulani ni zaidi yako wewe mbele za Mungu. Hilo jambo halipo, Mungu hana utaratibu huo wa kulinganisha watu.Yeye huwa anasimama katika utaratibu wake. Ni sawa na mwalimu anayesahihisha mitihani, hasahishi kwasababu fulani ni machachari kuliko wengine, hapana, bali kwasababu amejibu sawasawa na alichotaka.
Ndivyo ilivyo kwa Mungu, hana habari na sura ya mtu, ikiwa wewe utatembea katika njia zake, basi atakuwa rafiki kwako, wala hakulinganishi na mtu mwingine aliye juu yako au aliye chini yako, na Yule mwingine hamlinganishi na wewe, bali wote anawalinganisha na Neno lake, kila mmoja kivyake.
Hivyo na wewe tembea katika njia yako, na Mungu wako, acha kujilinganisha na fulani, jilinganishe na biblia. Vinginevyo shetani atakuletea mikandamizo ya mawazo ukashindwa kumtumikia Mungu kwa ufanisi, kwa kumwona fulani tayari ni mtiwa mafuta wa Bwana, wewe huwezi kumfikia yeye.
Mawazo kama hayo yakatae.
Kumbuka, kuingia katika wokovu ni kurahisi sana, lakini kudumu kunakuwa kugumu, na hiyo yote inasababishwa na shetani na mapepo yake, Na dawa ya shetani sio tu kuomba, bali pia kulijua NENO. Nikisema Neno, sio kukariri vifungu vya biblia hapana, bali kupata ufunuo wa Neno la Mungu katika maisha yako ya kila siku.
Bwana Yesu alimshinda shetani kwa Neno kule jangwani, vivyo hivyo na wewe. Mungu anaweza akawa ameshakupa uhuru, lakini kama hutakuwa na maarifa ya kutosha ya kuupigania uhuru wako, bado ibilisi atakusumbua hata kama umeokoka. Maombi ya kufunguliwa pekee hayawezi kukufanya kuwa huru.. Kama ni hivyo Bwana Yesu asingesema..Mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru” (Yohana 8:32)Umeona kinachokamilisha uhuru wa mtu ni KWELI, na KWELI ni Neno la Mungu. (Yohana 17:17)
Hivyo jitahidi sana, uwe mtafakariji wa Neno. Ili ujue nafasi yako kwa Mungu ni ipi, wakati huu ni wakati wa vile VITA vikali ambavyo, Danieli alionyeshwa, katika (Danieli 10:1). Si vita tena vya kimwili, bali vita vya kifikra vinavyoletwa na ibilisi na mapepo yake.
Kama hujatubu, nafasi bado unayo. Tubu sasa mgeukie muumba wako, kisha ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako, ikiwa hukufanya hivyo. Na baada ya hapo Mungu atakupa Roho wake Mtakatifu atakayekusaidi kuifahamu kweli yote ili uwe huru (Yohana 16:13).
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
SI KWA UWEZA WALA KWA NGUVU BALI KWA ROHO YANGU, ASEMA BWANA.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/06/11/ukiokokahizi-fikra-zikija-ndani-yako-zikatae/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.