AHADI YA ROHO ILIYOSALIA SASA KWA KIPINDI CHETU.

by Admin | 17 June 2021 08:46 am06

Kufahamu huduma za Roho Mtakatifu wakati huu ni kugumu kwa wakristo, kama ilivyokuwa kufahamu huduma ya Yesu Kristo kwa wayahudi wakati ule. Wayahudi walimtazamia Kristo aje kama mfalme tu, Wakishikilia baadhi ya vifungu tu kama vile Isaya 9:6 na huku vingine wakiviacha nyuma. Hivyo pale alipokuja kama mwana-kondoo achinjwaye achukuaye dhambi za ulimwengu (sawasawa na Isaya 53) wakapoteza shabaha kabisa, na matokeo yake wakampinga wakasema huyu siye Masihi. Sisi tunafahamu masihi atakuja katika ukuu wa kifalme kama vile Daudi ili kutuokoa na maadui zetu.

Vivyo hivyo hata leo watu wengi wakisikia Roho Mtakatifu wanachojua ni kunena kwa lugha tu, halafu basi..Hawajui kazi nyingine za Roho Mtakatifu ni zipi katika kanisa, hawajui agenda yake ni ipi kwa wakati wetu huu tunaoishi sasa.

Leo tutatazama kazi ambazo Roho Mtakatifu anatarajia kuzitenda katika siku hizi za mwisho..

Ukisoma Ufunuo 1:4 inasema..

Ufunuo 1:4 “Yohana, kwa yale makanisa saba yaliyoko Asia; Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwake yeye aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja; NA ZITOKAZO KWA ROHO SABA WALIOKO MBELE YA KITI CHAKE CHA ENZI;”

Hapo utaona zikitajwa Roho saba za Mungu.. Sasa kiuhalisia Mungu hana roho saba, Mungu anayo Roho moja tu, ambaye ndiye Roho Mtakatifu. Lakini hapa tunaonyeshwa zikiwa saba, maana yake ni kuwa, Hizo ni SURA SABA, za Roho Mtakatifu, au HUDUMA /UTENDAJI KAZI saba wa Roho Mtakatifu.

Na utendaji kazi wake huu, ulianza kufanya kazi rasmi siku ile ya Pentekoste, na ukaendelea kutembea kwenye yale makanisa saba ambayo tunayasoma katika kitabu cha Ufunuo 2&3, kwa hizo Roho saba za Mungu..Ambapo tunajua kabisa kwa majira yakibiblia sisi tupo katika lile la mwisho la saba, lijulikanalo kama LAODIKIA.  Na kanisa hili kulingana na kalenda ya ki-Mungu lilianza mwaka wa 1906.

Mpaka hapo tunaweza kuona kabisa  kuwa sisi tunaongozwa na ile Roho ya Saba ya Mungu.

Sasa ni vizuri kujua jambo moja, kwa kawaida kitu cha kwanza na cha mwisho huwa vinakuwa na nguvu za kipekee na za kitofauti, msingi wa nyumba na finishing ya nyumba huwa vinatumia gharama kubwa sana.. Vilevile katika riadha mwanzo wa kukimbia na mwisho wa kukimbia huwa kunakuwa na ushindani sana, na ndio maana utaona wakimbiaji wengi wakikaribia kufika mwisho badala ya kupunguza mwendo utaona ndio wanaongeza nguvu zaidi.

Vivyo hivyo na utendaji kazi wa Roho Mtakatifu  kwa haya makanisa saba, kanisa la kwanza na la mwisho Roho Mtakatifu anafanya kazi kwa namna ya kipekee sana.. Alianza kwa nguvu nyingi sana na udhihirisho mwingi sana, wakati ule wa Pentekesto, kanisa la kwanza lilipoanza.. Na Vivyo hivyo atamaliza kwa nguvu nyingi na udhihirisho mwingi zaidi hata kuliko ule wa kwanza, kwa kanisa hili la mwisho la Laodikia.

Biblia inatuambia kipindi kile Mungu aliwatumia mitume wake, kufanya miujiza ya kupita kawaida, soma (Matendo 19:11). Na matokeo yake injili yao ikaenea ulimwenguni kote kwa kipindi kifupi sana. Miujiza kama ile iliyofanywa na mitume, mingi ya hiyo haikuwahi kutendeka kwa nyakati nyingine zilizofuata, kwasababu nyakati zilizofuata Roho Mtakatifu alitembea katika Uso mwingine na sio wa ishara na miujiza tena kama ilivyokuwa kwa kanisa la kwanza la mitume, hata zile karama za Roho nyingi hazikuonekana kwa hayo makanisa yaliyofuata. Soma historia ya kanisa utalithibitisha hilo.

Lakini tulipoingia katika kanisa hili la mwisho la Laodikia, ambalo lilianza mwaka wa 1906, Mungu alianza kuyarejesha tena yale ya mwanzo kama kipindi kile cha mitume. Karama za Roho zilianza kudhihirika kuonyesha kuwa Yule Roho wa SABA, ameanza kutenda kazi  katika uvuvio ule ule wa kama kanisa la kwanza. Na ndio maana utaona leo hii kutokana na udhihirisho wa karama za Mungu kuwa nyingi hata machafuko yamekithiri katika kanisa, manabii wa uongo wametokea humo humo, wengine wakigeuza karama za Mungu kuwa biashara na umaarufu.

Lakini ipo sehemu ya pili ambayo Roho Mtakatifu ameihifadhi kwa ajili ya WATUMISHI WAKE tu walio waaminifu. Na sehemu hiyo tunaweza kuisoma katika maandiko haya.

Yoeli 2:28 “Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono;

29 TENA JUU YA WATUMISHI WENU, WANAUME KWA WANAWAKE, KATIKA SIKU ZILE, NITAMIMINA ROHO YANGU.

30 Nami nitaonyesha mambo ya ajabu katika mbingu na katika dunia, damu, na moto, na minara ya moshi.

31 Jua litageuzwa kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla haijaja hiyo siku ya Bwana iliyo kuu na itishayo.

32 Na itakuwa ya kwamba mtu awaye yote atakayeliita jina la Bwana ataponywa; kwa kuwa katika mlima Sayuni na katika Yerusalemu watakuwako watu watakaookoka, kama Bwana alivyosema; na katika mabaki, hao awaitao Bwana”.

Ukisoma hapo kwa makini vifungu hivyo utaona sehemu ya kwanza katika unabii huo Mungu aliahidi kumwaga Roho wake, juu ya wote wenye mwili, ikiwa na maana kuwa WOTE, watakaomwamini yeye atawamwagia Roho wake bila kipimo, nao wataota ndoto, watatabiri, wataona maono..Lakini sehemu ya pili ya unabii huo, haimuhusu kila mtu. Bali itakuwa ni kwa watumishi wake tu.

Hao ndio amewaahidia, kuwamwagia Roho wake kwa kipimo cha kipekee sana na kupitia hao watakapokea nguvu za kitofauti sana, za kufanya miujiza isiyo ya kawaida.

Soma tena pale Anasema..

29 tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu.

30 Nami nitaonyesha mambo ya ajabu katika mbingu na katika dunia, damu, na moto, na minara ya moshi.

31 Jua litageuzwa kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla haijaja hiyo siku ya Bwana iliyo kuu na itishayo.

Haya ndio Roho Mtakatifu amejiandaa kuyafanya katika nyakati hizi za kumalizia, tutaona ishara ambazo hazijawahi kurekodiwa katika historia ya dunia, mfano wa zile za Musa na Eliya. Zikifanywa na watumishi waaminifu wa Mungu. Na ishara hizi hazitakuwa kwa ajili ya maonyesho kama wanavyofanya manabii wa uongo ili kujichotea umaarufu na pesa, hapana, bali zitakuwa kwa lengo la kuyavuta yale mabaki ya Mungu yaliyosalia duniani kwa sasa ambayo yamechanganywa na ukengeufu wa dini zao uongo na makristo na manabii  wa uongo..

Zingatia, umwagiko huu hautamuhusu kila mtu, bali watumishi wa Mungu wa Kike na wa Kiume waliowaaminifu tu.

Je! Wewe na wewe upo ndani ya wokovu? Na kama upo je ni mtumishi wa Mungu mwaminifu?.

Kumbuka wakati huo upo karibuni sana kutokea. Hivyo tumika kwa Bwana wako kwa uaminifu, ili wakati huo yamkini kama ukikukuta uko hai, basi Mungu akufanye wewe kuwa sehemu ya hiyo huduma. Tumeitwa hapa duniani tumtumikie Mungu kwa uaminifu, kwa kadiri  ya karama alizotupa.

Tumtambue Roho Mtakatifu na mipango yake. Ili tuishi sawasawa na mapenzi yake hapa ulimwengu.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

KUMBE MUNGU ANAWEZA KUKULIPA KWA USICHOSTAHILI!

NAMNA YA KUITAMBUA SAUTI YA MUNGU INAPOZUNGUMZA NA WEWE

Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

UFUNUO: Mlango wa 1

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/06/17/ahadi-ya-roho-iliyosalia-sasa-kwa-kipindi-chetu/