NJIA RAHISI YA KUMUHUBIRI KRISTO KWA MATAIFA.

by Admin | 9 July 2021 08:46 am07

Nakusalimu katika jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo. Ni siku nyingine tena Bwana ametupa neema ya kuiona, hivyo nakukaribisha sasa tuzidi kuyatafakari maneno matukufu ya Mungu wetu, Maadamu katujalia kuiona leo.

Kwanini leo hii imekuwa ngumu sana kuipeleka injili kwa watu walio nje, ili wamwamini Yesu Kristo (Tukisema walio nje, tunamaanisha watu wa kidunia, au watu walio katika dini nyingine), Tunaweza kusema Mungu anawajua walio wake, ni kweli, lakini hicho sio kisingizio, ipo sababu nyingine ambayo tumeikosa sisi kama kanisa na sababu yenyewe ni kukosa UMOJA.

Tukiupata huo kama kanisa basi hatutamia nguvu nyingi sana kuulezea ulimwengu uzuri wa Yesu, bali huo  umoja wenyewe tu utauaminisha ulimwengu yeye ni nani.

Bwana Yesu alilizungumza hilo katika..

Yohana 17:21 “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ILI ULIMWENGU UPATE KUSADIKI YA KWAMBA WEWE NDIWE ULIYENITUMA.

22 Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja.

23 Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ILI ULIMWENGU UJUE YA KUWA NDIWE ULIYENITUMA, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi”.

Umeona, kumbe ulimwengu unaweza kumwamini Yesu, kuwa ndiye mwokozi wa ulimwengu, ikiwa tu tutajitengeneza sisi kwanza katika umoja. Lakini tunapaswa tujue si kila umoja, ni umoja sahihi unaotokana na Mungu..Hapo Bwana hazungumzii  umoja wa kichama au umoja wa kidini, au umoja wa kimadhehebu, kama unaoendelea sasa hivi ulimwenguni.. bali umoja anaouzungumzia hapo ni umoja wa Roho,. Kwasababu haiwezekani watu wawili wanaamini vitu viwili tofauti, halafu wawe na umoja, huo sio umoja utakuwa ni umoja wa kimaslahi tu, lakini sio wa Roho.

Waefeso 4:3 “na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani.

4 Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.

5 Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja.

6 Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote”.

Umeona vifungu hivyo? Agizo mojawapo ni kwamba tuutambue ubatizo mmoja na sahihi ni upi, kisha wote tuwe nao, ambao ni ule wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo sawasawa na Matendo 2:38, 8:16, 10:48, 19:5, kisha wote tumpokee Roho mmoja, ambaye ndiye Roho Mtakatifu, tuwe na Bwana mmoja ambaye ni YESU KRISTO jiwe kuu la pembeni, na sio mtume mwingine, au mtakatifu mwingine pembeni yake hapana,.. Na vilevile tuwe na Imani moja, ambayo mzizi wake na shina lake ni BIBLIA TAKATIFU na sio dini au dhehebu.

Tukizingatia hayo, kisha tukashirikiana na ulimwengu ukatuona, basi hatutatumia nguvu kubwa kuwaamishi Kristo kwao, kwani huo umoja wenyewe tu utawahubiria watu uzuri wa Kristo. Lakini tukizidi kuupoteza umoja huo, kila mtu na imani yake, dhehebu lake,. Ni ngumu sana kuugeuza ulimwengu. Hivyo ni wajibu wetu sisi, kama kanisa la Kristo tujipime, je! Umoja huu uliosahihi upo ndani yetu? Kama haupo, basi ipo kasoro. Tujitahidi sana tuunde kwa bidii zote, ili Bwana aaminiwe katikati ya mataifa, matunda mengi yaje kwake..

Hilo ni agizo la Bwana, na sio la mwanadamu.

“Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ILI ULIMWENGU UJUE YA KUWA NDIWE ULIYENITUMA, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi”.

Shalom.

Maran atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/07/09/njia-rahisi-ya-kumuhubiri-kristo-kwa-mataifa/