Ni kweli Paulo alipuuzia maonyo aliyopewa ya kwenda Yerusalemu?

by Admin | 23 July 2021 08:46 am07

SWALI: Je Ni kweli Mtume Paulo alipuuzia, maonyo aliyoonyeshwa na Roho Mtakatifu kwa kinywa cha Agabo juu ya kwenda  Yerusalemu?


JIBU: Tusome habari yenyewe kwa faida ya watu wote;

Matendo 21:10 “Basi tulipokuwa tukikaa huko siku nyingi, nabii mmoja jina lake Agabo akashuka kutoka Uyahudi.

11 Alipotufikia akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, Roho Mtakatifu asema hivi, Hivyo ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa Mataifa.

12 Basi tuliposikia haya, sisi na watu wa mahali pale, tukamsihi asipande kwenda Yerusalemu.

13 Ndipo Paulo alipojibu, Mnafanya nini, kulia na kunivunja moyo? Kwa maana mimi, licha ya kufungwa, ni tayari hata kuuawa katika Yerusalemu kwa ajili ya jina lake Bwana Yesu.

14 Alipokataa shauri letu, tukanyamaza tukisema, Mapenzi ya Bwana na yatendeke.

15 Baada ya siku zile tukachukua vyombo vyetu tukapanda kwenda Yerusalemu.

Tofauti na wengi tunavyodhani kwamba mtume Paulo alipuuzia maono ya Mungu, na ndio maana akaenda kukumbana na matatizo makubwa kule Yerusalemu alipokwenda mambo ambayo hayakuwa na ulazima wa yeye kukutana nayo. Lakini si kweli, kama Paulo angekuwa ni mtu wa kupuuzia maono ya Mungu, asingeandika katika waraka wake mmoja “Msitweze unabii” (1Wathesalonike 5:20). Akimaanisha msipuuzie unabii.

Paulo alikuwa ni mtu aliyethamini sana maagizo ya Roho Mtakatifu, na kuyatekeleza wa wakati. Kuna wakati Mungu alimkataza asihubiri Neno Galatia na sehemu nyingine na akatii(mdo 16:6-9). Na wakati huo huo Mungu anamwonyesha maono avuke bahari aende Makedonia kuhubiri mahali ambapo hajawahi kufika hata siku moja. Na akatii

Hivyo kitendo cha kusema Paulo hakutii maagizo ya Roho Mtakatifu, ni kukosa shabaha.

Lakini swali linakuja kama sio kutii basi  ni kwanini aamue vile?

Jibu ni kuwa, ipo tofauti ya “mtu kupewa agizo” na “mtu kuelezwa uhalisia wa mambo / kupashwa habari”. Paulo hakupewa agizo na Roho Mtakatifu kuwa asipande Yerusalemu, kama alivyopewa maagizo sehemu nyingine. Hapana, bali alielezwa uhalisia wa mambo atakayokutana nayo huko mbeleni. Na ndio maana utaona kabla hata ya Agabo kumpa unabii ule, tayari Roho Mtakatifu alikuwa ameshamshuhudia mambo hayo kuwa atakutana nayo mbeleni. Soma.

Matendo 20:22 “Basi sasa, angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko;

23 isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja”.

Hivyo Paulo kwa kulitambua hilo, bado hakusita kukumbana na changamoto hizo, kwa ajili ya injili. Alifikiria sana akaona dhiki haziwezi kumfanya kondoo wa Mungu wasifikiwe na injili. Hivyo akajitia moyo na kwenda kama shujaa.

Jambo kama hilo utaona pia kwa mtume Petro, kipindi kile Bwana Yesu alimwambia wewe ni kijana, lakini ukiwa mzee watu watakuja kukufunga mikono yako na kukuchukua usipotaka, (Yohana 21:18). Kuonyesha kuwa vifungo na dhiki na vifo vinamsubiria mbeleni. Lakini lile halikuwa ni agizo kwamba Petro sasa akatafute namna ya kukwepa, dhiki hizo. Hapana.

Hata sasa ni kawaida ya Roho Mtakatifu kuzungumza nasi kwa namna zote mbili. Kuna wakati atatupa maagizo, na kuna wakati atatueleza uhalisia wa mambo. Sasa pale tunapopewa maagizo au tunapoonywa, ni sharti tutii, Mungu anapokuambia usihubiri mahali Fulani, ni kweli usiende kuhubiri, anapokuambia kahubiri mahali Fulani ni kweli nenda kahubiri.

Lakini kuna wakati utakuwa katika safari yako ya kumtumikia Mungu, na akakuonyesha, matunda, na changamoto zake, akakuonyesha hata, unapigwa mawe, au unafukuzwa, au unafungwa, au unazungumziwa vibaya. Moja kwa moja usikimbilie kusema Roho Mtakatifu ananionya nisiende kuhubiri, hapana, bali tazama pia upande wa pili wa matunda, Kwasababu dhiki kama hizo haziletwi na Mungu, bali ni shetani, ambaye anafanya hivyo ili akuzuie, usifanye kazi yake hilo tu. Lakini kumbe Mungu anatamani sana, ufike kule.

Kwahiyo usitafsiri kila ono, ni agizo ,  mengine Mungu anatuonyesha tu ili yatakapotokea tusifadhaike sana, kwasababu alishatutaarifu mapema.

Yohana 16:1 “Maneno hayo nimewaambia, msije mkachukizwa.

2 Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada.

3 Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba wala mimi.

4 LAKINI NIMEWAAMBIA HAYO, ILI MAKUSUDI SAA ILE ITAKAPOKUJA MYAKUMBUKE YA KUWA MIMI NALIWAAMBIA. Sikuwaambia hayo tangu mwanzo, kwa sababu nalikuwapo pamoja nanyi”.

Hivyo Bwana atusaidie na sisi tujifunze kuyapambanua maono ya Mungu.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

VIFO VYA MITUME WA YESU/ JINSI MITUME WALIVYOKUFA.

Tofauti kati ya ufunuo, unabii na maono ni ipi?

PINDO LA VAZI LAKE SASA LIMEREFUSHWA.

BADO UPO YERUSALEMU TU..GALILAYA HUTAKI KWENDA?

LIPI TUNAJIFUNZA KWA WALIOMWONA YESU ALIYEFUFUKA?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/07/23/ni-kweli-pualo-alipuuzia-maono-ya-kwenda-yerusalemu/