LIPI TUNAJIFUNZA KWA WALIOMWONA YESU ALIYEFUFUKA?

LIPI TUNAJIFUNZA KWA WALIOMWONA YESU ALIYEFUFUKA?

Shalom, Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe daima.

Siku ya leo, dunia inaadhimisha tukio kuu lililotokea takribani miaka 2000 iliyopita, Na tukio lenyewe ni lile la kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo kaburini.

Lakini lipo jambo nataka tujifunze, juu ya mazingira yaliyokuwa yanaendelea siku ile.  Lakini kabla ya kuingia katika kiini cha somo letu, nikurudishe nyuma kidogo ili tuweke msingi. Naomba ufuatilie mpaka mwisho lipo jambo kubwa utajifunza leo.

Siku mbili kabla ya Kristo kusulibiwa alikuwa ameketi katika nyumba ya mtu mmoja aliyeitwa Simoni mkoma, kama tunavyojua habari akiwa  anawafundisha alitokea mwanamke mmoja, akiwa amebeba kibweta cha Marhamu ya Nardo, akakifungua, akamwagia Yesu kichwani, lakini wale watu waliokuwa karibu walipoona tukio lile walianza kumnung’unikia yule mwanamke sana, kwanini anapoteza fedha nyingi katika mambo yasiyo  ya msingi. Sasa mpaka unaona watu wanakinung’unikia kitendo kile ujue kuwa marhamu ile ilikuwa si ya bei ya kawaida.

Kwani kama ingeuzwa wenyewe wanasema wangepata dinari 300, na dinari moja kwa enzi za kibiblia ni mshahara wa kibarua wa siku nzima, (Soma Mathayo 20:1-15), hivyo tukijaribu kubadilisha kwa wakati wetu huu, mshahara wa kibarua kwa siku nzima tunajua  ni kama sh. Elfu 20 hivi, ukiizidisha kwa 300, hiyo ni sawa na milioni 6.

Hivyo marhamu hiyo kwasasa ingeuzwa sh. Milioni 6. Kwahiyo unaweza kuona hapo mwanamke yule alijitoa kimasomaso kweli kuinunua, pengine aliuza kila kitu alichokuwa nacho ili tu, amnunulie Kristo marashi yale mazuri ya kupendeza. Na matokeo yake ni kuwa Bwana Yesu akampa thawabu kubwa sana, ya kumbukumbu lisilofutika daima..

Tusome.

Marko 14:3 “Naye alipokuwapo Bethania, nyumbani mwa Simoni mkoma, ameketi chakulani, alikuja mwanamke mwenye kibweta cha marhamu ya nardo safi ya thamani nyingi; akakivunja kibweta akaimimina kichwani pake.

4 Palikuwa na watu waliochukizwa katika nafsi zao wakisema, Kwani kupoteza marhamu namna hii?

5 Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa dinari mia tatu na kuzidi, wakapewa maskini. Wakamnung’unikia sana yule mwanamke.

6 Yesu akasema, Mwacheni; mbona mnamtaabisha? Amenitendea kazi njema;

7 maana sikuzote mnao maskini pamoja nanyi, na kila mpendapo mwaweza kuwatendea mema; lakini mimi hamnami sikuzote.

8 Ametenda alivyoweza; ametangulia kuupaka mwili wangu marhamu kwa ajili ya maziko

9 Amin, nawaambia, Kila ihubiriwapo Injili katika ulimwengu wote, na hili alilotenda huyu litatajwa kwa kumbukumbu lake”.

Sasa mpaka hapo tutakuwa tumeshajenga msingi wa somo letu la leo, Sasa tuzidi kusonga mbele.

Wakati Bwana Yesu anashushwa pale msalabani baada ya kufa kwake, biblia inatuambia kulikuwa na wanawake waliotoka naye Galilaya wakifuatilia kwa karibu, kujua  ni wapi watakapokwenda kuulaza mwili wa Bwana (Soma Luka 23:55-56 ).

Na walipoona na kupamaki, wakaondoka kwenda nyumbani, kuandaa, Manukato na Marhamu. Lengo lao lilikuwa ni kwenda kuipaka maiti ya Bwana marhamu hiyo. Lakini kwasababu siku hiyo ilikuwa ni maandalio ya sabato hawakuweza, ikawabidi, wayaweke tayari wasubiri mpaka siku ya jumapili asubuhi ambapo sabato itakuwa imeshakwisha, waende kuupaka mwili wake manukato hayo.

 Marko 16:1-3

 “1 Hata sabato ilipokwisha kupita, Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yakobo, na Salome walinunua manukato wapate kwenda kumpaka.

2 Hata alfajiri mapema, siku ya kwanza ya juma, wakaenda kaburini, jua lilipoanza kuchomoza;

3 wakasemezana wao kwa wao, Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe mlangoni pa kaburi”?

Lakini tunapaswa tujifunze, katika habari hiyo, kulikuwa hakuna umuhimu wowote wa kwenda kuupamba na manukato mwili ambao tayari upo kaburini, tena umeshakaa siku 3 mule,  uzingatia tena kaburi lenyewe limetiwa muhuri na walinzi, kiashirio kuwa hakuna mtu yoyote aliyeruhusiwa kusogelea mahali pale.

Kwa namna ya kawaida Marhamu ile ilistahili kumwagiwa Yesu akiwa hai, kama alivyofanya yule Mwanamke wa kwanza nyumbani kwa Simoni mkoma, au kama alivyofanya Miriamu nduguye Martha siku ile Yesu alipokwenda kwao (Yohana 12:3)..

Au wangemwagia, wakati bado hajazikwa, yaani mwili ukiwa bado haujaenda kaburini ili kuufanya usiotoe harufu, kama alivyofanya Nikodemo wakati ule walipomshusha msalabani ili kwenda kumzika

Yohana 19:39 “Akaenda Nikodemo naye, (yule aliyemwendea usiku hapo kwanza), akaleta machanganyiko ya manemane na uudi, yapata ratli mia.

40 Basi wakautwaa mwili wake Yesu, wakaufunga sanda ya kitani pamoja na yale manukato, kama ilivyo desturi ya Wayahudi katika kuzika”.

Lakini tunaona hawa wanawake, hawakujali upotevu wowote, waliindaa kwa ajili ya maiti iliyokwisha kuzikwa tayari,..Hilo ni tendo kuu sana la Upendo kwa Bwana wao.

Japokuwa walijua kuwa watakumbana na kikwazo cha Jiwe kubwa pale kaburini, japokuwa walijua kwa namna ya kawaida zoezi lao wanalojaribu kulifanya haliwezi kufanikiwa lakini walijitoa ufahamu, wakaanza safari yao hivyo hivyo, ya kwenda kupoteza marhamu zao za thamani nyingi, kwa ajili ya maiti iliyokwisha kuzikwa siku chache nyuma..

Lakini kwa tukio lao lile la upendo usio wa kawaida, walipofika tu pale kaburini, biblia inatuambia waliona kaburi limeshakuwa wazi tayari, malaika wa Bwana alitangulia kuwafungulia, tena akiwa mule ndani ya kaburi tayari anawangojea,… Embu Tuendelee kusoma..

Marko 16:3-8

“3 wakasemezana wao kwa wao, Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe mlangoni pa kaburi”?

4 Hata walipotazama, waliona ya kuwa lile jiwe limekwisha kuvingirishwa; nalo lilikuwa kubwa mno.

5 Wakaingia kaburini wakaona kijana ameketi upande wa kuume, amevaa vazi jeupe; wakastaajabu.

6 Naye akawaambia, Msistaajabu; mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulibiwa; amefufuka; hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka.

7 Lakini enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia.

8 Wakatoka nje, wakakimbia kutoka kaburini; kwa maana wameingia tetemeko na ushangao; wala hawakumwambia mtu neno, maana waliogopa”.

Unaona? Na baadaye wakati wanarudi walitokewa na Bwana Yesu mwenyewe, wakamsujudia, na kupewa maagizo ya kwenda kuwaambia mitume wake yawapasayo kufanya (Soma Mathayo 28:1-10)

NI UJUMBE GANI TUNAFUNDISHWA?

Kuna wakati Yesu atakuwa hai anatambea, na pia kuna wakati Yesu atajifanya kama amekufa..Tunapaswa tuonyesha upendo wetu dhati, na wa hali na mali kwake nyakati zote, kwasababu zote zina thawabu zake kubwa.

Wapo wale wanawake walimtia Yesu marhamu wakati akiwa hai, na Kristo akawapa thawabu zao, lakini tunaona wanawake hawa wengine watatu nao walikuwa radhi hata kwenda kufukua kaburi la Yesu ili tu wautie mwili wake mafuta ya thamani, japokuwa walijua kuwa hakuna matumaini yoyote, masaa machache baadaye yatageuka kuwa harufu mbaya, kutokana na kuwa Bwana alikaribia kwenda kutoa harufu, lakini hawakujali, kutoa walichokuwa nacho maadamu ni kwa ajili ya Bwana wao waliyempenda walifanya hivyo kwa furaha tele, na matokeo yake walipofanya hivyo, walikuwa wa kwanza kabisa kutokewa na Bwana, na kupewa maagizo ya kuwapelekea wale wengine, ambao hawakujishughulisha na chochote.

Na sisi pia, kuna wakati tunaweza kuona kazi ya Mungu imekufa, au inakaribia kufa, au haina thamani sana machoni petu, pengine unaweza kuona hata kama ukiisaidia au kutoa msaada wako ni kama unapoteza nguvu zako tu, au mali zako tu.. Lakini katika mazingira kama hayo, wewe jitoe kwenye kazi ya Mungu, kama ni fedha peleka, kama ni nguvu zako zipeleke, kama ni utumishi wako uachie hapo, hata kama kutakuwa hakuna matumaini yoyote ya kazi hiyo kufanikiwa kwasasa.. Wewe mfanyie Kristo kwa moyo wako wote..

Na matokeo yake ni kuwa utakuwa wa kwanza kumwona Kristo aliyefufuka, katika kanisa lake. Na yeye ndiye atakayekupa ujumbe wa kuwapelekea wengine..Hiyo yote ni kwasababu ulimthamini hata angali akiwa maiti inayokaribia kuoza na kunuka.. Hivyo na yeye atakuthamini na kukujalia kumuona katika utukufu wa kufufuka kwake.

Hivyo ujumbe wa leo ni kuwa tunapoadhimisha, kufufuka kwa Kristo, tukumbuke kuwa waliomwona wa kwanza  walikuwa ni wale wanawake watatu, Na kilichowafanya wamwone Yesu ni moyo wao ule wa kumtendea jambo bila kujali, kupotea kwa tumaini lao.

Injili kama hizi, zinazohubiriwa na wanawake wacha Mungu kama hawa, zinamatokeo makubwa sana rohoni, kama tutazizingatia katika maisha yetu ya ukristo.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

NI KITU GANI PETRO NA YOHANA WALIKIGUNDUA KABURINI?

HEKIMA YA KIMUNGU, INAINGIAJE MIOYONI MWETU?

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 1

RABI, UNAKAA WAPI?

MWANZO WA INJILI YA YESU KRISTO.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Emanuel kipwasa
Emanuel kipwasa
2 years ago

Amen nimebarikiwa na mafundisho