Naomba kujua maana ya haya maneno katika biblia..“Siti Msharifu”, “Mitalawanda” na “kulalama”

by Admin | 28 July 2021 08:46 am07

Jibu: Tukianza na Neno “Siti Msharifu”. Neno hili tunalipata mara moja tu! Katika biblia nzima katika kitabu cha Wimbo ulio bora 7:1.

Wimbo ulio bora 7:1 “SITI MSHARIFU, jinsi zilivyo nzuri Hatua zako katika MITALAWANDA. Mapaja yako ya mviringo ni kama johari, Kazi ya mikono ya fundi mstadi”

Maana ya neno hilo ni “binti wa Mfalme”.. Kiswahili cha zamani cha binti wa Mfalme ni “siti-msharifu”.. Kwahiyo katika mstari huo unaweza kusomeka kama “Binti wa mfalme, jinsi zilivyo nzuri hatua zako katika Mitalawanda”.

Na neno “Mitalawanda” linapatikana mara moja tu katika biblia yote, na tunalisoma katika kitabu hicho hicho cha Wimbo ulio bora 7:1.. Na maana ya neno hilo ni “Viatu vilivyotengenezwa kwa kamba”…kwa kiingereza sandals au sendoz.

Maeneo ya mashariki ya kati, watu hawakuwa wanavaa viatu kama hivi vyetu, bali vile vilivyotengenezwa kwa kamba, Kwahiyo Kiswahili cha zamani cha sendoz, ndio hiyo Mitalawanda.

Hivyo Mstari huo wa wimbo uliobora 7:1, unaweza kusomeka hivi.. “Binti wa mfalme, jinsi zilivyo nzuri hatua zako katika sendozi”.

Kwaujumla kitabu cha Wimbo ulio bora, kinahusu mazungumzo ya kimahusiano kati ya  mtu na mke wake katika hatua tofauti tofauti, kikifunua uhusiano wetu sisi na Kristo katika hatua tofauti tofauti (yaani wakati tunampokea Yesu na baada ya kumpokea Yesu), kwasababu kimaandiko, Kristo ndiye Bwana na sisi ni bibi-arusi wake.

Na neno la mwisho ni “Kulalama”. Neno hili limeonekana sehemu kadhaa katika biblia, na maana ya Neno hili ni “kuugua rohoni au moyoni, hususani kwa kuomba”.. Mtu anayeomba kwa kuugua sana, mtu huyo ni ANALALAMA!

Na ni wajibu wa kila Mkristo kuomba kwa kulalama kila wakati, kwasababu kama jambo una mzigo nalo huwezi kuliombea juu juu tu!, bali utaomba kwa kuugua sana. Na jambo linaloombewa kwa mzigo mzito ni rahisi kuleta matokeo haraka sana zaidi ya lile linaloombewa juu juu tu!

Baadhi ya mistari inayolitaja neno ni pamoja na.

Zaburi 55: 1 “Ee Mungu, uisikilize sala yangu, Wala usijifiche nikuombapo rehema.

2 Unisikilize na kunijibu, Nimetanga-tanga NIKILALAMA na kuugua”.

Na mingine ni Zaburi 55:17 na Yeremia 9:10.

Je umempokea Yesu??…Kumbuka Bwana yu karibu na siku zote yakumbuke maneno yake haya..

Marko 8:36  “Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake? 37 Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake?”

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

SOMO no.02 (BINTI WA YEFTHA).

KAMA MKRISTO FAHAMU ZIPO HATUA UTAPIGISHWA NA MUNGU.

Pambaja ni nini katika Biblia kama tunavyosoma katika kitabu cha Wimbo ulio bora 1:2?

FUNGUO WALIZOKUWA NAZO MABINTI WATANO WA SELOFEHADI!

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 11 (Mithali, Wimbo ulio bora, Mhubiri)

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/07/28/naomba-kujua-maana-ya-haya-maneno-katika-biblia-siti-msharifu-mitalawanda-na-kulalama/