Kwanini Yesu aliwaambia wale wakoma wakajionyeshe kwa makuhani?

by Admin | 12 August 2021 08:46 pm08

SWALI: Kwanini Bwana Yesu aliwaambia wale watu wenye ukoma waende kujionyesha kwa makuhani?, kwanini asiwaponye tu hivyo hivyo na kuwaacha mpaka awaambie waende kwa makuhani.

Luka 17:12 “Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali,13 wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu!

14 Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika”.


JIBU: Kama vile Injili ya Kristo inavyowafikia watu katika namna mbili, wengine kuwaokoa na wengine kama ushuhuda kwao (Mathayo 24:14)

Vivyo hivyo na uponyaji wake alivyouachia, alikusudia uwafikie watu kwa namna mbili. Kuokoa na wakati huo huo kuwa Ushuhuda.Si kila uponyaji au muujiza Yesu aliokuwa anaufanya ulikuwa ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Hapana, bali ponyaji nyingine aliziruhusu mahususi kwa lengo la kuwa ushuhuda kwa wengine, ili siku ile ya hukumu wasije wakasema hatukuona, au hatukusikia.

Tunasoma jambo kama  hilo katika..

Mathayo 8:1 “Naye aliposhuka mlimani, makutano mengi walimfuata.

2 Na tazama, akaja mtu mwenye ukoma akamsujudia, akisema, Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa.

3 Yesu akanyosha mkono, akamgusa, akisema Nataka; takasika. Na mara ukoma wake ukatakasika.

4 Yesu akamwambia, Angalia, usimwambie mtu; ila enenda zako, ukajionyeshe kwa kuhani, ukaitoe sadaka kama alivyoamuru Musa, IWE USHUHUDA KWAO”.

Ndicho kilichowakuta Makuhani, pamoja na mafarisayo na waandishi. Ni watu ambao walikuwa hawataki kusikia wala kuamini, Hivyo Bwana Yesu, alipowaponya baadhi ya watu hakuwaacha tu hivi hivi waende,kama alivyofanya sehemu nyingine, bali aliwaagiza waende kuwaeleza makuhani miujiza iliyowakuta,. Hivyo walikuwa wanapokea shuhuda nyingi sana kutoka kwa watu  mbalimbali walioponywa.. Pengine kwa siku  hata watu 100. Na kila walipoulizwa ni nani kawaponya wanasema YESU.

Hivyo hata sasa na sisi, tusifurahie tu miujiza ya Mungu anatuletea miujiza mingi, watu wanaponywa, wanafunguliwa, na huku maisha yetu yapo nje ya Kristo. tusifurahie kwasababu tujue ni hukumu tu tunajiandikia. Na ndio maana Bwana alisema maneno haya sehemu fulani;

Mathayo 11:21 “Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu.

22 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zao siku ya hukumu kuliko ninyi.

23 Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa mpaka mbinguni? Utashushwa mpaka kuzimu; kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika katika Sodoma, ungalikuwapo mji huo hata leo.

24 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko wewe”.

Hivyo hiyo ndio iliyokuwa sababu kwanini aliwaambia wakajionyeshe kwa makuhani, kwasababu wao ndio waliokuwa hawamwamini wala kuziamini kazi zake.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312 Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

Ukoma wa nyumba ulifunua nini zamani?

Nini maana ya msiwe waalimu wengi (Yakobo 1:3)?

Kwanini Bwana Yesu alitokea katika ukoo wa Yuda?

MIUJIZA YA KRISTO, HAITEGEMEI KANUNI ZA KIBINADAMU.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/08/12/kwanini-yesu-aliwaambia-wale-wakoma-wakajionyeshe-kwa-makuhani/