NI LIPI KATI YA MAKUNDI HAYA, WEWE UPO?

by Admin | 15 August 2021 08:46 pm08

Ikiwa Bwana Yesu atarudi leo, atakutana na makundi matatu ya watu wanaomsubiria yeye.

Sasa ni vizuri ukafahamu wewe upo katika kundi lipi, kuanzia sasa, kabla ya wakati huo kufika. Kwasababu wakristo wengi wanadhani ukishamkiri tu YESU basi, inatosha wewe ni tiketi ya moja kwa moja, kwenda katika unyakuo.

Ndugu yangu, hizi ni siku za mwisho, hatuna muda mrefu wa kuishi hapa duniani, kama hulijui hilo ndio ulifahamu sasa, ni wajibu wetu sisi, tunaosema tumeokoka, kuyatathimini maisha yetu ya wokovu, ili tujue tupo upande upi.

1) Tukianzana na kundi la kwanza la HENOKO.

Kama sote tunavyojua Henoko alikuwa ni mtu wa saba tangu Adamu, na mtu pekee aliyenyakuliwa kutoka ulimwenguni pasipo kuonja mauti kwenye dunia ya wakati ule. Na biblia inatueleza sababu ya kuhamishwa kwake ni kwasababu alishuhudiwa kuwa alimpendeza Mungu,

Waebrania 11:5 “Kwa imani Henoko alihamishwa, asije akaona mauti, wala hakuonekana, kwa sababu Mungu alimhamisha; maana kabla ya kuhamishwa alikuwa ameshuhudiwa kwamba amempendeza Mungu”.

Biblia inasema alitembea na Mungu kwa muda wa miaka 300. Hivyo Mungu hakuona vema awepo katika uharibifu  wa gharika uliokuwa unakuja ulimwenguni kote.

Vivyo hivyo wakati tunaoishi sasa ni wakati wa nyakati ya SABA ya kanisa kwa mujibu wa kalenda ya Mungu kama tunavyosoma katika kitabu cha Ufunuo sura ya 2&3. Hivyo hadi sasa lipo kundi dogo sana la watakatifu linalofananishwa na Henoko, litakalotembea na Kristo hadi wakati wa kuja kwake, Watu hawa katika biblia wanajulikana kama Wanawali werevu na Bibi-arusi wa Kristo (Ufu 21). Ndio watakatifu watakaokwenda katika unyakuo ikiwa parapanda ya mwisho italia leo.

Hawa Mungu atawaepusha na dhiki kuu, na adha zitakazokuja huko mbeleni, kwa tukio linaloitwa UNYAKUO, kwasababu ni vipenzi wa Mungu.

Ufunuo 3:10 “Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, utoke katika saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi”.

Ni watu ambao thawabu yao mbinguni ni kubwa sana.. ndio wale ambao watatawala na Kristo kama Wafalme, mabwana na makuhani. Na makao yao itakuwa ni katika ile Yerusalemu mpya ishukayo kutoka mbinguni kwa Baba.

Kundi la Pili, ni NUHU.

Hili kundi halituhusu sisi watu wa mataifa, Bali linawahusu Wayahudi. wayahudi tu peke yao ndio watakaokuwa katika kundi hili na Nuhu, Kristo atakaporudi. Ikiwa na maana kuwa, Unyakuo utakapopita hawatakwenda popote, kwasababu hawakuwa ndani ya Kristo. Na Mungu alifanya hivyo kwa makusudi, kuwapiga upofu ili sisi tuipokee hii neema. Lakini wakati utafika, hii neema Kristo atairudisha kwao, (Soma Warumi 11)  na baadhi yao wataiamini. Sasa hao, ndio wataingizwa katika Safina(mafichoni) ambayo Mungu ataindaa wakati huo, ili kuwalinda na hiyo dhiki kuu ya mpinga-Kristo, pamoja na ghadhabu ya Mungu itakayokuja ulimwenguni wakati huo. Soma (Ufu 7:1-8, 14:1)

Ufunuo 12:14 “Mwanamke yule akapewa mabawa mawili ya tai yule mkubwa, ili aruke, aende zake nyikani hata mahali pake, hapo alishwapo kwa wakati na nyakati na nusu ya wakati, mbali na nyoka huyo”.

Na hawa vilevile hawatakuwa wengi, idadi yao itakuwa ni 144,000 tu Basi, hawa watahifadhiwa mbali na mpinga-Kristo, hivyo mpaka dunia inateketezwa kwa moto, hawa watakuwa mafichoni mahali ambapo Mungu amewaandalia wao tu. Hawakufa, mpaka utawala wa miaka 1000 utakapoanza, kama vile Nuhu alivyoishi hadi gharika ilipoisha.

Kundi la tatu ni LUTU.

Kundi hili ndio gumu zaidi, kwasababu halinyakuliwi, wala halitunzwi, bali linajiokoa lenyewe. Kama vile Lutu, wakati wa maangamizi ulipofika, hakunyakuliwa kama Henoko, wala hakuhifadhiwa kwenye safina, au handaki Fulani, kama Nuhu, bali aliambiwa na wale malaika, jiponye nafsi yako. (Mwanzo 19:17). Ikiwa na maana akiendelea kubaki pale, ni kifo.

Na utaona Lutu, alikuwa ni tajiri sana, lakini siku alipolazimika kuondoka, hakuondoka na kitu chochote pamoja naye hata kijiko, isipokuwa familia yake.

Ndivyo itakavyokuwa kwa kundi hili la wakristo vuguvugu watakaokosa unyakuo, ambao wanaojulikana kama wanawali wapumbavu. Siku hiyo watalazimika, kuingia katika dhiki kuu, ambayo kujiponya kwao ni lazima kuambatane na vifo na dhiki, na mateso mengi sana.

Na kwa bahati mbaya wengi sana hawataweza kustahili, wategeuka nyuma. Na matokeo yake ni kuwa jiwe la chumvi kama mke wa Lutu. Wengi wanadhani, kipindi cha dhiki kuu, kitakuwa ni chepesi, usidanganyike, mke wa Lutu, alidhani hivyo alipokuwa anatoka, lakini mbeleni aliona alipotoka ni heri kuliko alipokuwa anaelekea na ndio maana akagueka nyuma akawa jiwe la chumvi. Nataka nikuambia Siku hiyo ya dhiki kuu, na ya mapigo Mungu, mateso utakayokuwa unayapitia,  utaona ni heri upokee tu chapa,  kama sio  kumkufuru Mungu kabisa, kuliko kuvumilia dhiki hizo.

Kulithibitisha hilo soma.

Ufunuo 16:8 “Na huyo wa nne akakimimina kitasa chake juu ya jua, nalo likapewa kuwaunguza wanadamu kwa moto.

9 Wanadamu wakaunguzwa maunguzo makubwa, nao wakalitukana jina la Mungu aliye na mamlaka juu ya mapigo hayo; wala hawakutubu wala kumpa utukufu”.

Na kibaya zaidi, ni kuwa kundi hili hata kama litafanikiwa kustahimili dhiki(yaani kufa bila kuikana imani), kule litakapokwenda litakuwa la chini kabisa, halitakuwa na thawabu yoyote. Kwasababu halina chochote mkononi mwao, kama vile Lutu alivyopoteza vyote.

Ndugu, haya mambo yapo karibuni sana. Swali la kujiuliza Je! Wewe upo katika kundi lipi, Je! Ni la HENOKO au la LUTU. Jibu unalo moyoni mwako, ikiwa leo hii maisha yako yote ni kufikiria tu mambo ya ulimwenguni, hutaki kuishi maisha ya utakatifu yanayompendeza Mungu, Usitazamie kuwa Utakuwa katika kundi la Henoko. Ikiwa habari za siku za mwisho hazikuvutii, lakini habari za kutabiriwa biashara yako ni zenye kipaumbele, basi ujue hapa duniani utabaki tu kama paraparanda italia leo.

Tujifunze kwa Henoko, yeye alitembea na Mungu mpaka Mungu mwenyewe akamwonyesha Siku ya Kiama itakavyokuwa, unategemea vipi Mungu asimwepushe na ile gharika iliyokuwa mbele yake?

Yuda 1:14 “Na Henoko, mtu wa saba baada ya Adamu, alitoa maneno ya unabii juu ya hao, akisema, Angalia, Bwana alikuja na watakatifu wake, maelfu maelfu,

15 ili afanye hukumu juu ya watu wote, na kuwaadhibisha wote wasiomcha Mungu, kwa ajili ya kazi zao zote za upotevu walizozitenda bila kumcha Mungu, na kwa ajili ya maneno magumu yote ambayo hao wenye dhambi wasiomcha Mungu wameyanena juu yake”.

Bwana atusaidie.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

MAJONZI YA MTUME PAULO KWA NDUGU ZAKE.

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita..

SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

KWA MIOYO YAO WAKAREJEA MISRI.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/08/15/ni-lipi-kati-ya-makundi-haya-wewe-upo/