Nini maana ya “Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi”?

by Admin | 21 August 2021 08:46 pm08

SWALI: Biblia inamaanisha nini inaposema “Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi”?


JIBU: Tusome

Mithali 22:1 “Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi; Na neema kuliko fedha na dhahabu”.

Inaposema kuchagua jina jema, inamaanisha Sifa njema, kwamfano labda kwenye jamii utasikia watu wanasema mtu Fulani ni mkarimu, au fulani ana upendo, au yule ana utu, hilo tayari ni jina jema, ambalo limezalika kutokana na tabia zake nzuri, Lakini ukisikia wanasema mtu yule ni muhuni, au kibaka, au tapeli, au fisadi, au jambazi, tayari hilo ni jina baya, ambalo halijazuka hivi hivi tu, bali limeonekana katika maisha ya yule mtu.

Sasa tukirudi katika mstari huo , hapo haimaanishi mtu kuwa na mali nyingi ni vibaya.. Hapana, bali anamaanisha kuchagua mali, Zaidi ya sifa njema hiyo ndio mbaya sana.

Kwamfano, utakuta mtu anachagua kufanya kazi ya bar/ casino, kisa tu inamlipa pesa nyingine kuliko zile nyingine za kawaida. Jiulize, mtu kama huyu atatafsiriwaje katika jamii, kama sio barmaid, au kahaba? Hiyo yote ni kwasababu kachagua pesa Zaidi ya jina zuri.

Au mkristo unapoacha kumwimbia Mungu wake, unakwenda moja kwa moja kuimba jimbo za kidunia, kisa tu atapata pesa za haraka. Hajui kuwa jina lake linabadilika kutoka katika kuwa mtumishi hadi muhuni.

Au kanisa la Kristo, linaposhiriki katika kampeni za kisiasa kisa tu limeahidiwa donge nono kutoka kwa wanasiasa. Jiulize ni nini kinajengeka katika macho ya jamii? Si wataliita chama cha kisiasa na sio kanisa tena sivyo? Japo ni kweli watapata pesa lakini tayari jina lao limeshabadilika. Hakuna mtu atakayewaamini.

Vivyo hivyo na sisi katika mambo yetu ya maisha ya kila siku, Ni heri tuchague jina jema, kwamfano sio kila huduma tutoze watu pesa, tukifanya hivyo hatuwezi kuitwa wakarimu, hatuwezi kuitwa wenye utu, au wenye upendo.

Tumuige Bwana wetu Yesu Kristo ambaye alitafuta, heshima, na jina jema katika huu ulimwengu Zaidi ya kitu kingine chochote.

Luka 2:52 “Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu”.

Jina jema linatupa kibali kikubwa sana cha kukaribiwa au kutumiwa na Mungu, Mfano, Kornerio alitokewa na Mungu mpaka kupewa neema ya wokovu kutokana na sifa yake nzuri katika jamii.

Warumi 10:22 “Wakasema, Kornelio akida, mtu mwenye haki, mchaji wa Mungu, aliye na sifa njema kwa taifa lote la Wayahudi, alionywa na malaika mtakatifu kutuma watu kwako, uende nyumbani kwake, apate kusikiliza maneno kwako”

Na wengine wengi utawasoma katika biblia kama vile Anania (Matendo 22:12) na Stefano, (Matendo 6:3-5) wote hawa kutokana na sifa zao nzuri, Mungu aliwatumia sana. Vivyo hivyo na sisi tuthamini jina jema, kuliko mali, au mambo ya huu ulimwengu yanayopita.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.

Pesa za bindoni ni nini?(Marko 6:8)

Maswali na Majibu

Nini maana ya Mungu amemfanya mwanadamu mnyofu?

Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake wote.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/08/21/nini-maana-ya-heri-kuchagua-jina-jema-kuliko-mali-nyingi/