by Admin | 29 August 2021 08:46 pm08
Kuna Nabii mbili zilizotabiriwa na Mungu zinazokuja mbele yetu, Na nabii hizo ni KUOKOLEWA au KUHUKUMIWA. Wanadamu wote ni lazima waangukie katika mojawapo ya sehemu hizo mbili.
Lakini kabla ya yote kuna maswali machache ambayo tunaweza kujiuliza!,
Na maswali yenyewe ni haya; Je! Mungu anamchagua mtu kabla ya hata ya yeye kuzaliwa?, na je! Anajua kuwa huyo mtu hatma yake itakuwa ni ipi?, katika ziwa la moto au mbinguni?
Jibu ni kwamba Mungu anajua mambo yote, kwasababu ili awe Mungu ni lazima awe anajua kila kitu, na awe na upeo wa mbali sana kupita wetu na wa viumbe vyote, hivyo Mungu anamjua mtu kabla ya huyo mtu kuzaliwa, na anajua hatma yake kabla hata mtu huyo kuzaliwa..
Anajua kabisa mwisho wake utakuwaje, kama ataokoka au atapotea!. Sisi wanadamu hatujui ni Mungu peke yake ndio anajua, na wala hakuna mtakatifu yoyote anayejua hatima ya mwanadamu mwenzake yeyote. Hiyo siri anajua yeye mwenyewe!.
Sasa swali sisi tutajijuaje kama tumekusudiwa uzima wa milele tangu asili (kwamba tutaokolewa), Tutakuja kuona mbeleni kidogo ni kwa namna gani tunaweza kujijua kama tutaokolewa au tutahukumiwa siku za mwisho..
Lakini kwanza hebu tutazame unabii wa watakaohukumiwa siku za mwisho…
Ufunuo 20:12 “Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.
13 Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake”.
Umeona hapo?.. Huo unabii ni lazima utimie kama ulivyo.. Mungu alishaliona kundi lote na anawajua wote watakaosimama hukumuni siku hiyo, na anawajua kwa majina kwamba watakuwa ni Fulani na fulani, na Unabii huo ni lazima uje kutimia kama ulivyo.
Kadhalika upo unabii wa watakaookolewa siku za mwisho…
Ufunuo 7:9 “Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-Kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao”
Umeona na hapo pia? Wapo watu kutoka kila taifa, ambao wataokolewa, na Mungu anawajua wote watakaokolewa kwa majina na kwa sura… Lakini vile vile hajawataja!.. Maana yake hakuna mwanadamu yeyote aliyeambiwa na Mungu kuwa atakuwepo mbinguni siku za mwisho.
Sasa tutajijuaje kama tutakuwa miongoni mwa watakaokwenda mbinguni? Au watakaohukumiwa siku za mwisho..
Jibu ni rahisi, tutajua kama tutaokolewa siku ya mwisho kwa maisha tuanayoishi sasa… kama tunalitii Neno lake na kulifuata, maana yake kama tumetubu na kubatizwa na kumpokea Roho Mtakatifu na kuishi maisha ya utakatifu na ya kumpendeza yeye baada ya hapo, kama tutakaa na kuishikilia neema hiyo bila kuiachaia basi tuna uhakika wa kuwa miongoni mwa lile kundi kubwa la watakaokolewa.
Lakini kinyume chake kama tunaukataa wokovu leo, na kufa katika hali hii, basi tutakuwa miongoni mwa watakaotimiza unabii wa kuhukumiwa na kutupwa katika lile ziwa la moto siku za mwisho.
Hivyo uchaguzi ni wetu!.. kuchagua uzima wa milele au kuchagua mauti ya milele.
Yeremia 21:8 “Nawe waambie watu hawa, Bwana asema hivi, Tazama naweka MBELE YENU NJIA YA UZIMA, NA NJIA YA MAUTI”
Kumbukumbu 30: 15 “Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya”
Je! Umechagua unabii upi kuutimiza?
Bwana atubariki na kutujalia tuzidi kusogea kwake.
jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/08/29/je-umejiandaa-kutimiza-unabii-upi/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.