Je Eliya aliandika waraka baada ya kupaa mbinguni?

Je Eliya aliandika waraka baada ya kupaa mbinguni?

SWALI: Tunajua kuwa Nabii Eliya alipaa mbinguni katika upepo wa kisulisuli, lakini tunakuja kuona miaka mingi baadaye akituma waraka kwa mfalme mfalme Yehoramu juu ya ugonjwa wake (2Nyakati 21:12). Jambo hilo linawezekanikaje?


Jibu: Labda tusome,

2Nyakati 21:11 “Tena ndiye aliyefanya mahali pa juu milimani pa Yuda, na kuwaendesha katika uasherati wenyeji wa Yerusalemu, na kuwakosesha Yuda.

12 LIKAMJIA ANDIKO KUTOKA KWA ELIYA NABII, kusema, Bwana, Mungu wa Daudi baba yako, asema hivi, Kwa sababu hukuziendea njia za Yehoshafati baba yako, wala njia za Asa mfalme wa Yuda;

13 lakini umeiendea njia ya wafalme wa Israeli, ukawaendesha katika uasherati Yuda na wenyeji wa Yerusalemu, kama walivyofanya nyumba ya Ahabu; tena umewaua ndugu zako wa nyumba ya baba yako, waliokuwa wema kuliko wewe;

14 tazama, Bwana atawapiga pigo kubwa watu wako, na watoto wako, na wake zako, na mali yako yote;

15 nawe utakuwa na ugonjwa mkuu kwa maradhi ya matumbo, yatakapotokea matumbo yako kwa sababu ya ugonjwa huo siku kwa siku”

Ni kweli kabisa unabii huo ni wa kipindi cha mbele kabisa, wakati ambao Nabii Eliya ameshachukuliwa juu… Lakini swali la msingi hapo ni kwanini Eliya aonekane tena hapa akimtolea unabii huyu mfalme, je alituma huo waraka kutoka mbinguni huko alikokuweko au?

Jibu ni la! Hakutuma waraka kutoka mbinguni, bali ulikuwa ni waraka ambao aliuandika kabla ya kunyakuliwa juu. Alipewa unabii wa mbeleni, kwamba atatokea mfalme anaitwa Yehoramu ambaye atafanya mambo yasiyompendeza Mungu, na Bwana Mungu akampa maagizo aandike habari ya mambo yake pamoja na adhabu atakayoipata, hivyo Nabii Eliya akaandika katika waraka, na baada ya hapo pengine alimpa Eliya au mtumishi mwingine chini yake ili baada ya yeye kuondoka na huyo mfalme atakapotokea basi apewe ujumbe wake.

Na kweli baada ya hapo waraka ule ulihifadhiwa mpaka Mfalme Yohoramu alipotokea, na kufanya mabaya sawasawa na unabii huo wa Eliya, na mwisho akapatwa na mabaya kama Eliya alivyoandika..Kwani maandiko yanasema Yehoramu alipata ugonjwa wa matumbo, utumbo ukawa unatoka nje, huku unaoza!, na alikufa kifo cha kutokutamanika.

2Nyakati 21:18 “Na baada ya hayo yote Bwana akampiga matumbo kwa ugonjwa usioponyeka.

 19 Ikawa baada ya siku, ikiisha miaka miwili, matumbo yake yakatokea kwa sababu ya ugonjwa wake, akafa akiugua vibaya. Wala watu wake hawakumfukizia mafukizo kama ya baba zake”.

Hivyo sio kwamba Nabii Eliya alirudi kumtabiria wala kutuma wakara kutoka mbinguni, hapana bali aliuandika kabla ya kuondoka kwake.

Jambo kama hilo hilo pia tunaliona kwa Nabii mmoja ambaye alipewa unabii wa kuzaliwa mfalme atakayeitwa Yosia, ambaye atazibomoa bomoa madhabahu zote za baali katika Israeli..

1Wafalme 13:1 “Na tazama, akatoka mtu wa Mungu katika Yuda kwa neno la Bwana, akafika Betheli. Naye Yeroboamu alikuwa akisimama penye madhabahu, afukize uvumba.

 2 Basi mtu huyo akapiga kelele juu ya madhabahu, kwa neno la Bwana akasema, Ee madhabahu, madhabahu, Bwana asema hivi, Angalia, mtoto atazaliwa katika nyumba ya Daudi, jina lake Yosia; na juu yako atawachinja makuhani wa mahali pa juu, wanaofukiza uvumba juu yako, na mifupa ya watu itateketezwa juu yako”

Baada ya unabii huu kutoka kwamba atazaliwa mtoto anayeitwa Yosia, uliandikwa chini, na kisha kuhifadhiwa, ilipita miaka zaidi ya 100 ndipo mtoto huyo alipokuja kuzaliwa.. na akafanya yote sawasawa na yaliyotabiriwa kuhusu yeye.. Unaweza kusoma habari hiyo katika kitabu cha 2Wafalme 23:16-20.

Sio hao tu!, hata Nabii Isaya alishatabiri habari za kutokea Mfalme anayeitwa Koreshi ambaye atamjengea Mungu nyumba katika Israeli, na akamwandikia waraka huo, na ukahifadhiwa na wakati ulipofika miaka mingi baadaye, mfalme huyo alitokea kweli na akapewa ujumbe wake huo. Unaweza kusoma unabii huo katika Isaya 44:28, Isaya 45:1 na kutimia kwa unabii huo unaweza kusoma Ezra 1:2

Hivyo tunachoweza kujifunza ni kuwa Mungu anayajua yote yanayokuja, na kwamba Neno la Mungu halipiti, kama aliweza kuandika habari za Yehoramu miaka mingi kabla hajaja, na habari zake zikatimia kama zilivyo, vile vile kama aliweza kuziandika habari za Koreshi mfalme wa Uajemi na zikatimia kama zilivyo…  Basi tujue kuwa maneno yake aliyosema kuwa walevi, waasherati, waabuduo sanamu, wezi, n.k hawataurithi uzima wa milele  sawasawa na Wagalatia 5:21, basi tutambue kuwa Neno lake sio uongo, ni lazima litimie tu!, kwasababu Mungu ni yeye Yule jana, leo na hata milele habadiliki.

Wagalatia 5:19 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,

20  ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,

21  husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, KAMA NILIVYOKWISHA KUWAAMBIA, YA KWAMBA WATU WATENDAO MAMBO YA JINSI HIYO HAWATAURITHI UFALME WA MUNGU”

Hivyo kama bado hatujamkabidhi Bwana maisha yetu, huu ni wakati wa kufanya hivyo.. Kama bado hujaokoka, ni  vizuri kufanya sasa kama mambo hayajaharibika, na ikashindikana kuyafanya upya tena. Hivyo hapo ulipo usipoteze muda, jigenge dakika chache na kisha tubu dhambi zako zote ukimaanisha kuziacha, na kisha tafuta ubatizo sahihi ambao ni wa maji mengi na kwa jina la Yesu ili ubatizwe upate ondoleo la dhambi zako, na hatimaye utapokea kipawa cha Roho Mtakatifu, ambaye atakuongoza na kukutia katika kweli yote ya maandiko.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

NI VIZURI SISI KUWAPO HAPA.

KAMA MKRISTO FAHAMU ZIPO HATUA UTAPIGISHWA NA MUNGU.

JINSI MTUME PAULO ALIVYOUTHAMINI WITO WAKE, JUU YA WENYE VYEO.

WALA MSIUANGALIE MWILI, HATA KUWASHA TAMAA ZAKE.

KUJIFUNUA KWA YESU KWA PILI.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments