MWANAMKE, BINTI, MAMA. (Sehemu ya 3)

by Admin | 23 October 2021 08:46 pm10

Hii ni sehemu ya tatu ya mfululizo wa masomo kwa wanawake, katika sehemu ya kwanza  na ya pili tumeona, ni kwanini Bwana aliwatambua baadhi ya wanawake, kwa jinsia zao, na sio kwa majina yao, kwa kuwaita “wanawake”, na sehemu nyingine kuwatambua kwa mionekano yao kwa kuwaita “Binti” na sio labda kwa majina yao..ipo sababu, ikiwa hujapata bado, chambuzi zake, basi tutumie msg inbox tukutumie..

Lakini leo tutasonga mbele tena, kuona ni kwanini baadhi ya wanawake, aliwatambua kwa majina ya “MAMA”.

Mama ni cheo cha ukomavu, kwasababu mpaka uitwe mama ni wazi kuwa lazima utakuwa na watoto uliowazaa au unaowalea chini yako. Sasa tukirudi kwa Bwana Yesu, kuna wanawake aliwaona ni “Wamama rohoni”, sio mwilini, kwasababu kulikuwa na wanawake wengi, lakini si wote aliwaita “Mama” kama tu vile si wote aliwaita “Binti yangu”, bali baadhi tu.

Sasa embu twende tukasome baadhi ya Habari katika biblia kisha tuone, ni nini Bwana anatufundisha katika Habari husika. Mwanamke wa kwanza tutakayemtazama ni yule mkananayo. Tusome;

Mathayo 15:21 “Yesu akaondoka huko, akaenda kando pande za Tiro na Sidoni.

22 Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo.

23 Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu.

24 Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.

25 Naye akaja akamsujudia, akisema Bwana, unisaidie.

26 Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.

27 Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao.

28 Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, MAMA, IMANI YAKO NI KUBWA; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile”.

Angalia asili ya huyu mwanamke, hakumtafuta Bwana kwa shida zake mwenyewe, au kwa matatizo yake mwenyewe, bali alimtafuta Bwana Yesu kwa shida za mwanawe.. Japokuwa mwanzoni hakujibiwa chochote, hata baada ya pale alipewa na maneno ya kukatishwa tamaa ya kuitwa mbwa, lakini bado hakuacha kuomba kwa shida ya mtu mwingine, kwasababu uzito wa mwanae ulikuwa kama wakwake.

Hiyo ni kuonyesha ni jinsi gani asivyojali vya kwake tu, bali hata vya wengine…

Mwanamke mwingine ni Mama yake Yesu mwenyewe, ambaye tunamsoma katika Yohana 2:1-4 siku ile alipoalikwa katika Harusi..

Yohana 2:1 “Na siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwapo.

2 Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake.

3 Hata divai ilipowatindikia, mamaye Yesu akamwambia, Hawana divai. 4 Yesu akamwambia, MAMA, TUNA NINI MIMI NAWE? Saa yangu haijawadia”.

Angalia tabia yake alijali shida za wengine, aibu za wengine, akazifanya kama ni za kwake. Na kumpelekea Kristo, na muda huo huo akamwita “mama”

Mwingine ni Mariamu Magdalena, asubuhi ile ya kufufuka kwa Bwana, alikuwa akilia pale makaburini ndipo Yesu akamtokea na kumwambia “Mama unalilia nini?” Saa hiyo hiyo Yesu akamtuma kwa ndugu zake kwenda kuwatangazia injili. Akawa mtu wa kwanza kupewa neema ya kuwahubiria watu wengine Habari za kufufuka kwa Bwana Yesu. (Yohana 20:11-18)..

Neema hiyo si kila mwanamke atapewa, bali ni wale “wamama rohoni tu” Wanawake waliokomaa kiroho,ambao wanajua wajibu wao kwa Bwana, wanajua kuwaongoza wengine katika njia za Mungu, haijalishi umri wao Rohoni watu kama hawa, wanawekwa kundi moja na akina Sara, na Rebeka, na Mariamu, na Elizabeti na wengineo. Kwasababu wamevuka viwango cha utoto, hadi kufikia hatua ya utu uzima ya kuzaa na kulea.

Swali ni je! Wewe, dada upo katika kundi gani? Bwana anapokuona anakutambuaje? msichana? Au Mtu? Mtoto? Au Mama?. Kabla hujafikiria kuyatazama Maisha ya mitume wa Yesu mfano wakina Petro waliishije, embu tafakari kwanza, Maisha ya wanawake wacha Mungu katika biblia waliishije. Hiyo itakusaidia sana mwanamke.

Tamani sana, Kristo akutambue kama “Mama” Ni heshima ya juu sana, Kristo anaweza kumpa mwanamke, iliyosawa na ya “Kitume”. Kua kiroho timiza wajibu wako wa kuitangaza injili na pia kuwasaidia wengine kumjua Mungu rohoni.

Bwana akubariki.

Maran atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/10/23/mwanamke-binti-mama-sehemu-ya-3/