UMEDI NA UAJEMI ZILITAWALAJE?

by Admin | 18 November 2021 08:46 am11

Katika biblia tunaona kama Umedi na Uajemi zikitajwa kwa pamoja, kana kwamba ni Taifa moja, ingawa ni falme mbili tofauti, sasa zilitawalaje?

Umedi na Uajemi Ni utawala mmoja ulioundwa na Falme mbili tofauti, Ili kuelewa vizuri tuchukue mfano wa Taifa la Tanzania, Taifa la Tanzania limeundwa na mataifa mawili, Zanzibar na Tanganyika, Na yalipoungana ndio ikawa Tanzania, Kwahiyo badala ya kusema Tanzania, tunaweza kusema ni Taifa la Tanganyika na Zanzibar. Na ukitazama utaona unapofika wakati uchaguzi wa uRaisi, Raisi anayechaguliwa kuiongoza nchi yote anaweza kutoka upande wowote ule kati ya pande hizo mbili. Utaona leo anaweza kutokea Tanganyika, awamu ijayo akatokea Zanzibar.

Ndivyo ilivyokuwa kwa Ufalme wa Umedi na Uajemi. Zilikuwa ni falme mbili zilizoungana na kuwa ufalme mmoja. Lakini wafalme waliokuwa wanatawala, walikuwa wanapokezana, awamu hii mfalme anaweza kutokea Umedi, awamu ijayo akatokea Uajemi. Kama vile Raisi wa Tanzania, leo anaweza kutokea Bara, awamu ijayo akatokea Zanzibar.

Ndio maana utaona baada tu ya Ufalme wa Babeli kuanguka, ufalme uliochukua hatamu ni Dario, wa Umedi, huyu ndiye aliyemwangusha Nebukadneza, lakini bado hakuwapa ruhusa Israeli warudi nchini kwao, Israeli waliendelea kukaa mateka. Ingawa huyu Dario, alimheshimu sana Danieli, hata kumweka Danieli kuwa mkuu wa Maliwali wa ufalme wake wote.

Danieli 6:30 “Usiku uo huo Belshaza, mfalme wa Wakaldayo, akauawa.

31 Na Dario, Mmedi, akaupokea ufalme, naye umri wake alikuwa na miaka sitini na miwili”.

Danieli 7:1 “Ilimpendeza Dario kuweka juu ya ufalme maliwali mia na ishirini, wawe juu ya ufalme wote;

2 na juu yao akaweka wakubwa watatu, na Danielii alikuwa mmoja wao; ili maliwali hawa watoe hesabu kwao, mfalme asipate hasara.

3 Basi Danielii huyo alipata sifa kuliko wakubwa na maliwali, kwa kuwa roho bora ilikuwa ndani yake; naye mfalme akaazimu kumweka juu ya ufalme wote”.

Lakini ulipofika utawala wa Koreshi miaka michache baadaye ambaye alikuwa ni Muajemi ndipo Israeli walipofunguliwa kutoka katika utumwa, na kupewa ruhusa kurudi nchini kwao, kuutengeneza mji wao na Hekalu la Mungu lililobomolewa na Mfalme Nebukadneza.

2Nyakati 36:22 “Ikawa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, ili kwamba neno la Bwana alilolisema kwa kinywa cha Yeremia lipate kutimizwa, Bwana akamwamsha roho yake Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata akapiga mbiu katika ufalme wake wote, akaiandika pia, akisema,

23 Koreshi, mfalme wa Uajemi asema hivi; Bwana, Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote za dunia; naye ameniagiza nimjengee nyumba katika Yerusalemu, ulioko Yuda. Basi kila mtu katika ninyi nyote mlio watu wake, Bwana, Mungu wake, na awe pamoja naye, na akwee”.

Hivyo utawala huu wa Umedi na Uajemi, ndio Mungu alioutumia kuwapa raha Israeli, kwani ndio uliowaweka Israeli huru, na kuwapa ruhusa ya kwenda kuijenga nchi yao, ingawa ni kwa vipindi vya tabu, lakini hatimaye kazi ya ujenzi ilikamilika katika utawala huu kabla ya kuingia utawala wa UYUNANI, ambao uliusumbua sana Israeli.

Pia katikati ya utawala huu wa Umedi na Uajemi, ndipo Malkia Esta alitokea.

Esta 1:1 “Zamani za Ahasuero; naye huyu Ahasuero alimiliki toka Bara Hindi mpaka Kushi, juu ya majimbo mia na ishirini na saba;

2 siku zile mfalme Ahasuero alipoketi katika kiti cha enzi cha ufalme wake, huko Shushani ngomeni;

3 mwaka wa tatu wa kumiliki kwake, ikawa aliwafanyia karamu maakida wake wote na majumbe wake; WAKUU WA UAJEMI NA UMEDI, watu wenye cheo na maakida wa majimbo, wakihudhuria mbele zake”.

Lakini pamoja na kwamba ulikuwa ni ufalme uliotawala dunia, na uliowanufaisha Israeli kwa sehemu kubwa, hata kufikia wakati binti wa kiisraeli, (yaani Esta) kuwa Malkia wa dunia, lakini bado ufalme huo ulikuja kuanguka, kuonyesha kuwa Falme zote zitaanguka haijalishi ni Nzuri au Mbaya. Lakini ufalme wa Mmoja tu Yesu Kristo ndio utakaodumu milele. Sawasawa na maono aliyoyaona Nebukadreza.

Nebukadreza aliona jiwe lililochongwa pasipo kazi ya mikono, ikizipiga zile falme tano zilizotawala, (yaani Babeli, Umeni na Uajemi, Uyunani, na Rumi), na kuziangusha zote, na kisha jiwe hilo kuwa milima mikubwa iliyoijaza dunia yote. Na ufunuo wa jiwe hilo ni utawala wa Yesu Kristo, ambao ndio utazivunja falme hizo zote na utasambaa duniani kote.

Siku si nyingi parapanda ya mwisho italia, na wafu watafufuliwa na kwenda mbinguni, na hukumu ya mataifa waliosalia duniani itaanza, mataifa yataanguka yote na dunia itatikiswa, kabla ya kuanza utawala wa Mfalme Yesu Kristo, wa miaka elfu, ambao utasambaa ulimwenguni kote. Utakuwa ni utawala wa Amani kabla ya kuingia katika umilele katika mbingu mpya na nchi mpya.

Je utakuwa wapi siku hiyo? Utawala wa Farao ulipita, utawala wa Nebukadneza ulipita, utawala wa Malkia Esta ulipita, na tawala nyingine zote zilipita!, unadhani ni nini ambacho hakitapita kilichosalia katika huu ulimwengu?.. Vyote vitapita lakini Maneno ya Yesu Kristo hayatapita kamwe, alisema atarudi! Atarudi tu!, haijalishi dunia itasemaje!.. na atakuja kama mwivi.

Mathayo 24:35 “Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe”.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

UTAWALA WA MIAKA 1000.

Tofauti kati ya ufalme wa mbinguni na ufalme wa Mungu ni ipi?

YEZEBELI ALIKUWA NANI

IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.

MISTARI YA BIBLIA KUHUSU WATOTO.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/11/18/umedi-na-uajemi-zilitawalaje/