Nini maana ya “mtakayoyafunga duniani, yatakuwa yamefungwa mbinguni”?

by Admin | 9 December 2021 08:46 am12

Maneno hayo tunayasoma katika kile kitabu cha Mathayo 18:18,

Mathayo 18:18 “AMIN, NAWAAMBIENI, YO YOTE MTAKAYOYAFUNGA DUNIANI YATAKUWA YAMEFUNGWA MBINGUNI; NA YO YOTE MTAKAYOYAFUNGUA DUNIANI YATAKUWA YAMEFUNGULIWA MBINGUNI”

Sasa ili tuweze kuelewa vizuri tuanzie kusoma mistari ya juu kidogo, mstari wa 15

Mathayo 18:15 “Na ndugu yako akikukosa, enenda ukamwonye, wewe na yeye peke yenu; akikusikia, umempata nduguyo.

16 La, kama hasikii, chukua pamoja nawe tena mtu mmoja au wawili, ili kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno lithibitike.

17 Na asipowasikiliza wao, liambie kanisa; na asipolisikiliza kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru.

18 AMIN, NAWAAMBIENI, YO YOTE MTAKAYOYAFUNGA DUNIANI YATAKUWA YAMEFUNGWA MBINGUNI; NA YO YOTE MTAKAYOYAFUNGUA DUNIANI YATAKUWA YAMEFUNGULIWA MBINGUNI ”.

Katika mazingira kama hayo Bwana alimaanisha kuwa, inapotokea mtu mmoja (aliyeokoka), kafanya kosa basi unapaswa ukamwonye ukiwa wewe na yeye peke yenu, akikusikia na kutubu basi utakuwa umemwokoa kutoka njia ya upotevu (yaani umempata), lakini kama hajakusikia wewe baada ya kumwonya kimaandiko, maandiko yanasema ukachukue watu wengine wawili au watatu urudie mmwonye tena kwa pamoja na kama hataki kusikia basi kanisa liambiwe na aonywe na wengi zaidi na kama pia hataki kusikia na kutubu kwa kosa lake hilo au makosa yake…, maandiko yameruhusu mtu huyo kuachwa kama alivyo.

Na madhara ya kuachwa na kanisa kama alivyo ni makubwa kwasababu hayaishii tu hapa duniani, bali hata mbinguni mtu huyo anakuwa ameachwa (ametengwa na uwepo wa Mungu)..Hakuna chochote atakachovuna katika roho baada ya hapo, mpaka yeye mwenyewe atakapotubu..

Ndio maana kuna umuhimu mkubwa sana wa kuitii injili. Hususani tunapoisikia zaidi ya mara moja, pale inapotuonya, kwasababu tusipoitii, basi inageuka kwetu kuwa USHUHUDA, (yaani sababu ya kutuhukumu siku ile ya mwisho), na inakuwa inafungwa juu yetu, kwasababu tumeidharau, na inapofungwa juu yetu, maana yake imekuwa imetufungia na dhambi.

Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake maneno haya..

Marko 6:10 “Akawaambia, Mahali po pote mtakapoingia katika nyumba, kaeni humo hata mtakapotoka mahali pale.

11 Na mahali po pote wasipowakaribisha ninyi wala kuwasikia, MTOKAPO HUKO, YAKUNG’UTENI MAVUMBI YALIYO CHINI YA MIGUU YENU, KUWA USHUHUDA KWAO.

12 Wakatoka, wakahubiri kwamba watu watubu.”

Utaona pia katika kanisa la kwanza, sehemu nyingi mitume walipokuwa wakifika, na kuhubiri injili, wenyeji wa miji ile walipowakataa walikung’uta mavumbi na kuondoka kwenda miji mingine, maana yake ni kwamba tayari watu wa huo mji, mbingu zimefungwa juu yao, hakuna chochote cha kiroho watakachonufaika nacho baada ya hapo, (wanakuwa wamefungiwa dhambi sawasawa na Yohana 20:23) kwasababu wameidharau injili iliyoletwa kwao zaidi ya mara moja, ikiwataka watubu wamgeukie Mungu.

Matendo 13:50 “Lakini Wayahudi wakawafitinisha wanawake watauwa wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika mipaka yao.

51 NAO WAKAWAKUNG’UTIA MAVUMBI YA MIGUU YAO, WAKAENDA IKONIO”.

Hivyo Kaka/Dada, usidharau maonyo yoteyote ya Mungu yanayoletwa kwako, unapoonywa na kanisa juu ya uzinzi wako, juu ya huyo mwanamke/mwanaume wa kizinzi unayeishi naye, unapaswa uogope!, na kugeuka na kutubu haraka..Maana siku ile kanisa litakaposema basi!, na mbinguni kutakuwa ni BASI!!..Ni Mungu ndio kaamua iwe hivyo, si mwanadamu, ni Mungu ndio kaamua kanisa lake liwe na hayo mamlaka na si mwanadamu.. Na ni kwanini kaamua iwe hivyo, ni kwasababu kama hutaweza kumsikiliza ndugu mwenzako anayekuonya, au kulisikiliza kanisa, basi hata Kristo akikutokea hutaweza kumsikiliza, ndio maana kanisa litakaposeama basi, basi hata mbinguni nako ni Basi!

kwahiyo ni jambo la kuogopa sana!.. kadhalika usiidharau injili inayoletwa kwako, kwasababu siku ikiondolewa kwako, na ile nguvu ya kumrudia Bwana inakuwa haipo tena juu yako, hivyo itii injili yake leo, kwasababu anakupenda na anatupenda sote, hataki tuangamie, sawasawa na ahadi zake.

Luka 10:10 “Na mji wo wote mtakaouingia, nao hawawakaribishi, tokeni humo, nanyi mkipita katika njia zake semeni,

11 Hata mavumbi ya mji wenu yaliyogandamana na miguu yetu tunayakung’uta juu yenu. Lakini jueni hili, ya kuwa Ufalme wa Mungu umekaribia.

12 Nawaambia ya kwamba siku ile itakuwa rahisi zaidi Sodoma kuistahimili adhabu yake kuliko mji huo

13 Ole wako Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza hiyo iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu tangu hapo, huku wakiketi katika nguo za kigunia na majivu.

14 Lakini, siku ya hukumu itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zake kuliko ninyi.

15 Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa hata mbinguni? Utashushwa hata kuzimu.

16 Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma”.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/12/09/yatakuwa-yamefungwa-mbinguni/