FANYA BIDII ZOTE ULE MATUNDA YA UZIMA.

by Admin | 12 January 2022 08:46 pm01

Mwanzo 2:9

[9]BWANA Mungu akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.

Unaweza kujiuliza kulikuwa na sababu gani Mungu kuuweka mti wa ujuzi wa mema na mabaya pale bustanini wakati alikuwa anajua kabisa una kifo ndani yake?

Kwanini asingeuacha tu ule wa uzima na ile mingine ..ili mwanadamu aishi milele kwa furaha pale Edeni.

Je Ni kwamba Mungu hana mipango ya kueleweka kwa watu wake au?(tukizungumza kibinadamu)

Jibu la La! Nataka nikuambie mipango ya Mungu ni mikamilifu sikuzote na ni mizuri..tofauti na tunavyodhani kuwa ule mti  wa ujuzi wa mema na mabaya ulikuwa ni mbaya, haukustahili kuwepo pale.

Ukweli ni kwamba ule mti ulikuwa ni mzuri na unafaa sana, tena twamshukuru Mungu kwa kuuweka pale bustanini….Unajua ni kwasababu gani?

Ni kwasababu sisi kamwe tusingeweza kuwa kama Mungu, na malaika zake kama tusingepata ujuzi ndani yetu.

Kumbuka ujuzi ni jambo ambalo mwanadamu hakuumbiwa tangu mwanzo,  si asili yetu..sisi tuliumbwa kutokujua mambo kama aibu, ustaarabu, mipango, maamuzi, ibada n.k hayo yote yalikuja baada ya kula matunda yale,

Sasa, Mungu aliliona hilo tangu mwanzo, hivyo akaona  njia pekee ya kumkamilisha mwanadamu ili afanane na yeye ni kumpa ujuzi huo ndani yake..lakini aliona pia hatari yake..kwamba siku zote ujuzi una nguvu kubwa ya kupoteza,(1Wakorintho 8:1) hivyo akamtaadharisha mapema.

Ujuzi wa kujua mtu anahitaji kuishi katika nyumba na sio porini, kwamba anahitaji kujenga nyumba, kufanya biashara, kugundua vitu, kuvaa nguo na sio kukaa uchi, kujijengea mfumo n.k Mungu aliona mwisho wake utampoteza mtu, japo ujuzi wenyewe sio mbaya.

Ndipo akabuni njia ya kuweza kudhibiti tatizo hilo. Akaweka mti mwingine bustanini unaoitwa mti wa Uzima. Ambao mwanadamu akiyala matunda yake ataurejesha ule uzima ambao angeupoteza kwa kupokea ujuzi.

Na hapo mwanadamu atakuwa amepata faida mara mbili, kwanza ni kufanana na Mungu, pili ni kurejesha uzima wa milele.

Nachotaka ujue ni kuwa kila mwanadamu anayeishi  duniani..ujuzi huu upo ndani yake..Na ndio maana unaweza kujiamulia mambo yako mwenyewe, unaweza kusema hapana au ndio..unaweza kusema nataka au sitaki..huwi kama mnyama, Au kama roboti bali una ujuzi wote wa kufanya unachotaka mwenyewe bila hata kumtegemea Mungu, mwanadamu au shetani..

Lakini nakuambia hii ni hatari kubwa kwasababu uhuru huu wa kifikra umetufanya wanadamu ndio tuende mbali sana na Mungu wetu, tupotee kabisa, tuone Mungu ni nani, mbona tunaweza kufanya wenyewe bila yeye, rangi zetu pekee hazitoshi, tujichubue kidogo, tujichore tatoo kidogo tupendeze, tuvute sigara, tunywe pombe tuwe fresh, tuzini na Wanyama, kwani kuna shida gani? . Kwa kifupi ni kuwa tumepotea kama tutaishi katika hii hali pasipo kuifahamu kinga.

Tunauhitaji mti wa uzima. Na mti wenyewe ni YESU KRISTO. Hakuna namna utaweza kuishi kwa ujuzi wako, au akili zako bila Yesu Kristo kukusaidia. Mwisho wa siku utakufa tu na kupotelea motoni.

Yohana 14:6

[6]Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.

Watu wengi leo wanadhani elimu zao, ndio zitawapa maisha, wanadhani tafiti zao ndio zitawafikisha ng’ambo, wanadhani mawazo yao na imani zao na teknolojia zao na ustaarabu wao ndio zitakazowavusha..

Hawajui kuwa mioyo yetu sisi wanadamu huwa ni midanganyifu kuliko kitu chochote huku duniani.

Yeremia 17:9

[9]Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?

Na ndio maana Bwana Yesu alisema “Mtakufa katika dhambi zenu, kama msiposadiki kuwa mimi ndiye.”(Yohana 8:24)..tusipookolewa..hakuna tumaini ndugu. Bwana Yesu ndiye mti wenyewe wa uzima. Shusha kiburi chako, yasalimishe maisha yako kwake..akusaidie.

Siku hizi ni za mwisho, wakati wowote parapanda inalia hakuna mtu asiyelijua hilo, ipo wazi kulingana na dalili tunazoziona sasa. Hii dunia inafikia mwisho, mtafute Yesu Kristo, akuokoke na udanganyifu wa ujuzi.

Kama hujaokoka basi mkaribishe leo Yesu katika maisha yako, kisha ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo, kisha utapokea ondoleo la dhambi.

Mungu akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

HUTATAMBUA LOLOTE, SIKU YA UNYAKUO IKIFIKA.

USITUPE LULU ZAKO MBELE YA NGURUWE.

Nini maana ya kilichotarajiwa kikikawia kuja moyo huugua (Mithali 13:12)?.

Nini maana ya “yasiyokuwapo hayahesabiki”(Mh 1:15)

UFUNUO: Mlango wa 22

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/01/12/fanya-bidii-zote-ule-matunda-ya-uzima/