Je ni viatu gani Musa aliambiwa avivue?  Vya mwilini au vya rohoni? (Kutoka 3:5).

by Admin | 7 February 2022 08:46 pm02

Tusome,

Kutoka 3:5 “Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu.

Viatu Musa alivyoambiwa avivue ni vya mwilini kabisa!, na si vya rohoni. Na tunasoma si tu Musa peke yake bali hata Yoshua kuna mahali alifika akaambiwa avue viatu vyake (Yoshua 5:15).

Katika agano la kale Usafi mbele za Mungu ulithibitishwa kwa vitu vya nje!…kama kuoga, kunawa, kutawadha, kuvua n.k! Kwamfano watu walikuwa hawali chakula kabla hawajanawa mpaka kwenye viwiko..Mtu yeyote aliyekula bila kunawa alionekana ni mchafu (najisi), mbele za Mungu na wanadamu.

Marko 7:2 “wakaona wengine katika wanafunzi wake wakila vyakula kwa mikono najisi, yaani, isiyonawiwa.

3 Kwa maana Mafarisayo na Wayahudi wote wasiponawa mikono mpaka kiwiko, hawali, wakishika mapokeo ya wazee wao

4 tena wakitoka sokoni, wasipotawadha, hawali; na yako mambo mengine waliyopokea kuyashika, kama kuosha vikombe, na midumu, na vyombo vya shaba.”.

Ndivyo Mungu alivyotembea na watu wa agano la kale. (Usafi ulithibitika kwa vitu vya nje). Ndio maana tunaona hata hapo Musa alipokutana na Mungu alimwambia avue viatu vyake, kadhalika wakati Fulani Mungu alipotaka kukutana na wana wa Israeli na kusema nao katika mlima huo huo, aliwaambia  wafue nguo zao wawe safi (Kutoka 19:10).

Sasa kwanini Musa aambiwe avue viatu na si kitu kingine?.. Viatu ni vazi linalokanyaga uchafu wa kila aina njiani, kiatu hicho hicho hapa kinakanyaga taka, mbele kidogo kinakanyaga mavumbi..mbele tena kidogo kinakanyaga kinyesi cha mtu au mnyama.. hivyo si kitu kisafi!. Ndio maana Musa akaambiwa avue viatu vyake.

Lakini je! Hiyo ni sheria hata sasa?, kwamba tukitaka kwenda kwenye nyumba za ibada kukutana na Mungu ni lazima tuvue viatu vyetu, au tuoge au tutawadhe ili tusiwe najisi mbele za Mungu?

Jibu ni la!, Usafi wa nje, hautosogezi karibu na Mungu. Kutokuoga na kuingia kwenye nyumba ya ibada hakutufanyi tukataliwe na Mungu, vile vile kuingia katika nyumba ya Mungu na viatu mguuni hakutufanyi tuwe najisi.

Bwana Yesu alisema…

Mathayo 15:16 “Yesu akasema, Hata sasa ninyi nanyi mngali hamna akili?

17 Hamjafahamu bado ya kuwa kila kiingiacho kinywani hupita tumboni, kikatupwa chooni?

18 Bali vitokavyo kinywani vyatoka moyoni; navyo ndivyo vimtiavyo mtu unajisi.

19 Kwa maana MOYONI HUTOKA MAWAZO MABAYA, UUAJI, UZINZI, UASHERATI; WIVI, USHUHUDA WA UONGO, NA MATUKANO;

20 hayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi; LAKINI KULA KABLA HAJANAWA MIKONO HAKUMTII MTU UNAJISI”.

Lakini hiyo haitupi amri ya kuwa wachafu wakati wote!, kwamba tuifanye nyumba ya Mungu jalala!..au tusiwe watu wa kuoga, au tusiwe watu wa kunawa mikono kabla ya kula!. Tuna wajibu wa kuwa wasafi kwa kadri tuwezavyo!..na kuifanya nyumba ya Mungu kuwa safi wakati wote, kama viatu vina matope ni vizuri kuvisafisha nje kabla ya kuingia navyo ndani kwenye nyumba ya ibada (Hiyo inahitaji tu akili za kawaida, kupambanua!).. lakini sio kulifanya jambo hilo ndio msingi wa kumkaribia Mungu. La! Hatumkaribii Mungu kwa hayo mambo.

Hivyo tunapaswa tuvue viatu vya roho zetu, na si vya mwilini, viatu vyetu vya rohoni ndivyo vinavyobeba uchafu wa kila aina haya maisha!, ambao ndio huo Bwana alioutaja.. Uongo, mawazo mabaya, uasherati, uzinzi, wizi na mengine yote yanayofanana na hayo,

Je! Umempokea Yesu?, umeoshwa dhambi zako kwa damu?, viatu vya moyo wako umevivua?

Bwana Yesu yu karibu!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Gidamu ni nini? Kwanini Yohana alisema hastahili kuzilegeza gidamu za Yesu?

Tofauti kati ya uchafu wa mwilini na rohoni ni  ipi?

Tofauti ya kazi ya Damu ya Yesu na Jina la Yesu ni ipi?

YANAYOENDELEA SASA KATIKA MADHABAHU YA MUNGU ROHONI.

YANAYOENDELEA SASA KATIKA MADHABAHU YA MUNGU ROHONI.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/02/07/je-ni-viatu-gani-musa-aliambiwa-avivue-vya-mwilini-au-vya-rohoni-kutoka-35/