Ninyi mnaoimba nyimbo za upuzi pamoja na sauti ya vinanda.

by Admin | 26 February 2022 08:46 pm02

SWALI: Bwana alimaanisha nini katika mstari huu;

Amosi 6:5 “ninyi mnaoimba nyimbo za upuzi pamoja na sauti ya vinanda, na kujifanyizia vinanda vya namna nyingi, kama vile Daudi”

Je! alimkosa Daudi, kwa namna alivyokuwa anamsifu?


JIBU: Jibu ni la! Mstari huo haumaanishi kuwa Mungu anachukizwa na watu wanaomsifu kwa ala, na vyombo vingi vya muziki, hapana, kinyume chake anasisitiza sana tufanye hivyo, tena hiyo pia ilikuwa ni sababu nyingine iliyomfanya Mungu ampende Daudi..

Daudi kwa uvuvio wa Roho aliandika maneno haya;

Zaburi 150:3 “Msifuni kwa mvumo wa baragumu; Msifuni kwa kinanda na kinubi;

4 Msifuni kwa matari na kucheza; Msifuni kwa zeze na filimbi;

5 Msifuni kwa matoazi yaliayo; Msifuni kwa matoazi yavumayo sana.

6 Kila mwenye pumzi na amsifu Bwana. Haleluya”.

Umeona? Kuonyesha kuwa Mungu anapendezwa sana na kufisiwa kwa ala na midundo mbalimbali ya miziki.

Lakini sasa kwanini kwenye mstari huyo wa Amosi, anaonekana kama anawakemea watu wanaofanya hivyo?

Kumbuka hapo, anasema ninyi “mnaoimba nyimbo za upuzi”. Ikiwa na maana, wanachokiimba  hakimtukuzi Mungu, kinamfano wa ki-Mungu lakini ni cha kidunia, na pia hawamuiimbi Mungu katika Roho na Kweli, yaani, matendo yao, yapo mbali na Mungu halafu wanajifanya wanamwimbia yeye katika ustadi wa ala mbalimbali..

Ndicho walichokifanya wana Israeli hicho kipindi, walikuwa wanafanya maasi mengi, lakini wanajifanya wanajua kumtukuza Mungu kwa nguvu kama Daudi..Matokeo yake, Mungu akawazira kwa sifa zao za kinafki, akawapa adhabu ya kuchukuliwa utumwani Babeli..

Ukisoma mistari ya mbele kidogo Bwana anasema;

Amosi 6:8 “Bwana MUNGU ameapa kwa nafsi yake, asema Bwana, Mungu wa majeshi; Naizira fahari ya Yakobo, nachukizwa na majumba yake; kwa sababu hiyo nitautoa huo mji, pamoja na wote waliomo ndani yake.

9 Hata itakuwa, wakisalia wanaume kumi katika nyumba moja, watakufa”.

Umeona, mfano wa Kanisa la Kristo lililopo sasa.

Tuna vyombo vingi vya kisasa vya kumsifu Mungu, tuna magitaa, tuna maspika yenye nguvu, tuna mapiano, vinanda vya kisasa, matarumbeta n.k. jambo ambalo ni zuri kumsifu Mungu kwa namna hiyo. Lakini angalia kinachoimbwa sasa, na staili za uchezaji, ni ‘upuuzi’ sawasawa na maneno ya Bwana. Huwezi tofautisha nyimbo ya ki-Mungu na nyimbo za wasanii wa kidunia.

Na hata kama tutaimba maneno ya kumsifu Mungu, lakini angalia matendo yetu nyuma ya pazia, yapo mbali kabisa na wokovu na utakatifu.

Hivyo unabii huo unatuhusu sisi, tunapaswa tujirekebishe, ili Bwana asituzire kwa kutupa adhabu kama alivyowapa wana wa Israeli kwa kuwapeleka utumwani Babeli.

Biblia inasema tumwabudu Mungu katika uzuri wa utakatifu, Na Sio katika vinywa tu, na midundo, Ili tupokee baraka alizozikusudia katika kufanya hivyo.

1Nyakati 16:29 “Mpeni Bwana utukufu wa jina lake;…. Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu”;

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Matoazi na Matari ni nini? (Kutoka 15:20)

Kinubi ni nini katika biblia? (1Samweli 16:16, 23)

Zaburi maana yake nini, katika Biblia?

Amwimbiaye nyimbo mtu mwenye moyo mzito.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/02/26/ninyi-mnaoimba-nyimbo-za-upuzi/