USICHELEWE KUMPAKA BWANA MARHAMU!

by Admin | 14 March 2022 08:46 am03

Jina la Bwana, Yesu libarikiwe.

Kuna tofauti ya Marhamu na Manukato, kujua tofauti yake fungua hapa >> Marhamu na manukato ni nini?.

Lakini kwaufupi ni kwamba Marhamu ni pafyumu.

Sasa maandalio ya wayahudi kabla ya kuzika, ilikuwa ni desturi ya kumpaka maiti Marhamu kichwani, kisha Manukato yanafungiwa katika sehemu nyingine ya mwili. Na manukato hayakuwa katika mfumo wa kimiminika.

Lakini tunaona Bwana Yesu alipokufa, Yusufu yule mtu Tajiri Pamoja na Nikodemo waliandaa tu Manukato!, bila Marhamu na kwenda kuyafungia ndani ya mwili wa Bwana Yesu.

Yohana 19:38 “Hata baada ya hayo Yusufu wa Arimathaya, naye ni mwanafunzi wa Yesu, (lakini kwa siri, kwa hofu ya Wayahudi), alimwomba Pilato ruhusa ili auondoe mwili wake Yesu. Na Pilato akampa ruhusa. Basi akaenda, akauondoa mwili wake.

39 Akaenda Nikodemo naye, (yule aliyemwendea usiku hapo kwanza), AKALETA MACHANGANYIKO YA MANEMANE NA UUDI, YAPATA RATLI MIA.

40 Basi wakautwaa mwili wake Yesu, wakaufunga sanda ya kitani pamoja na YALE MANUKATO, kama ilivyo desturi ya Wayahudi katika kuzika”.

Lakini desturi ni kwamba, Maiti lazima apakwe pia Marhamu.. Lakini hapa tunaona hawakufanya hivyo!. Na utaona wale wanawake  walipanga kurudia hilo zoezi la kuupaka uso wa Bwana Marhamu siku ya kwanza ya juma baada ya sabato kuisha!…wangeupaka siku ile ile lakini tayari sabato, ilikuwa imeshaingia na kulingana na desturi za wayahudi, ilikuwa si ruhusa kufanya shughuli yoyote siku ya sabato!, hivyo ikawapasa wasubiri mpaka jumapili asubuhi.

Lakini chaajabu ni kwamba asubuhi walipokwenda wakiwa na Marhamu zao, Pamoja na manukato mengine hawakumkuta Bwana kaburini..Hivyo Marhamu zao zikawa hazina kazi tena!.

Luka 23:54 “Na siku ile ilikuwa siku ya Maandalio, na sabato ikaanza kuingia.

55 Na wale wanawake waliokuja naye toka Galilaya walifuata, wakaliona kaburi, na jinsi mwili wake ulivyowekwa.

56 Wakarudi, wakafanya tayari MANUKATO NA MARHAMU. Na siku ya sabato walistarehe kama ilivyoamriwa.

Luka 24:1 “Hata siku ya kwanza ya juma, ilipoanza kupambazuka, walikwenda kaburini, wakiyaleta manukato waliyoweka tayari.

2 Wakalikuta lile jiwe limevingirishwa mbali na kaburi,

3 Wakaingia, wasiuone mwili wa Bwana Yesu”.

Umeona hapo?.. wenyewe walikuja kwa lengo la kuupaka uso wa Bwana Yesu  marhamu na  mwili wake kuufungia manukato!, lakini hawakumkuta!..walikuwa wamechelewa.. Kumbe nafasi ya kumpaka Marhamu kichwani ilikuwa ni kipindi yupo hai!, si kipindi amekufa kama wafu wengine wanavyofanyiwa..

Na utaona yule mwanamke wa kwanza alipata huo ufunuo, na akawahi kumpaka Bwana Marhamu ya thamani kichwani mwake, na Bwana Yesu akawaambia watu “AMEFANYA VILE KUMWEKA TAYARI KWA MAZIKO YAKE”..Na popote injili itakapohubiriwa.. itahubiriwa kwa kumbukumbu lake!.

Mathayo 26:6 “Naye Yesu alipokuwapo Bethania katika nyumba ya Simoni mkoma,

7 MWANAMKE MWENYE KIBWETA CHA MARHAMU YA THAMANI KUBWA ALIMKARIBIA AKAIMIMINA KICHWANI PAKE ALIPOKETI CHAKULANI.

8 Wanafunzi wake walipoona, wakachukizwa, wakasema, Ni wa nini upotevu huu?

9 Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa fedha nyingi wakapewa maskini.

10 Yesu akatambua akawaambia, Mbona mnamtaabisha mwanamke? Maana ni kazi njema aliyonitendea mimi.

11 Kwa maana siku zote mnao maskini pamoja nanyi; lakini mimi hamnami siku zote.

12 MAANA KWA KUNIMWAGIA MWILI WANGU MARHAMU HIYO, AMETENDA HIVYO ILI KUNIWEKA TAYARI KWA MAZIKO YANGU.

13 Amin, nawaambieni, Kila patakapohubiriwa Injili hii katika ulimwengu wote, tendo hilo alilolitenda huyu litatajwa pia kwa kumbukumbu lake”.

Na kwa heshima yake, utaona Bwana Yesu alipofufuka, vile vitambaa vya sanda vilifunguliwa na kuachwa pale, lakini ile LESO ya kichwani, maandiko yanasema “ilizongwa zongwa pembeni (Yohana 20:7)”.. maana yake ilikunjwa vizuri na kuwekwa pembeni..

Sasa kwanini ikunjwe na kuwekwa pembeni?, ni kuonesha uthamani wa leso ile, kwamba isitupwe, bali iwekwe ije itumike tena!!..kwasababu bado inafaa kwa matumizi, na kufaa huko ni kutokana pia na ile Marhamu yule Mwanamke aliyompaka Bwana siku chache nyuma kabla ya kufa kwake!

Nini tunajifunza hapo?

Kuna wakati unaofaa wa kumfanyia jambo Bwana, na pia upo wakati usiofaa!!.. Ukipata nafasi ya kumtolea Bwana fedha zako, au mali zako, au muda wako.. Mtolee sasa usingoje siku Fulani mbeleni ifike. Huo muda unaoungoja ukifika, utakapokwenda kumfanyia Bwana huduma utakuwa sio muda unaofaa..

Akina Mariamu Magdalene na wenzake, ni kweli walikuwa wana nia nzuri ya kwenda kumpaka Bwana Marhamu lakini walikuwa wamechelewa, Bwana havihitaji tena hivyo vitu kwa wakati huo!!…

Aliwaambia wale watu, “maskini mnao siku zote, lakini mimi hamnami siku zote”.

Ndugu, Watoto wako unao siku zote, ndugu zako wenye shida unao siku zote, Rafiki zako wenye matatizo unao siku zote, lakini kazi ya Bwana haipo kwako siku zote!, mfanyie Bwana kitu leo usingoje kesho.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

LIPI TUNAJIFUNZA KWA WALIOMWONA YESU ALIYEFUFUKA?

LIPI TUNAJIFUNZA KWA WALIOMWONA YESU ALIYEFUFUKA?

BIBLIA INAITAJA NJIA KUU YA MFALME, NJIA HII NI IPI?

TABIA YA WAZI INAYOWATOFAUTISHA MANABII WA UONGO NA WALE WA UKWELI.

Naivera ni nini? Kwanini Daudi aliihitaji alipomtafuta Mungu?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/03/14/usichelewe-kumpaka-bwana-marhamu/