by Admin | 15 March 2022 08:46 pm03
Moja ya mambo ambayo yanadhoofisha karama, au yanamchelewesha mtu kuifanya kazi ya Mungu, ni tabia ya kusubiria Mungu amwambie jambo Fulani, au Mungu amwoneshe jambo kwanza.
Watu wengi sana leo hii wamekuwa watu wa kungojea ngojea!.. Utamwuliza mtu kwanini huanzi kuifanya kazi ya Mungu?.. Jibu atakalokupa ni “nangojea wakati wa Bwana” au “Nangoja Bwana aniambie kwanza au anioneshe kwanza”. Na ilihali kashamwamini Yesu na kupokea Roho Mtakatifu.
Leo nataka nikuambie ndugu yangu.. Usiendelee kungoja!!.. Nenda kaanze kumtumikia Bwana, maadamu umeshamwamini Bwana Yesu, na kubatizwa na kupokea Roho Mtakatifu, usisubiri maono, wala sauti ikuambie nenda kanitumikie!.. “Hiyo utaingoja sana”.. Anza sasa.
Utauliza nitaanzaje anzaje sasa?
Usiogope, Roho Mtakatifu aliye ndani yako atakufundisha na kukuongoza!.. hutaanza katika ukamilifu wote lakini utaishia katika ukamilifu, kwasababu Roho Mtakatifu yu Pamoja nawe, kukufundisha cha kusema au cha kufanya, anachosubiri kutoka kwako ni wewe tu kuchukua hatua ya kuanza.
Luka 12:11 “Na watakapowapeleka ninyi mbele ya masinagogi na maliwali na wenye mamlaka, msifadhaike kwa kuwaza maneno yenu jinsi mtakavyojibu au kusema;
12 kwa kuwa Roho Mtakatifu atawafundisha saa ile ile yawapasayo kuyasema”.
Hakikisha unamtumikia Mungu tu! Katika Neno lake, hayo mengine mwachie yeye!.
Sasa utazidi kuuliza ni kwa namna gani??..kama sipaswi kungoja kusikia sauti, nitasemaje au nitafanyaje?..
Jibu ni rahisi, kama tayari umeshampokea Roho Mtakatifu, Songa mbele, FANYA KAMA UONAVYO VYEMA!
1. Kama unaona ni vema wewe kumwimbia Mungu, Basi fanya hivyo kwa bidii.. usisubiri uambiwe au uone maono, au Malaika akutokee.
2. Kama unaona ni vema wewe kuhubiri, basi anza kufanya hivyo hata kama unajiona huna ujasiri, Bwana atakupa ujasiri pale tu utakapotia nia ya kuanza kuwahubiria watu.
3. Kama unaona ni vema wewe kuishikilia kazi ya Mungu kwa maombi au michango!, usingoje uwekewe mikono, au Roho Mtakatifu akuambie, wewe fanya na Bwana atakuwa na wewe, na kukupa kibali.
4. Kama unaona ni vema wewe kuwafundisha Watoto, basi usingoje ngoje, anza kufanya kazi hiyo,. Kwasababu ni Roho Mtakatifu kaliweka hilo ndani yako.
5. Kama unaona ni vema wewe kuhubiri mitaani, au mitandaoni, usisubiri utokewe na Bwana, wala usiseme ngoje, wakati Fulani ufike ndio uanze!, anza sasa!
6. Kama unaona vema kuandaa Makala mbali mbali au kuchapisha vitabu vya mahubiria au mafundisho, basi fanya hivyo usingoje ngoje, usizidi kupoteza muda, kwasababu Muda haukungoji wewe. Na mambo mengine yote!, usingoje.. FANYA KAMA UONAVYO VEMA.
Ili tujifunze Zaidi, hebu tuutazame wito wa Mfalme Sauli, jinsi Mungu alivyompaka mafuta, na jinsi alivyoagizwa namna ya kuuongoza ufalme aliopewa!.
Sauli baada ya kupakwa mafuta na nabii Samweli ya kuwa mfalme wa kwanza wa Israeli, alikuwa anajiuliza uliza atawezaje kutawala, atafanyaje fanyaje!. Lakini Nabii Samweli alimpa maneno makubwa sana yaliyompatia Mwanga!.. na maneno hayo ni kwamba.. “BAADA TU YA KUPOKEA ROHO, BASI AFANYE KAMA AONAVYO VEMA”.
Tusome,
1Samweli 10:1 “Ndipo Samweli akatwaa kichupa cha mafuta, akayamimina kichwani pake, akambusu, akasema, Je! Bwana hakukutia mafuta [uwe mkuu juu ya watu wake Israeli? Nawe utamiliki watu wa Bwana, na kuwaokoa na mikono ya adui zao; kisha hii itakuwa ishara kwako ya kuwa Bwana amekutia mafuta] uwe mkuu juu ya urithi wake.
2 Utakapoondoka kwangu leo, utakutana na wanaume wawili karibu na kaburi la Raheli, katika mpaka wa Benyamini huko Selsa; nao watakuambia, Punda hao uliokwenda kuwatafuta wameonekana; na tazama, baba yako ameacha kufikiri habari za punda, anafikiri habari zenu, akisema, Nifanye nini kwa ajili ya mwanangu?
3 Kisha utakwenda mbele kutoka hapo, na kufika kwa mwaloni wa Tabori, na hapo watu watatu watakutana nawe, wanaokwea kumwendea Mungu huko Betheli, mmoja anachukua wana-mbuzi watatu, na mwingine anachukua mikate mitatu, na mwingine anachukua kiriba cha divai;
4 nao watakusalimu na kukupa mikate miwili; nawe utaipokea mikononi mwao.
5 Baada ya hayo utafika Gibea ya Mungu, hapo palipo na ngome ya Wafilisti; kisha itakuwa, utakapofika mjini, utakutana na kundi la manabii wakishuka kutoka mahali pa juu, wenye kinanda, na tari, na kinubi, na filimbi mbele yao, nao watakuwa wakitabiri;
6 na roho ya Bwana itakujilia kwa nguvu, nawe utatabiri pamoja nao, nawe utageuzwa kuwa mtu mwingine.
7 Basi, hapo ishara hizi zitakapokutukia, FANYA KAMA UONAVYO VEMA; KWA KUWA MUNGU YU PAMOJA NAWE”.
Umeona hapo mstari wa 7??.. Samweli hakuendelea kumpa maagizo kwamba, baada ya ishara hizo, aende akatwae jeshi, au aende akatawale watu kwa namna hii au ile, bali alimwambia tu maneno haya machache… “hapo ishara hizi zitakapokutukia, FANYA KAMA UONAVYO VEMA; KWA KUWA MUNGU YU PAMOJA NAWE”.
Maana yake jinsi ya kutawala, afanye jinsi aonavyo, kwasababu Mungu yu Pamoja naye..hataruhusu ajikwae wala akose, atamlinda na mashauri ya adui, hivyo yeye kile kijacho kichwani mwake maadamu ni cha kujenga, basi akifanye asiogope!, asianze kusubiri maono na ishara!.
Hali kadhalika na wewe leo!… Umeshamwamini Bwana Yesu, umeshabatizwa na tena umepokea Roho Mtakatifu.. unachosubiria ni nini???..Ishara ya mwisho ya Roho Mtakatifu imeshatimia juu yako unachosubiri ni nini??...HARAKA SANA FANYA UONAVYO VEMA, KWASABABU ROHO MTAKATIFU HAKUDHARAU.
Lakini kama bado hujampokea Yesu usifanye lolote kwanza!!..kwasababu utaharibu badala ya kujenga!.. Mpokee Yesu kwanza, na ubatizwe kwa ubatizo sahihi wa maji tele (Yohana 3:23), na kwa jina la BWANA YESU KRISTO (Matendo 2:38). Baada ya hapo Roho Mtakatifu ataingia ndani yako na kukuongoza katika kweli yote!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/03/15/fanya-kama-uonavyo-vema/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.