NIFANYE NINI ILI NIPENDWE NA MUNGU?

by Admin | 20 April 2022 08:46 pm04

Ni jambo la kawaida katika familia yoyote, si Watoto wote watakuwa na mahusiano sawa na wazazi wao. Wapo ambao wataonekana kuaminiwa Zaidi ya wengine, wapo ambao watapendwa Zaidi ya wengine, pia wapo ambao watategemewa na wazazi wao kuliko wengine,  n.k. Lakini hilo haliwafanyi wale wengine wasiwe Watoto wa wazazi wao.

Inatokea hivyo, kutokana na aidha tabia zao, ujuzi  au nafasi walizonazo. Vivyo hivyo na kwa Mungu katika familia yake ya watakatifu (Waliookoka), Si watakatifu wote watakuwa vipenzi wa Mungu, si wote wataaminiwa na Mungu, na si wote watategemewa na Bwana. Lakini hayo hayawafanyi hao wengine wasiwe Watoto wa Mungu.

Leo tutatazama mambo ambayo tukiwa nayo, basi tujue tutakuwa Watoto ambao tutapendwa sana na Mungu. Hivyo Ili tufahamu hayo tutaangalia katika biblia, mifano ya watu watatu (3) ambao, walipendwa na Mungu, ili na sisi tuige tabia kama zao tupendwa na Mungu.

Tabia ya kwanza ni Upendo.

Upendo ndio tabia ya kwanza itakayokuzogeza karibu na Mungu, na upendwe sana. Kati ya mitume 12 wa Bwana Yesu, Mtume Yohana peke yake ndiye aliyependwa na Yesu sana. Mpaka akawa muda wote anaegemea kifuani pake.

Yohana 21:20 “Petro akageuka akamwona yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu anafuata; (ndiye huyo aliyeegama kifuani pake wakati wa kula chakula cha jioni, akasema, Bwana, ni nani akusalitiye?)

21 Basi Petro akamwona huyo, akamwambia Yesu, Bwana, na huyu je?

Lakini lililomfanya apendwe na Yesu, ni upendo ambao aliuiga kutoka kwake. Na ndio maana utaona injili zake zote anahimiza upendo, kwasababu Mungu mwenyewe ni Upendo. Hivyo ili na sisi tupendwe na Bwana, hatuna budi kuonyesha bidii katika kupendana,

Na tabia za upendo tunazisoma katika 1Wakorintho 13:4-8….ambazo ni hizi;

13.4 Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni;

13.5 haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya;

13.6 haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli;

13.7 huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.

13.8 Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika.

Tabia ya pili ni Kuwa na moyo thabiti kwa Mungu.

Maana yake, ni kuwa tayari kukataa mambo yote yanayoweza kukukosesha na Mungu bila kujali gharama/hasara gani utakayoingia kwa kutokufanya hivyo. Huo ndio uthabiti wa moyo Mungu anaoutaka. Ambao alikuwa nao Danieli, ndio uliomfanya Mungu ampende sana.

Danieli 10:11 “Akaniambia, Ee Danieli, mtu upendwaye sana, yafahamu maneno nikuambiayo, ukasimame kiwima-wima; maana kwako nimetumwa sasa. Na aliponiambia neno hili, nalisimama nikitetemeka.

Soma pia Danieli 10:19,

Unaona Danieli, alikuwa ni mtu aliyependwa sana. Hiyo yote ni kutokana na moyo wake wa msimamo, tangu alipoingia kule Babeli wakati wayahudi wote, wapo vuguvugu, akiwa bado ni kijana mdogo alipoitwa akae katika milki za mfalme hakusita kutaa vyakula najisi vya kifalme..Na hata bado akiwa mzee, walipotaka kumzuia asimwabudu Mungu wake, bado aliendelea kumwabudu kutwa mara tatu, bila kuogopwa kutupwa katika tundu la simba.

Moyo kama huo unaonyesha upendo mkamilifu kwa Mungu wake, hivyo Mungu naye angeonyesha upendo wake tu. Na ndio maana Danieli kila alipotembelewa na Malaika alianza kwa kuambiwa mtu upendwaye sana.

Vivyo hivyo na sisi, katika mambo yetu, Ikiwa boss wako/ kazi yako vinakuzuia usiwe karibu na Mungu wako kwa ule muda unaokupasa umwabudu. Ukionyesha uthabiti, kwamba ni lazima ukamtumikie Bwana wako, ukamfanyie ibada, Bwana atakupenda..Ikiwa kazini kwako wanakulazimisha uvae suruali na vimini wewe kama binti uliyeokoka, ukakataa na kusema Imani yangu hainiruhusu bila kuogopa kufukuzwa kazi, basi ujue, upo katika njia ya kupendwa na Mungu kama Danieli.

Mwisho, Tafuta kuwa na Hekima, ya kuwasaidia watu wa Mungu.

Sulemani, ni mtu mwingine ambaye biblia inatuambia alipendwa na Mungu. Tunalithibitisha hilo katika,

Nehemia 13:26 Je! Sulemani, mwana wa Daudi, hakufanya dhambi kwa kutenda hayo? Lakini katika mataifa mengi hapakuwa na mfalme mwingine mfano wake. TENA ALIPENDWA NA MUNGU WAKE, naye Mungu akamfanya mfalme juu ya Israeli; walakini wanawake wageni walimkosesha hata yeye.

Ni kwasababu gani? Ni  kwasababu yeye hakuwa kama wafalme wengine, kama Sauli, ambao akili zao zilielekea katika kutawala tu, na vita  dhidi ya maadui. Bali yeye alitamani kupata njia ya namna ya kuyatengeneza mambo kwa hekima, watu wa Mungu wafurahi katika Bwana na kumtimikia katika utulivu. Ndipo Mungu akasikia ombi lake, akampatia. (1Wafalme 3:1-15)

Ndio hapo utaona hata vile ambavyo hakuomba, kama vile Mali Mungu alimpatia, kwasababu alipendwa sana na Mungu kwa kile alichokitamani. Na kama isingekuwa yeye mwenyewe kuja kukengeuka mwishoni, basi angekuwa ni mfano mkubwa sana wa kuigwa katika biblia nzima.

Vivyo hivyo na wewe, ukiitafuta hekima, ujue unatafuta kupendwa na Mungu, na hekima ya Mungu ipo katika Neno lake. Ukiwa ni mtu wa kujifunza biblia, na sio msomaji tu, kama gazeti, Hekima hiyo itaingia yenyewe moyoni mwako (Mithali 2:10). Na Mungu atakusaidia kuwapa wengine neema hiyo. Na mwisho wa siku utapendwa na Mungu.

Hekima zote za kimaisha, za kiutumishi, za kifamilia, za kijamii, zipo katika Neno la Mungu. Hivyo hakuna namna utaweza kuishi bila kusoma biblia.

Hivyo mambo hayo matatu tukiyachanganya. Yaani UPENDO, UTHABITI WA MOYO, NA HEKIMA.

Basi tujue kupendwa na Mungu, ni lazima kutatokea tu kwetu, . Na faida yake ni kuwa, tutaonyeshwa na mambo makubwa Zaidi ya tunayoyajua. Danieli na Yohana ndio waliopewa siri za nyakati za mbeleni. Na mpaka sasa tunagemea sana nabii zao ili kutambua nyakati na majira ya siku za Mwisho. Vilevile hata na vyote tunavyovisumbukia vya mwilini, ikiwa tutapendwa na Mungu basi yeye mwenyewe atavisogeza karibu na sisi. Kama alivyofanya kwa mtumwa wake Sulemani, na Danieli.

Bwana akubariki, na nikutakie kupendwa kwema na Bwana.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Group la whatsapp Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

UPENDO NI NINI NA JE! KUNA AINA NGAPI ZA UPENDO?

Na ulimi laini huvunja mfupa.(Mithali 25:15)

NITAUPATAJE UPENDO WA KI-MUNGU NDANI YANGU?

Donda-Ndugu ni nini?

MAISHA ULIYOPITIA NYUMA NI USHUHUDA TOSHA WA WEWE KUMTUMIKIA MUNGU

Kile kinara cha Taa ndani ya Hekalu la Sulemani kilikuwa kinawakilisha nini?

Moabu ni nchi gani kwasasa?

Kigao ni nini? Na Je kinafunua nini kwa agano jipya?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/04/20/nifanye-nini-ili-nipendwe-na-mungu/