WEWE U MUNGU UONAYE.

by Admin | 6 January 2023 08:46 am01

Mafundisho maalumu kwa ajili ya waajiriwa: Sehemu 1

Wewe U Mungu uonaye

Kwa kuwa tupo katika huu ulimwengu, na hivyo Bwana ametuagiza tufanye kazi za mikono (kwa sisi ambao hatuna huduma ya kudumu madhabahuni kwa Bwana).  tumeona ni vema pia tuwe na madarasa, ambayo, yatatupa mwongozo, wa namna ya kuishi katika maisha ya kazi. Na kama tujuavyo, kazi imegawanyika katika makundi mawili

  1. Ya Kujiajiri
  2. Ya Kuajiriwa

Lakini, watu wengi wameangukia sana katika hilo kundi la pili(Yaani kuajiriwa). Hivyo leo tutaangazia hapo. Kazi ya kuajiriwa maana yake ni kuwa ni sharti mtu awekwe chini ya mwajiri (Boss) wake. Tutatazama kimaandiko, migogoro inayotokea mara nyingi katika kazi za kuajiriwa.

Watu wengi ukiwauliza, shida ni nini? Mbona huna raha na kazi yako? Watakuambia shida ni boss wangu, mwingine atasema haniamini, mwingine atasema ananionea wivu, mwingine atasema ni mbinafsi sana, anawapandisha wengine cheo hanipandishi mimi,mwingine atasema hatujali wafanyakazi, n.k. n.k.

Lakini  wewe kama mkristo hupaswi umfikirie kiongozi wako, kwa jicho hilo, kwasababu, hata kama kweli anazo hizo tabia zinazokukwamisha, bado hawezi kuzuia kufanikiwa yako, au maono ambayo Mungu amekuwekea mbele yako.

Embu tutafakari kile Kisa cha Sarai na kijakazi wake Hajiri..Biblia inasema Sarai mwenyewe ndiye, aliyemwambia mumewe Abramu, amwingilie kijakazi wake ili ampatie uzao.. Wazo hilo halikuwa la Hajiri wala Abramu,. Kwa namna nyingine tunaweza kusema, Sarai alikusudia kumpandisha cheo kijakazi wake Hajiri, aonekane na yeye kama ni sehemu ya wake wa Ibrahimu.

Lakini mambo yalikuja kubadilika mbeleni, Hajiri alipoonekana ana mimba, Sarai akaanza kumtesa mama Yule. Na sababu ya kumtesa sio kwamba alimwonea wivu, hapana, bali aliona tabia za Hajiri zimebadilika ghafla hataki tena kuishi kama kijakazi bali anataka kuishi kama mke-mwenza, akiambiwa na Sarai aoshe vyombo anasema embu, niache hujui kama mimi ni mzazi!.

Hivyo Sarai kuona vile akaanza kumtesa, na kufadhaisha, mpaka uzalendo ukamshinda,Yule binti, ikabidi akimbilie jangwani huko akafie mbali. Lakini akiwa njiani, malaika alimtokea, akamwambia unakwenda wapi, akasema ninamkimbia bibi yangu Sarai kwasababu ananitesa nusu aniue,..Malaika akamwambia, Rudi kwa boss wako UKANYENYEKEE..

Tuisome habari..

Mwanzo 16:1 “Basi Sarai mkewe Abramu hakumzalia mwana, naye alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake Hajiri.  2 Sarai akamwambia Abramu, Basi sasa, Bwana amenifunga tumbo nisizae, umwingilie mjakazi wangu labda nitapata uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai.  3 Sarai mkewe Abramu akamtwaa Hajiri Mmisri mjakazi wake, baada ya kukaa Abramu katika nchi ya Kanaani miaka kumi, akampa Abramu mumewe, awe mkewe.  4 Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata mimba. Naye alipoona ya kwamba amepata mimba, bibi yake alikuwa duni machoni pake.  5 Sarai akamwambia Abramu, Ubaya ulionipata na uwe juu yako; nimekupa mjakazi wangu kifuani mwako, naye alipoona kwamba amepata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake. Bwana na ahukumu kati ya mimi na wewe.  6 Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake.  7 Malaika wa Bwana akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya kuendea Shuri.  8 Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi, nawe unakwenda wapi? Akanena, Nakimbia mimi kutoka mbele ya bibi yangu Sarai.  9 Malaika wa Bwana akamwambia, Rudi kwa bibi yako, UKANYENYEKEE CHINI YA MIKONO YAKE.  10 Malaika wa Bwana akamwambia, Hakika nitauzidisha uzao wako, wala hautahesabika kwa jinsi utakavyokuwa mwingi.  11 Malaika wa Bwana akamwambia, Tazama! Wewe una mimba, utazaa mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Ishmaeli, maana Bwana amesikia kilio cha mateso yako.  12 Naye atakuwa kama punda-mwitu kati ya watu, mkono wake utakuwa juu ya watu wote na mkono wa watu wote utakuwa juu yake, naye atakaa mbele yao ndugu zake wote.  13 Akaliita jina la Bwana aliyesema naye, WEWE U MUNGU UONAYE, kwani alisema, Hata hapa nimemwona yeye anionaye”?

Tafakari kwa umakini hiyo habari..

Rudi ukanyenyekee, Mungu anajua kuwa unateswa, lakini wakati mwingine ni kwasababu ya kukosa  kwako unyenyekevu..Rudi, kwasababu Baraka zako haziwezi kuzuiliwa na  mtu yeyote kama mtoto utazaa tu, naye atakuwa taifa kubwa..Na kweli Hajiri akatii, japo hapo mwanzo alidhani kuwa Mungu haoni mateso yake..lakini hapa mpaka akasema, hakika  “Wewe U Mungu uonaye”

Ndugu uliyeajiriwa, hakuna mtu anamchukia “mnyenyekevu”, usishindane na boss wako, hata kama ni mkali, wala usimkimbie, ukaacha kazi kwasababu za chuki, na fitina n.k., unaweza usipate nyingine nzuri kama hiyo.. bali kuwa tu mtulivu, kwasababu “Yupo aonaye”..Ukidhulumiwa mshahara “Yupo aonaye”.. Baraka zako zipo palepale. Yusufu alinyanyuliwa visa na boss wake wa kike, akawekwa gerezani, lakini mwisho wake tunaujua.

Hivyo zingatia hilo kama mkristo, katika maisha ya kuajiriwa,kuwa mnyenyekevu, ili uifurahie kazi yako.

 na Bwana atakubariki.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Biblia inasemaje kuhusu Kazi?

JINSI MUNGU ATAKAVYOTOA THAWABU ZAKE, NA VIGEZO ATAKAVYOTUMIA. (Sehemu ya 3)

Biblia inapotumia neno “Bila kazi ya mikono”, ina maana gani?

USIISHI BILA KUIFANYA KAZI YA MUNGU KABISA..

Moyo wake mwenye hekima upo upande wa kuume, maana yake nini?

Maji ya Zamzam yapo kibiblia?

JE! UNAMPENDA BWANA?

MIEZI 13 YA KIYAHUDI.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/01/06/wewe-u-mungu-uonaye/