Nini maana ya Mhubiri 10:16, inaposema Ole wako, nchi, akiwa mfalme wako ni kijana?

by Admin | 1 June 2023 08:46 pm06

Mhubiri 10:16 “Ole wako, nchi, akiwa mfalme wako ni kijana, Na wakuu wako hula asubuhi!”


Mstari huu umegawanyika katika sehemu mbili;

  1. Sehemu ya kwanza ya huu mstari inasema Ole wako, nchi, akiwa mfalme wako ni kijana.
  2. Na ya pili ni hiyo, ikiwa wakuu wako hula asubuhi.

Tuitazame sehemu ya kwanza: mfalme kijana.

Hapo mhubiri anajaribu kueleza uhusiano uliopo kati ya uongozi na ukomavu wa mtu. Akatumia mfano wa kijana, kwasababu mara nyingi ni ngumu sana kuipata busara kwa vijana,  kutokana na kuwa hawana uzoefu mwingi wa maisha na pia hawajaandaliwa vya kutosha, kumudu nafasi za uongozi, kinyume chake kitakachowaongoza ni hisia tu za ujana na si vinginevyo. Na ndio maana mtu kama Sulemani alilitambua hilo alipotawadhwa tu mfalme akiwa bado kijana mdogo, alimwomba Mungu ampe hekima ya namna ya kuwaongoza watu wake. Na Bwana akamjalia.

1Wafalme 3:7 “Na sasa, Ee Bwana, Mungu wangu, umenitawaza niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo tu; sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia. 

8 Na mtumwa wako yu katikati ya watu wako uliowachagua, watu wengi wasioweza kuhesabiwa, wala kufahamiwa idadi yao, kwa kuwa ni wengi. 

9 Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi?  10 Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, ya kuwa Sulemani ameomba neno hili”

Walikuwepo pia wafalme wengine waliotawadhwa wakiwa wadogo kama Yoashi, lakini akasaidiwa na kuhani Yehoyada katika ufalme wake, na ukawa bora (2Wafalme 11-12)

 Lakini tunakuja kuona kwa mwanawe Sulemani aliyeitwa Rehoboamu. Yeye naye alikuwa ni kijana lakini hakutaka mashauri kwa wazee waliomtangulia, kinyume chake, akasikiliza mashauri ya vijana wenzake Hivyo ikapelekea ufalme wake kugawanyika, na kupoteza makabila kumi kati ya kumi na mbili ya Israeli.(Soma 1Wafalme 12:1-16)

Lakini sehemu ya pili ya mstari huu inasema Ole wako nchi ikiwa wakuu wako hula asubuhi.

Maana yake kwamba kuwa na viongozi ambao wanatanguliza maslahi yao kabla ya kazi, nchi hiyo sikuzote huishia pabaya. Sikuzote watu wanakwenda kufanya kazi asubuhi, wakitarajia kile walichokihangaikia kutwa nzima ndio wakifaidi jioni, lakini hapa tunaona ni kinyume chake. Na jambo hili ni kweli, Tunaona katika baadhi ya mataifa yanayoendelea, wananchi wao wanapitia katika taabu, na umaskini wa hali ya juu, kutokana na kuwa viongozi wao, wanatazama maslahi yao binafsi wanapoingia madarakani na sio maslahi ya taifa.. Uchu wa madaraka na ukuu, ndio wanachokitazama lakini sio kujenga mataifa yao.

Hii inafunua nini rohoni?

Neno hili linawahusu, watumishi wote wa Mungu wanaosimama katika ngazi za uongozi. Ikiwa wewe bado ni kijana au mchanga katika huduma(hata kama una-mvi) na umepewa kundi ulichunge, Omba sana hekima kwa Mungu, pia kuwa tayari kujifunza kwa waliokutangulia, Sikuzote viongozi-wachanga, katika hatua za awali wanajiamini kuwa wanajua kila kitu, lakini kwa jinsi siku zinavyozidi kwenda ndivyo wanavyotambua kasoro zao nyingi. Hivyo ili kuepuka, kufanya makosa ya kiutumishi, tafuta sana msaada kwa Mungu katika hekima na mashauri.

Lakini pia, ikiwa wewe ni mchungaji, askofu, mtume, mwalimu, au unatumika katika huduma yoyote, epuka tamaa hususani ya mali. Si kila shilingi unayoipata uipeleke tumboni, au kujijengea majumba na biashara. Ni heri ukatazama kwanza hali ya kanisa la Kristo. Kama mchungaji mwema yakupasa kuipendezesha kwanza nyumba ya Bwana, kisha Baadaye Bwana mwenyewe ndio akupendezeshe wewe. Unatembelea gari ya Tsh milioni 40, halafu kanisa ni la makuti, Hapo ni nini unategemea kama sio ufukara wa kiroho hadi kimwili baadaye.

Kwahiyo hekima hizi zinatuonya, ili uongozi wetu usianguke mbeleni, hivyo tuzingatie sana maneno haya ya hekima. Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312 Au jiunge na makundi yetu ya mafundisho ya kila siku kwa kwa njia ya Whatsapp kwa kubofya hapa >>>> WHATSAPP GROUP

Mada Nyinginezo:

NJIA YA ‘UTAJIRI MKUU’ KWA KIJANA.

Je ile nyota ya asubuhi inamwakilisha shetani au Bwana Yesu?

VIJANA NA MAHUSIANO.

Bwana Yesu alikufa akiwa na umri gani?

Vifungu vya biblia kuhusu Uongozi.

NITAJUAJE KAMA MAOMBI YANGU YAMEFIKA (YAMEJITOSHELEZA)?

Makerubi wenye sura nne, ni kweli wapo? na je! wanyama wataenda mbinguni?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/06/01/nini-maana-ya-mhubiri-1016/