MAOMBI MAALUMU YA WA-WAMAMA / WANAWAKE WA KANISANI.
by Admin | 1 January 2024 08:46 pm01
Kama mwanamke uliyeokoka. Fahamu kuwa una wajibu wa kujiombea wewe, kuombea jinsia yako, na kuliombea Kanisa la Kristo kwa ujumla. Huu ni mwongozo wa kipengele muhimu vitakavyokusaidia katika maombi yako. ambavyo kama utakuwa ni mwombaji wa mara kwa mara katika maeneo hayo, basi unajijengea mazingira ya kuwa mwanamke bora, mama bora, na zaidi sana mtumishi bora wa Bwana katika mwili wa Kristo.
Mwongozo huu unaweza kuutumia pia muwapo wanawake wawili au watatu katika kikundi chenu cha maombi, au kanisani. Na hivyo kila kipengele tenga muda wa kutosha kuomba.
- Omba Bwana akufanye kuwa shujaa wa injili, pia omba Bwana anyanyue jeshi la wanawake watetea injili, watumike vema katika nafasi zao kanisani,na nje ya Kanisa, kuwaokoa wenye dhambi. Katika maandiko Mfano wa Hawa ni Prisila Matendo 18:18, 26.
NANGA: Zaburi 68:11 “Bwana analitoa neno lake; Wanawake watangazao habari ni jeshi kubwa;”
- Omba Bwana akupe uwezo wa kuirithisha imani kwa vizazi vijavyo, Pia awanyanyue wanamwake vijana/wazee wengi wa namna hiyo, wenye uwezo wa kuirithisha imani ya Kristo kwa vizazi vingi mbeleni. Imani isiishie kwao tu, bali hata kwa vijukuu na vitukuu vyao.
Mfano wa wanawake hawa alikuwa ni Loisi.
NANGA: 2Timotheo 1:5 nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo
- Omba Bwana aamshe kwako na kwa wanawake wote Roho ya uombolezaji(kuugua ndani) mtakaosimama katika mahali palipo bomoka kwa ajili ya kulinyanyua kanisa na wenye dhambi.
NANGA: Yeremia 9:17 Bwana wa majeshi asema hivi, Fikirini ninyi, mkawaite wanawake waombolezao, ili waje; mkatume na kuwaita wanawake wenye ustadi, ili waje; 18 na wafanye haraka na kutuombolezea, ili macho yetu yachuruzike machozi, na kope zetu zibubujike maji. 19 Maana sauti ya maombolezo imesikiwa toka Sayuni, Jinsi tulivyotekwa! tulivyofadhaika sana! Kwa sababu tumeiacha nchi, kwa kuwa wameangusha makao yetu.
- Omba Bwana aamshe Kiu ya kupenda kujifunza Neno, ndani yako na kwa wanawake wengine wote wamchao Mungu. Mfano wa Hawa alikuwa ni Mariamu Dada yake Martha.
NANGA: Luka 10:39 Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake.
- Omba Bwana akupe Roho ya upole na utulivu; Sio ya vurugu au kutanga-tanga huku na huko kiroho, au kimwili. Sawasawa na Agizo Mtume Petro aliloliandika kwa kanisa (1Petro 3:1-6).
NANGA: 1Petro 3:4 bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu.
- Bwana aweke Roho ya utii, wewe na kwa Wanawake wote wamchao Bwana ndani ya Kanisa. Mfano wa ile iliyokuwa ndani ya Sara, ambayo aliweza kumtii Mungu, lakini pia mume wake.
NANGA: 1Petro 3:6 Kama vile Sara alivyomtii Ibrahimu, akamwita Bwana; nanyi ni watoto wake, mfanyapo mema, wala hamkutishwa kwa hofu yo yote
- Bwana akupe Roho ya kupenda kujisitiri, na kuvaa mavazi ya jinsia yako, vilevile awape na wanawake wote watakatifu moyo huo. (Kumbu 22:5)
NANGA: 1Timotheo 2:9 Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani
- Bwana akuumbie Roho ya kujitoa kwake Bwana, kwa mali zako, na kwa nguvu zako. ( Mfano wa hawa alikuwa ni Mariamu magdalena, Mshunami (Yohana 12:3, 2Wafalme 4:8-18))
NANGA: Luka 8:3 na Yoana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao
- Bwana aiamshe Roho ya ‘usaidizi’ katika huduma, pia iumbike katikati ya wanawake. Kumbuka wewe kama mwanamke umepewa karamu kubwa sana ya usaidizi tangu kuumbwa kwako. Ombea itende kazi vema ili iifaidie kanisa na familia.
NANGA: Mwanzo 2:18 Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye
- Bwana akuumbie Roho ya uaminifu hata pale ambapo hujapata kitu chochote. Usimwache Bwana.
NANGA: Luka 1:6 Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu, wakiendelea katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama. 7 Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana
- Akupe Roho ya kumwimbia Mungu kwa moyo wote wa furaha na kuchangamka Mfano wa wanawake mashujaa waliomcha Mungu zamani, ambao hawakuona aibu kumwimbia Bwana kwa mioyo yao yote.
NANGA: Kutoka 15:20 Na Miriamu, nabii mke, ndugu yake Haruni, akatwaa tari mkononi mwake; wanawake wakatoka wote wakaenda nyuma yake, wenye matari na kucheza. 21 Miriamu akawaitikia,Mwimbieni Bwana ,kwa maana ametukuka sana;Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini
- Omba Bwana akuumbie Nguvu ya “maombi ya kung’ang’ania” mpaka ipatikane ichipushwe pia miongoni mwa kundi Mfano wa Hawa alikuwa ni Rispa binti aya ambaye aliweza kukesha milimani kufunga na kuombeleza kwa miezi mingi mpaka mfalme akasikia habari zake, akatoa agizo juu yake
NANGA: Soma – 2Samweli 21, yote
- Bwana akupe Roho ya Uwazi na kusaidiana kwa umoja na wanawake wenzako wacha Mungu ndani ya kanisa na pia iwepo kwa wanawake wote.
NANGA: Luka 24:22 tena, wanawake kadha wa kadha wa kwetu walitushitusha, waliokwenda kaburini asubuhi na mapema, 23 wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika waliosema kwamba yu hai
PIA OMBA…
- Bwana akuumbie Roho ya uangalizi na ulezi kwa watoto, na vijana katika maadili ya kumcha Bwana
NANGA: 2Yohana 1:1 Mzee, kwa mama mteule na watoto wake niwapendao katika kweli; wala si mimi peke yangu, bali na wote waijuao ile kweli;
- Upewe Roho ya huruma na ya kutunza uhai. Mfano wa hawa ni (yehosheba). Aliuhifadhi uzao wa kifalme katika Israeli kwa kumficha mtoto asiuawe. (2Wafalme 11:2). Ilikuwa pia kwa mama yake Musa, lakini pia kwa Shifra na Pua wazalisha wa kiebrania
NANGA: (Soma Kutoka 1:15-19)
- Roho ya unyenyekevu na ya kujiachilia kwa Bwana moja kwa moja, bila kigugumizi chochote cha rohoni. Mfano wa Ruthu kwa Naomi, ambaye alijitoa kwa mkwewe katika hali zote bila kujali ujana wake, au umaskini wa mkwewe.
NANGA: Ruthu 1:16 Naye Ruthuu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; 17 Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; Bwana anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe name
- Akupe Moyo wa ujakazi mwema wenye manufaa, utakaowaleta wengine kwa Kristo ikiwa wewe ni mwajiriwa mahali fulani (Mfano wa hawa alikuwa ni Roda, & Yule kijakazi wa Naamani) – 2 Wafalme 5:1-19, Matendo 12:13
- Bwana akupe moyo wa kupenda kudumu hekaluni mwa Bwana. Vivyo hivyo na wanawake wote kanisani. Mfano ni Ana binti Fanueli.
NANGA: Luka 2:36 Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. 2.37 Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba
- Bwana akupe ufahamu wa kuyatunza Maneno ya Mungu moyoni wako. Usiwe wa kutokuzingatia kile Mungu anachosema na wewe. Mfano bora ni (Mariamu mamaye Yesu)
NANGA: Luka 2:51 Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia. 51 Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake
- Roho ya kupenda kujitaabisha kwa Bwana katika hekima yote ya ki-Mungu itokee ndani yako na kwa wanawake wengine. (Martha)-
NANGA: Luka 10:40 “Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi;..”
- Bwana akujalie wewe na wanawake wote Roho ya nguvu na ya ujasiri ya kuweza hata kuliamua taifa. Mfano wa Debora, katika nafasi yako kama mama.
NANGA: Waamuzi 4:4 Basi Debora, nabii mke, mkewe Lapidothi, ndiye aliyekuwa mwamuzi wa Israeli wakati ule. 5 Naye alikaa chini ya mtende wa Debora, kati ya Rama na Betheli, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu; wana wa Israeli wakakwea kwake, awaamue
- Roho ya kuthamini, Bwana alivyoviweka mkononi mwako, kuvilinda na kuvitafuta pindi vipoteapo.
NANGA: Luka 15:8 Au kuna mwanamke gani mwenye shilingi kumi, akipotewa na moja, asiyewasha taa na kufagia nyumba, na kutafuta kwa bidii hata aione? 15.9 Na akiisha kuiona, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimeipata tena shilingi ile iliyonipotea.
- Bwana akupe Roho ya kuridhika na hali, na mwonekano wako, kutoongeza mapambo mwilini. Usiwe kama Yezebeli-2Wafalme 9:30
- Bwana awajalie wanawake wote wakue kiroho, ili wasichukuliwe mateka na watu wadanganyifu (2Timotheo 3:6)
- Bwana awafariji wajane wote, lakini pia awape moyo wa kupenda kutoa na kutumika (Mfano wa Yule aliyetoa senti mbili, Yule aliyetembelewa na Eliya)-
NANGA: Soma (Marko 12:42, 1Wafalme 17:12, Luka 7:11)
OMBA PIA…
- Roho ya kuwajibika kwa wanawake, Bwana aiamshe kwako na katika kanisa (kupenda kushughulika Mithali 31:10-31
- Bwana awajalie wanawake wote Wajawazito kujifungua salama.(Kutoka 1:15-17, Isaya 66:9)
- Mabinti/ wanawake katika kanisa wanaotaka kuolewa, Bwana awape wenzi sahihi (Abigaili aliolewa na Nabali mume asiyestahili. -1Samweli 25) Jambo hilo lisitokee ndani ya kanisa.
- Magonjwa yanayoishambulia jinsia ya kike. Bwana ayafute mbali na wewe na ndani ya kanisa la Mungu (Marko 5:25-34)
PIA OMBA HIZI TABIA ZIONDOKE NDANI YAKO NA WANAWAKE WOTE…
- Roho ya kujichanganya na makundi yasiyofaa/ kutokuwa na mipaka, itoweshwe (Dina hakuwa na mipaka, akahadaiwa na watu wa kidunia – Mwanzo 34:1).
- Roho ya utoaji mimba, ipotelee mbali kwa wanawake wacha Mungu na kwa jamii yetu (Kutoka 20:13, Ayubu 3:3-12).
- Bwana aifutilie mbali tabia ya kupuuzia maono: Mke wa Herode alisemeshwa kwa ajili ya haki ya Yesu lakini hakuchukua hatua stahiki, kama Bwana alivyotaka (Mathayo 27:19)
- Wanawake wa kikristo wanaonyanyaswa kijinsi agh. Kulazimishwa kuolewa, kukeketwa, kubakwa, kupigwa, kunyimwa haki za elimu, na kumcha Mungu n.k. Bwana afutilie mbali hiyo roho; > Mfano ni Kisa cha Tamari na amnoni (2Samweli 13)
- Nguvu za giza zinazowavaa wanawake kiwepesi, zisipate nafasi ndani ya kanisa la Kristo.( Marko 16:9)
- Roho ya udanganyifu wa nyoka, (kushawishwa) Bwana aifukuzie mbali na kanisa lake takatifu (Mwanzo 3:1)
- Roho ya uuaji ya Yezebeli na Athalia, na herodia isipate nafasi ndani ya Kanisa la Bwana –, (2Wafalme 11:1, Mathayo 14:8)
- Roho ya kiburi isitokee miongoni mwa kundi (Vashti –Esta 1:12)
- Roho ya masengenyo, na udadisi ifutwe katikati ya kundi la Kristo (1Timotheo 5:13)
- Roho za ndoa kuvunjika, na magomvi zisitoe mzizi ndani ya kanisani. (Waefeso 5:33)
- Roho ya kukufuru kama ya Mke wa Ayubu Bwana aifutilie mbali. (Ayubu 2:9)
- Roho ya kupenda ulimwengu na mambo ya kidunia, iondoshwe (Mke wa Lutu) –Mawnzo 19:26
- Roho ya tamaa ya kuiba vya Mungu, isichipuke ndani ya kundi la wanawake ( mkewe Safira) Matendo 5:1
- Roho ya uzinzi ife iyeyushwe kabisa (mke wa potifa)- Mwanzo 39:7
- Roho ya ushirikina na uchawi isipate nafasi miongoni mwa wanawake (mganga wa Sauli)-Samweli 28:11
- Roho ya mashindano itoweke miongoni mwa wanawake (Lea na Raheli, wanawake hao)-Mwanzo 29:30
- Roho ya kuzira/ kukwazika mapema hata kutaka kuacha kutumika ifitwe miongoni mwa wanawake (Hajira- Mwanzo 16:9)
- Roho ya kutumiwa na adui (u-agent), ili kuliangusha kundi ifutwe (Delila –Waamuzi 16)
- Roho ya kusema uongo/ kutumia hila, isionekane ndani ya kundi (Mama yake Yakobo – Rebeka- Mwanzo 27:6)
- Roho ya uchungu usiokoma moyoni, vinyongo, visasa, kutokuachilia, kutokusamehe, iyeyuke ndani ya wanawake.(Yakobo 3:14)
- Roho ya matabaka, ndani ya Kanisa ipotelee mbali(Wafilipi 4:2). Sintike na Euodia
- Roho ya udhuru isisimame ndani ya kundi la wanawake kanisani. – (Matendo 1:14)
- Roho ya kudharau, watu wa Mungu, au kazi ya Mungu, isiwe na sehemu miongoni mwa wanawake( Mfano wa Mikali, binti Sauli. 2Samweli 6:16
Kwa ushauri/ Msaada/ Maombezi /Ratiba za ibada, wasiliana nasi kwa mawasiliano haya;
Na, Mwl Denis & Devis Julius
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine:
KANUNI YA KUOMBA NA KUPOKEA.
MWONGOZO WA MAOMBI YA WAHUDUMU/ WASIMAMAO MADHABAHUNI.
Kwanini wanawake wengi huwa wanalipuka mapepo?
NIFANYE NINI ILI MUNGU AYAJIBU MAOMBI YANGU?
MWANAMKE, BINTI, MAMA.( Sehemu ya 1)
Rudi nyumbani
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/01/01/maombi-maalumu-ya-wa-wamama-wanawake-wa-kanisani/