MWONGOZO WA MAOMBI YA WAHUDUMU/ WASIMAMAO MADHABAHUNI.

MWONGOZO WA MAOMBI YA WAHUDUMU/ WASIMAMAO MADHABAHUNI.

Ikiwa wewe una kazi ya kusimama madhabahuni/Mimbarani mara kwa mara kuwahudumia watu wa Mungu, basi ujue umewekwa mahali pa heshima sana, lakini pia pa kuwa makini sana. Kwa namna gani? Mahali pa heshima kwasababu ndio sehemu Mungu hushukia kuwahudumia watu wake, Hivyo wewe unakuwa kama lango la kwanza la Mungu, kusema au kutenda kazi kwa watu wake. Lakini pia usipopatumia ipasavyo una hatari kubwa sana ya kuuharibu utukufu wa Mungu. Na matokeo yake ni kuliathiri kundi zima kabisa, au ibada yote kutokuwa na maana.

Mara nyingine ibada kutofikia kilele cha Roho Mtakatifu, sio wale watu wasikiao kutokuwa makini, hapana ni kutokana na wahudumu kutokuwa na maandalizi ya kutosha ya kiroho na ki-mwili pindi haudumupo.  Kwa mfano ikiwa wewe ni mhubiri/Mchungaji, na unajua unaingia katika semina, au  jumapili utahudumu, halafu inafika asubuhi ya jumapili ndio uwaza ni nini cha kwenda kufundisha. Unaanda somo dakika 15tu, kisha unakwenda kusimama kuwahudumia watu wa Mungu, ambao wanatazamia walishwe Neno litakalowageuza maisha yao. Hapo ndugu usijidanganye, kuhudumu kwa namna hiyo sio kama Bwana anavyotaka.

Kumbuka kuwa machachari madhabahuni, kuwa na sauti kubwa, kuwa na uwezo wa kutoa vionjo mbalimbali, na watu kushangilia na kuruka-ruka, wakasema AMEEEN! Kubwa, ukadhani hiyo ndio ibada iliyowabariki watu. Hapo umejidanganya. Ibada isiyo na maandalizi haijalishi, imewarukisha watu kiasi gani. Hakuna uvuvio wa Roho!.

Ibada inaweza isiwe na makelele yoyote, mhubiri akawa ni mwenye kigugumizi, lakini ikiwa imeandaliwa vema kiroho. Maneno machache yanaweza yakawa na maana zaidi ya maneno elfu, na ya milio ya vinanda na gitaa. Watu wakajengwa, wakaguswa, wakafarijiwa, roho zao kwa namna ambayo wewe mhubiri unaweza ukadhani hujafanya jambo lolote. Isipokuwa wao wenyewe ndio wanaelewa mioyoni mwao.

Hivyo epuka njia za kisiasi na za kijamii, katika habari za kiroho. Mungu anataka amwachie Roho wake Mtakatifu kushughulika na hali za mioyo ya watu. Hivyo ni lazima ujue namna ya kumwandalia mazingira hayo Roho wake, ili afanye kazi kama apendavyo.

Kama wewe ni mhudumu yoyote, aidha mhubiri/ mwana-kwaya. Jifunze kuwa na maandalizi marefu. Andaa somo lako, ukianza siku kadhaa kabla, au kama umetingwa sana, siku moja kabla, ukitenga saa za kutosha za kukaa uweponi kwenye utulivu walau SAA 4-5, tena ikizidi  hapo inakuwa ni vizuri zaidi. Katika hizo, Tumia saa 2 na nusu Kuombea Somo na ibada, tena Tumia Saa 2 na nusu kuandaa somo lako. Ikiwa mchana kuna usumbufu, Muda wa usiku ni mzuri zaidi.

Sasa katika maombi yako omba Roho Mtakatifu akufanyie mambo yafuatayo;

1) Omba Mungu akupe Somo la Kufundisha: (Dk 15)

Wakati mwingine unaweza ukawa na somo lako kichwani, hiyo ni vema. Lakini liondoe hilo kwanza, msihi Roho Mtakatifu akufunulie alilolikusudia kuwafikia watu wake siku hiyo. Na kwa kufanya hivyo aidha atakupa jipya kabisa pale utakapokuwa unatafakari, au ataliboresha hilo ulilokuwa umeliwaza, au siku ile ile atayazungumza maneno mapya kwa kinywa chako. Hivyo usikimbilie moja kwa moja kuhitimisha na kile ulichokipanga kukisema. (Yohana 16:13)

2) Omba Bwana akujalie kuihubiri kweli yote ya Neno lake na kwa ujasiri.(Dk 15)

Ni rahisi kama mwanadamu, kuhubiri mawazo yako, au injili nusu-nusu, aidha kwa kuwaogopa watu, au kuwapendeza watu, au kuwahurumia watu. Hivyo omba Bwana akusaidie hapo. Ili usilighoshi Neno lake na mawazo au hisia zako. Bwana Yesu alisimamia kweli katika mafundisho yake yote.

Yohana 8:40  Lakini sasa mnatafuta kuniua mimi, mtu ambaye nimewaambia iliyo kweli, niliyoisikia kwa Mungu. Ibrahimu hakufanya hivyo.

Yohana 7:7  Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi; bali hunichukia mimi, kwa sababu mimi naushuhudia ya kuwa kazi zake ni mbovu

3) Omba Bwana aweke mifano kinywani mwako:(Dk 15)

Wakati mwingine lazima tuombe kuhubiri kama Bwana alivyohubiri. Yeye alitumia mifano mingi katika kuwasilisha Neno la Mungu. Na sisi pia hatuna budi kumwomba Roho Mtakatifu atujalie hekima hiyo. Husaidia sana watu kulielewa Neno kiurahisi na kulifurahia. Ukiomba Roho Mtakatifu anaweza kukufunulia wakati unaandaa somo, au wakati ule ule utakaokuwa unafundisha.

Marko 4:33  “Kwa mifano mingi ya namna hii alikuwa akisema nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulisikia; 34  wala pasipo mfano hakusema nao;..”

4) Bwana ayajalie maneno yako yawe yenye uweza pindi uhudumupo:(Dk 15)

 Maneno yenye uweza, ni maneno yenye mamlaka. Bwana akitujalia karama hii ambayo ilikuwa ndani ya Yesu, tutaweza kuitiisha madhahabu, na watu kulisikiliza Neno la Mungu kwa hofu ya Mungu, na kwa nidhamu, na kwa bubujiko, mpaka watu Kuokoka na kuacha maovu.

Luka 4:32  “wakashangaa mno kwa mafundisho yake, kwa kuwa neno lake lilikuwa na uwezo”.

5) Omba jina la Mungu litukuzwe:(Dk 15)

Katika kuhubiri kwako ni muhimu sana, kuomba jina la Yesu litukuzwe. Wahubiri wengi wasimamapo hujijengea mazingira yao ili watukuzwe. Ili waonekane wanaupako, wanashuhuda n.k.. Lakini sio Kristo ainuliwe. Msihi Mungu akupe unyenyekevu madhahabuni pake, Ibada isiyo mtukuza Kristo, haijalishi itakuwa na uzuri kiasi gani, ni bure. Watu watoke wamemwona Kristo na sio mtu au vitu (Wakolosai 3:17).

6) Mungu akupe roho ya upambanuzi, (macho yako ya rohoni yafumbuliwe).(Dk 15)

Tuhudumupo hatuna budi kumwomba Mungu daima atupe upambanuzi, ni maombi ya daima, inaweza isiwe katika ibada zote, lakini pale ambapo anataka kufanya jambo basi atupe kuona rohoni. Ili tuweza kutembea katika wazo lake. Kwamfano labda mtu anatatizo Fulani, na Bwana anataka afunguliwe kwa wakati huo. Hivyo ni vema tumwombe Mungu karama hii. (Yohana 16:30)

7) Bwana akujalie usiathiriwe na mazingira:(Dk 15)

Mazingira huwaarithi wahudumu, kwamfano pale unapoona watu hawazingatii unachowafundisha, wengine wamelala, au mazingira ya sauti za mbali, au watu wanaozungumza, janga Fulani n.k.. Huweza kukutoa katika umakini wa Roho Mtakatifu. Hivyo Bwana akufanye kipofu katika eneo hilo ili usiuzimishe mtiririko bora wa Roho Mtakatifu. Adui hupenda kutumia mbinu hii, kukuvuruga. (Matendo 20:7-12)

8) Omba nguvu za Mungu ziwepo kuwahudumia watu:(Dk 15)

Omba Kwa kupitia mahubiri au mafundisho watu wafunguliwe, waponywe, wabarikiwe, wafarijiwe, ishara. Ibada isiwe baridi, au ya maneno matupu tu. Shuhuda zitokee, ili watu wamtukuze Mungu.

Luka 5:17  Ikawa siku zile mojawapo alikuwa akifundisha, na Mafarisayo na waalimu wa torati walikuwa wameketi hapo, waliotoka katika kila kijiji cha Galilaya, na Uyahudi, na Yerusalemu; na uweza wa Bwana ulikuwapo apate kuponya

9) Omba Bwana akulinde na mishale yote ya yule mwovu: (Dk 15)

Adui huwawinda sana wahudumu, na wahubiri na hivyo mishale mingi huwa inatumwa rohoni kukuvuruga, aidha kihisia, au kiafya, au kiakili. Omba Bwana akuzungushie wigo wake. Uchawi wowote, au roho zozote nyemelezi zisipate nafasi ya kupakaribia pale ulipo, au kuvuruga unachokifundisha. (Zaburi 127:1)

Kumbuka maombi haya sio kwa wahubiri tu, bali pia kwa wengine wote wahudumuo, kama vile Wana-kwaya, waalimu wa watoto, vijana, wakina-mama, wainjilisti, wamishionari.n.k. maadamu unahudumu hakikisha unakuwa na maandalizi, ili huduma yako isiwe bure. Zingatia sana maandalizi ya muda mrefu. Ukimaliza walau Dakika hizo zote 135 kwenye maombi. Sawa na SAA MBILI NA NUSU. Ukatumia tena muda kama huo kuandaa chakula chako cha kiroho. Utajiweka vizuri sana Roho Mtakatifu kufanya kazi vema kupitia wewe.

Bwana akubariki. Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Pia tazama >>> JINSI YA KUSIMAMA NA KUFUNDISHA/ KUHUBIRI

Bwana

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

Mimbari ni nini? Je tofauti kati ya Mimbari na madhabahu ni ipi?

Jinsi ya kuandaa Somo la kufundisha

NIFANYE NINI ILI MUNGU AYAJIBU MAOMBI YANGU?

Nini maana ya kuabudu?

EPUKA KUCHELEWA IBADA.

Nini maana ya kumwabudu Mungu katika Roho na kweli?

SABATO ILIFANYIKA KWAAJILI YA MWANADAMU NA SI MWANADAMU KWAAJILI YA SABATO!

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments