Title September 2026

BWANA, UNATUACHAJE?

Kuna  kauli ambayo tunayo sana kwenye vinywa vyetu…Hususani pale boss au kiongozi wetu anapomalizana nasi katika mpango fulani na kutuaga..tunasema “bwana unaniachaje”?

Maana yake, baada ya kukaa chini yake muda mrefu, au kumtumikia, kuna namna anapaswa akuandalie mazingira ya kukufanya uendeleze lile jambo lake, au lako mwenyewe.. ndio hapo utaona wanawaachia watumwa wao aidha viinua mgongo, mitaji, au fedha za matumizi. 

Hili linaonekana ni jambo zuri kufanywa na bwana au kiongozi yeyote mwenye busara. 

Lakini kwa Yesu mambo yalikuwa tofauti, kwenye kauli yake ya mwisho alipokuwa anapaa.. Mitume hawakuachwa na lolote, na zaidi wanaambiwa wakashuhudie habari zake kutoka pale Yerusalemu walipo, waende uyahudi, Samaria na mpaka mwisho wa nchi.

Ukitafakari kwa ukaribu jambo hilo linahitaji rasilimali nyingi za kifedha, kiuchumi n.k. lakini hawakuachiwa hata senti kumi.

Ukiwa na mawazo kuwa kiongozi wako wa kiroho akuandalie rasilimali za kujikimu kimaisha, ndio ukamtumikie Bwana vizuri, ndugu utavunjika moyo..kwasababu yeye mwenyewe alipoitwa hakuandaliwa rasilimali, Na hilo halikuanzia kwake, lilianzia kwa mitume, hadi kwa wote waliofuata baadaye yao. Tena ungekuwepo nyakati za mitume ungevunjika moyo mara kumi zaidi.

Kumbuka Yesu anaonekana kama  “Bwana mgumu” kwa baadhi ya watumwa. Usipokuwa makini unaweza kumwona pia hivyo.

Kivipi?

Mkumbuke yule aliyepewa talanta moja aliona ameachwa bila màandalizi mazuri kimtaji…akabakia tu kulalamika na kusema huyu Bwana wangu ni mgumu sana.… hii talanta moja aliyoniachia  nitafanyia nini, Hata chakula cha siku moja tu hainitoshi, Bado anataka nimletee vingi, anataka kuvuna asipopanda… Ninakwenda kumwekea pesa yake. Nikafanye mambo yangu akirudi nimpe sitaki lawama.

Hakujua uamuzi huyo ni kosa kubwa..

Luka 19:20-26

[20]Akaja mwingine akasema, Bwana, hili ndilo fungu lako, ambalo nililiweka akiba katika leso. 

[21]Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna usichopanda. 

[22]Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako, mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, niondoaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda; 

[23]basi, mbona hukuiweka fedha yangu kwa watoao riba, ili nijapo niipate pamoja na faida yake? 

[24]Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang’anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi. 

[25]Wakamwambia, Bwana, anayo mafungu kumi. 

[26]Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang’anywa hata alicho nacho. 

Ukiona unasubiri ufanyiwe na Yesu kwanza kitu fulani ndipo uwe na hamasa ya kuifanya kazi. 

Kuwa makini. ROHO MTAKATIFU TAYARI YUPO NDANI YAKO UMESHAPEWA. Hakuna kingine zaidi ya hiko.  Simama kwenye huduma yako, Timiza utume wako.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

FUNDISHO, NI KUSEMA NENO USILOLIJUA

Ubora wa Kuhubiri au kufundisha haupimwi kwa elimu kubwa ya biblia, au mifano mizuri, au utashi fulani wa kupangilia maneno. Hapana, bali ni uwezo wa kupenya katika mioyo ya watu.

Haimaanishi kuwa na elimu ya biblia haichangii ubora wa fundisho au hubiri..inachangia sana lakini hiyo ni kama gamba la juu sana..ambalo linaweza lisitoe pia matokeo yoyote.

Pale fundisho linapoweza kuingia ndani ya moyo wa mtu, kupambanua, kuchoma, kulainisha, kupindua-pindua, kukarabati, kuponya hadi kumfanya mtu kuwa na mwitikio wa dhahiri wa nje. Hilo ndio linaitwa fundisho au hubiri kibiblia.

Sasa tendo hilo mpaka kufikiwa, si jambo rahisi hata kidogo, hakuna utashi wa kibinadamu unaweza kufanya hivyo.

Kwasababu hakuna anayejua ndani ya mtu mwingine kuna nini?

Lakini lililo gumu zaidi ni kuwa hata yeye mwenyewe hajijui vema, kama anahitaji matengenezo katika eneo fulani la moyo wake. Anaweza akawa ana hofu akadhani huwenda chanzo cha hofu hiyo ni ule ugonjwa uliomshika, kumbe chanzo ni kingine kabisa.

Kwasababu mwanadamu mwenyewe moyo wake ni fumbo kubwa.

Yeremia 17:9

[9]Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?

Umeona jinsi ilivyo ngumu sana. Ikiwa yeye mwenyewe hajijui, wewe mtu wa tatu utayajulia wapi yaliyomo moyoni mwake? Lakini Mungu anataka uyahubiri yahusuyo moyo wake.

Usifikiri unapomwona mtu, labda ana huzuni, au furaha au ana tabia za ulevi, wizi, , ukadhani anahitaji fundisho linaloendana na hiyo tabia unayoiona kwa nje.

Unaweza ukakosa shabaha kwa maili nyingi sana, ukifikiri tu hivyo.

Utamwona analia, pengine ni mgonjwa, amefiwa, amepoteza kila kitu kama ilivyokuwa kwa Ayubu na wewe unamfuata na fundisho la faraja, ukadhani kuwa ndio uponyaji wake utakapotokea.

Kumbe Mungu anajua anataka makemeo, na makaripio ili aponywe.

Wakati mwingine utasimama kwenye mkusanyiko wa watu wengi labda mia. Huko huko wapo wanaohitaji faraja, wanaohitaji unabii, wanaohitaji maonyo, wanaohitaji maarifa, wanaohitaji kufunguliwa. Sasa wewe unasimama na fundisho lako lenye mlengo mmoja wa makemeo, unadhani wote watahudumiwa na hilo. Kama ukikosa namna ya ki-ungu, unaweza ukawa unazungumza maneno yako.

Na lengo la Mungu ni watu wote wahudumiwe na Neno.

Hapo ndio linakuja suala la hakuna mbobezi wa fundisho au hubiri. Inahitaji hekima nyingine itokayo juu, ya kuhubiri usichokuwa na ufahamu nacho, au ujuzi nacho.

Siku ile ya Pentekoste, kilichotendeka mpaka ikapelekea watu wale kuchomwa mioyo, na hatimaye kuamini kwa idadi ile kubwa ya watu.

Haikuwa kwasababu walipaza sauti sana, au walihubiri kwa ujasiri sana, au maneno yao yalikuwa na elimu kubwa ya theolojia..

Hapana angalia utaona yalikuwa ni maneno ya kawaida kabisa… lakini yaliyoundwa na Roho Mtakatifu kwa namna ambayo yalipenya katika moyo wa kila mmoja.

Utaona, hatua ya kwanza walinena kwa lugha ambazo hata wao wenyewe hawakuzijua, lugha hizo zilikuwa zinawahubiria wengine.. zinanena mambo yao ya sirini, zinawakemea, zinawafariji, zinawaponya, zinawashuhudia Kristo.

Mpaka baadaye wanamaliza kunena tayari injili imeshahubiriwa wasijue ni kitu gani kimehubiriwa.

Petro aliposimama kumalizia maneno yake, wote wamenywea wanasubiri tu kupewa maelekezo ni nini cha kufanya baada ya pale..

Matendo ya Mitume 2:37

[37]Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

Hao ni watu wasio na elimu yoyote, walikuwapo waandishi, na mafarisayo wenye elimu lakini hakuna matokeo yoyote ya mafundisho yao.

Hata leo hii mimi na wewe.. Tujue kuwa kuhubiri na kufundisha hakutegemei sana ujuzi, au utashi, bali kunategemea zaidi Roho Mtakatifu.

Kwanini Roho Mtakatifu?

Kwasababu yeye ndiye anayeweza kuzama ndani ya mioyo ya watu na kujua shida zao, na kuwaponya.

Ni nini tunapaswa kufanya, ili fundisho likazame moyoni, lisitoke kwa makisio yetu?

Jambo kuu ni Kuwa na maandalizi ya kutosha.

Maandalizi hayo yapo kwa namna mbili.

1) Kumwandalia Roho Mtakatifu njia ya kuanzia..Ndio hapo unahitaji kwanza kusoma na kuandaa somo / fundisho. Kumbuka Ni lazama utenge muda kuandaa fundisho ambalo utalihubiri. Andika, na ujue pa kuanzia, bila kuwa na maandalizi hayo, unasema nitaenda tu kuzungumza. Ujue tayari umeizuia njia ya Roho Mtakatifu kufundisha.

2) Lakini hilo peke yake halitoshi, hatua nyingine ni kuomba maingilio ya Roho Mtakatifu yawe makubwa. Hapo ndipo unatenga muda mrefu wa kuomba, ili Roho Mtakatifu akatembee kwenye vyumba vya ndani kabisa ambavyo wewe hujui, wakati utakaposimama na kufundisha, kushuhudia.

Sasa ukimaliza hapo. Jiandae kwenda kusema ulichokusudia.. kumbuka mhubiri anayetumia dakika kumi kufundisha lakini amekuwa na maandalizi ya masaa matano kwenye kusoma na maombi. Ana nguvu zaidi ya yule atakayefundisha masaa matano, halafu alijiandaa kwa dakika tano.

Mwisho Ukienda kufundisha na kuona mazungumzo yako yanasogea nje ya mada, au taarifa nyingine zinakuja kichwani mwako tofauti na zile ulizoziandika kwenye daftari ujue ni kazi za Roho Mtakatifu usizizuie.

Baadaye utakuja kusikia tu shuhuda, na hata kama hazitasemwa, ujue Neno lako halijakwenda bure.

Tukiwa wahubiri na waalimu wa namna hii. Roho nyingi za watu zitaokolewa.

Kuhubiri ni kusema tusichokijua, cha wengine.

Shalom

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

NENO NA MAOMBI~ Sehemu ya 2 (AMRI YA UPENDO)

Jina la Bwana YESU libarikiwe, karibu katika kujifunza Neno na Maombi. Kusoma Neno bila Maombi, au kuomba bila Neno ni sawa na kitamba cha bendera kisicho na mlingoti, kupitia mfululizo huu wa tafakari hizi tutapata mwongozo sahihi wa kuomba kupitia maandiko ya kwenye Biblia.

PENDO LA MUNGU.

Bwana YESU alitufundisha kuwa Amri ya kwanza ni “Kumpenda Bwana na ya pili ni kuwapenda majirani kama nafsi zetu”.

Mathayo 22:36 “Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu?

37 Akamwambia, MPENDE BWANA MUNGU WAKO KWA MOYO WAKO WOTE, NA KWA ROHO YAKO YOTE, NA KWA AKILI ZAKO ZOTE.

38 Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza.

39 Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, MPENDE JIRANI YAKO KAMA NAFSI YAKO.

40 Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii”.

Na tena alisema…

Yohana 14:21 Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.

 

   1. OMBA ONGEZEKO LA UPENDO WA MUNGU NDANI YAKO (Tumia dakika 30)

i. Kwa moyo wako wote.

  • Hapa utaomba Bwana akujalie kumtafuta kwa hiari bila shuruti, kwasababu hiyo ndio maana ya kumpenda kwa moyo wako wote.

     ii. Kwa roho yako yote

– Hapa utamwomba Bwana kuwa upendo wako ukatoke rohoni, katika kumtafuta kwasababu Neno linasema waabudua watamwabudu baba katika roho na kweli.

               iii.    Kwa akili zako zote.

                           – Hapa utaomba Bwana akuwezeshe kumtumikia yeye kwa ujuzi aliokupa, (ule wa asili na ule wa kujifunza) kama ni msomi basi kupitia elimu yako hiyo umtumikie MUNGU, na kuyafanya mapenzi yake.

          iv. Kwa Nguvu zako zote.

      – Nguvu zinaweza kuwa za mwili kama wewe ni kijana, lakini pia zinaweza kuwa za kifedha, katika maeneo hayo yote mwombe BWANA akusaidie uweze kumpenda MUNGU na kufanya mapenzi yake, Utoe muda wako au mali zako katika kumtumikia MUNGU.

            2. OMBA UPENDO KWA JIRANI. (Tumia dakika 30)

Neno la MUNGU linatufundisha kuwa “Tujaponena kwa lugha zote na kufanya ishara zote kama hatuna Upendo sisi sio kitu”

      1Wakorintho 13:1 “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao”.

Na tena inasema…

Waebrania 13:1 “Upendano wa ndugu na udumu”.

    i. Omba Upendo kwa ndugu wa kiroho (Wachungaji na washirika wenzako)

  • Hapa utaomba Bwana akakukumbushe mema waliyokutendea.
  • Utaomba Bwana akuondolee chuki na kutokusamehe.
  • Utaomba Bwana akuoneshe kasoro zako ili pendo kati yako na wapendwa wenzako lidumu.
  • UOmbea kanisa na wakristo wenzako wakajawe na Upendo wa kiMungu.
  • Omba Bwana akaachie roho ya kusameheana.

     ii.   Omba Upendo kwa ndugu wa kimwili (Wana familia)

  • Hapa mwombe Bwana akuongezee upendo kwa wazazi, na ndugu wengine wadogo kwa wakubwa.
  • Waombee wana familia yako wajawe na upendo kama wewe unavyojiombea..

        3. KEMEA KILA ROHO INAYOJIINUA KUPOOZA UPENDO WA MUNGU, NA WA KINDUGU

Kemea kwa jina la YESU KRISTO kila pando la chuki kanisani kwako, katikati yako na wakristo wenzako, katikati yenu kama familia.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine: