WATAMTAZAMA YEYE AMBAYE WALIMCHOMA; NAO WATAMWOMBOLEZEA.

by Admin | 19 November 2019 08:46 pm11

Shalom.

Biblia inatuambia kipindi kifupi sana kabla ya kurudi kwa Kristo, na kile kipindi chenyewe cha kurudi kwake, kutakuwa na makundi mawili ya watu ambao watakuwa wakimwombolezea, Kundi la kwanza ni Waisraeli, biblia inatuambia hivyo katika Zekaria 12.

Tusome,

Zekaria 12:10 “Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma; nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza.

11 Siku hiyo kutakuwa na maombolezo makuu huko Yerusalemu, kama maombolezo ya Hadadrimoni katika bonde la Megido.

12 Nayo nchi itaomboleza, kila jamaa peke yake; jamaa ya nyumba ya Daudi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Nathani peke yao, na wake zao peke yao;

13 jamaa ya nyumba ya Lawi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Shimei peke yao, na wake zao peke yao.

14 Jamaa zote zilizosalia, kila jamaa peke yake, na wake zao peke yao.”

Na kundi la Pili litakuwa ni watu wa mataifa yote duniani, tunasoma hilo katika,

Ufunuo 1:7 “Tazama, yuaja na mawingu; na kila jicho litamwona, na hao waliomchoma; na kabila zote za dunia wataomboleza kwa ajili yake. Naam. Amina”.

Lakini tunapaswa tujiulize, ni kwanini biblia inasisitiza sana juu ya hao walimchoma ndio watakaoomboleza, na sio labda hao waliomsulubisha au waliotemea mate, au waliopinga mijeledi au waliomvika taji la miiba, au waliomtukana au waliomuudhi…

Lakini badala yake ni wale waliomchoma?. Lipo jambo la kujifunza hapo, ili na sisi tuwe makini sana tusiwe miongoni mwa kundi hilo ambalo hukumu yake ilishatabiriwa miaka mingi hata kabla ya tukio lenyewe kutokea. Na kurudiwa kuzungumzwa tena miaka mingi baada ya tukio hilo kutokea.

Kama tukirudi kutazama matukio ya pale msalabani, utaona muda mfupi kabla ya Bwana Yesu kuchomwa mkuki ubavuni, mateso yote yalikuwa yameshamalizika. Na Kristo tayari alikuwa ameshakata roho, hivyo hata Roho yake haikuwepo tena pale. Lakini tunaona, wale askari wa kirumi, walipopewa maagizo ya kwenda kuivunja miguu yao wote waliosulibiwa msalabani. Walifanya hivyo kwa wale wafungwa wawili llakini walipofika kwa Bwana wetu YESU Kristo walimwona kama tayari ameshakufa. Hivyo hawakumvunja yeye miguu. Lakini waliamua kufanya jambo lingine ambalo pengine hawakuagizwa. Wakachukua mkuki mrefu, ili wamchome, mpaka kwenye moyo, wakithibitishe kifo chake.

Hivyo wakafanya kama walivyokusudia wakauzamisha ule mkuki kwa nguvu na kupasua mfuko wa maji unaozunguka moyo. Na kupenya mpaka kwenye moyo wa Kristo na kuupasua..Na uthibitisho kuwa ulifika mpaka kwenye moyo ni yale maji na damu vilivyotoka. Ndipo wakawa na uhakika sasa asilimia 100 huyu hata kama alikuwa katika Comma sasa atakuwa amekufa kweli kweli..

Lakini wao waliona ni kawaida, lakini kwa Mungu halikuwa ni jambo la kawaida hata kidogo. Majeraha yote ya nje Kristo aliyotiwa na wale watu Mungu hakuyaangalia, lakini lile jeraha lililoingia ndani tena isitoshe limepenyeza mpaka kwenye moyo wa Kristo. Moyo wa Mungu, hilo hakulisahau mpaka wakati wa mwisho..

Na kwa kupitia hilo hilo watu ndio watakaomwombolezea Kristo katika siku za mwisho.

Yohana 19:34 “lakini askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji”.

Ndugu, maovu unayoyofanya sasahivi ni sawa na unamtia Kristo majeraha ya nje. Upo wakati hayo majeraha yatafika ndani ya moyo wake, na ukishafikia hiyo hatua Mungu hatakusemehe tena, kitakachokuwa kimebakia kwako mbeleni ni maombolezo..Leo hii ukishajiona tu umeachwa katika unyakuo basi ufahamu kuwa umemtia tayari Kristo jeraha hilo. Kinachofuata kwako ni maombolezo na kilio katika ile siku ya kisasi cha Bwana.

Kama ulikuwa hufahamu kalenda ya Mungu, ni kwamba kwasasa hivi tunachokingojea mbele yetu ni Unyakuo tu, dalili zote zimeshatimia, Na Unyakuo huo hautakuwa kwa watu wote, hapana bali utakuwa ni kwetu sisi watu wa mataifa tuliomwamini Kristo na wale wayahudi wachache sana ambao wamezaliwa katika Imani ya kikristo…(hao ndio bibi-arusi wa Kristo)

Lakini kundi la wayahudi wengi waliobakia, Unyakuo hautawahusu. Ukumbuke kuwa kwasasahivi Wayahudi wengi hawamwamini YESU KRISTO kama ni Masihi atayekuja, na hiyo yote Mungu amewapofusha macho kwa makusudi ili sisi watu wa mataifa tumwamini yeye,.Na hiyo itaendelea hadi wakati wetu utakapotia, ambapo utatimia na kitendo cha Unyakuo.

Sasa baada ya hapo hii neema ya injili tulionayo sasahivi, hii nguvu inayokushuhudia utubu dhambi sasa na unapuuzia, itahamia Israeli.

Mungu  atawafumbua macho yao, nao watagundua kuwa yule waliyemsulibisha miaka 2000 iliyopita kumbe ndio aliyekuwa masihi wao..Hapo ndipo na wao watakapooanza kuomboleza kama tunavyosoma hapo juu kwenye ule mstari wa Zekaria 12, Israeli nzima kutakuwa kuna maombolezo siku hiyo..Lakini wao Mungu atawapa rehema hivyo katika ile siku ya BWANA watafichwa, kwasababu walipigwa upofu na Mungu makusudi kwa ajili yetu..Hivyo Mungu atawasamehe, na baadaye watakaokolewa na kuingia katika ule utawala wa miaka 1000,…

Lakini sasa kwa haya mataifa mengine yaliyosalia, ambayo yalikosa unyakuo watakachokuwa wanakisubiria mara baada ya ile dhiki kuu ya mpinga-Kristo kuisha itakuwa ni kilio na kusaga meno, wataomboleza kwa vile walivyomchoma Kristo kwa Maisha yao ya kutokutubu walipokuwa wanaishi duniani, hapo ndipo kutakuwa na kilio na kusaga meno, na mara baada ya mapigo hayo tunayoyasoma katika Ufunuo 16, kitakachofuata ni ziwa la moto.

Sio pa kutamani kufika huko hata kidogo.

Je! Na wewe leo hii Unazidi kumtia Kristo majeraha?..Hizi ni nyakati za kumalizia ndugu Tubu kwa kumaanisha kabisa kumfuata Kristo, kwasababu siku ya karamu ya mwanakondoo aliyoiandaa kwa ajili yako na mimi mbinguni imekaribia kufika sana, na muda wowote parapanda italia, tutaalikwa kule.Roho anawashuhudia watu wengi, kuwa ile siku ya karamu imeshafika mlangoni. Hivyo Bwana atusaidie tufike ng’ambo yetu salama.

Ubarikiwe. Tafadhali “Share” Ujumbe huu na kwa wengine. Na Bwana atakubariki.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

UFUNUO: Mlango wa 7 & 11

KUVUNJA MAAGANO YA UKOO.

Shetani anatolea wapi fedha, angali tunajua Fedha na dhahabu ni mali ya Bwana?.

NIFANYE NINI ILI NIIKWEPE HUKUMU.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/11/19/watamtazama-yeye-ambaye-walimchoma-3/