by Admin | 4 December 2019 08:46 am12
Mwananchi ni mtu aliye na uraia wa Nchi fulani.
Kwamfano mtu aliyezaliwa Taifa la Tanzania ni mwananchi wa Tanzania, Kadhalika lipo Taifa la kimbinguni..Na hilo yeyote anayezaliwa katika Taifa hilo anaitwa Mwananchi wa Taifa la Mbinguni..Na kila mwananchi analindwa na katiba.
Biblia inasema katika..
1Petro 2:9 “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, Taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu;
10 ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema”.
Huwezi kuzungumzia Taifa bila kuhusisha mwananchi wa hilo taifa. Palipo na Taifa ni lazima pawepo na wananchi..Na Taifa la Mbinguni lina wananchi wake.
Hebu tuzitafakari dondoo chache hizi muhimu, ili zitusaidie kuelewa ni namna gani ufalme wa Mbinguni unafanya kazi.
Hivyo tupo tayari sasa kujifunza juu ya upande wa Pili wa uraia wa MBINGUNI. Kumbuka mbingu ni Taifa kama tulivyosoma hapo juu..Kwahiyo hebu tutafakari pia dondoo chache zifuatazo ili tuelewe zaidi.
Waefeso 6:11 “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.
12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.
13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.
14 Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,
15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; 6.16 zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.
17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; 6.18 kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote”
Hivyo Mwananchi yoyote wa Ufalme wa mbinguni hana budi Kuifahamu katiba kikweli kweli…Kama vile ilivyo jukumu la kila mwananchi kuifahamu katika ya nchi yake.
Madhara ya kutoifahamu biblia(Neno la Mungu) kwa Mwananchi wa Taifa la Mbinguni,.hayatofautiani sana na madhara ya mwananchi wa kawaida kutoifahamu katiba.
Mwananchi asiyeifahamu katiba, ni rahisi kufanya makosa na asijue kama anafanya makosa..Ni rahisi kwenda kulala na ndugu yake wa damu, na wakati hajui sheria ya nchi (katiba) inasema kwamba ni kosa mtu yeyote kulala na ndugu wake wa damu, hukumu yake ni kifungo cha maisha.
Kadhalika anaweza akagombana tu na ndugu yake na kwa hasira akaenda kumchomea nyumba yake, pasipo kujua katiba inasemaje kwa mtu anayepatikana kwa kosa la kuchoma nyumba..Kosa la kuchoma nyumba kulingana na sheria ya nchi yetu, hukumu yake ni kifungo cha maisha. Sasa mambo madogo tu kama hayo yanaweza kumsababishia akapoteza maisha yake yote kutumikia vifungo.
Vivyo hivyo mwananchi wa Taifa la mbinguni asipoielewa katiba ya mbinguni (yaani biblia) inasema nini, anaweza kujikuta anafanya mambo akidhani anampendeza Mungu kumbe anamchukiza Mungu pakubwa..na adhabu yake ikawa ni ziwa la moto milele..Mtu anaweza akawa ni mlevi akidhani ulevi si dhambi..anaweza akawa mwasherati akidhania uasherati sio dhambi..anaweza akawa mwabudu sanamu akidhani sio dhambi..n.k
Pia madhara mengine ya kutoijua katiba ni KUONEWA NA KUNYANYASWA. Mwananchi asiyeijua katiba ya nchi yake hata mtu akija tu anaweza kumtishia na kumnyima haki yake..lakini kama anaijua hawezi kubabaishwa kwasababu anaelewa vizuri sheria za nchi..Hivyo ni ngumu kupoteza haki yake..Vivyo hivyo Mwananchi wa Ufalme wa mbinguni asipoielewa vizuri biblia ni rahisi adui shetani kumnyang’anya haki yake. Utaona anapelekeshwa huku na huku, majaribu haya na yale..kuteswa huku na kule..Yote hayo ni kwasababu haijui biblia Neno la Mungu.
Na Dondoo ya mwisho kabisa ni kwamba kila mtu ili awe Mwananchi halali wa Taifa hilo ni lazima awe amezaliwa katika hilo Taifa (Huo ndio utambulisho wake wa kwanza),.. Vivyo hivyo katika Uraia wa ufalme wa mbinguni..Ni lazima mtu azaliwe katika ufalme huo.
Na mtu hazaliwi kwa damu na nyama, bali anazaliwa kwa Roho na kwa Maji ndipo ahesabike kuwa ni Mwananchi wa Taifa la Mbinguni.
Maana ya kuzaliwa kwa maji ni kubatizwa kwa maji mengi (Yohana 3:23) Na kwa Jina la Yesu (Matendo 2:38). Na maana ya kuzaliwa kwa Roho ni kupata ubatizo wa Roho Mtakatifu. Hatua hizo mbili ndio zinazokufanya uwe umezaliwa mara ya pili na kuwa Mwananchi wa ufalme wa Mbinguni.
Yohana 3:3 “Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.
4 Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?
5 Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.
6 Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.
7 Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili”.
Je umezaliwa mara ya PILI?. Je wewe ni Mwananchi wa Taifa teule la kimbinguni..Je wewe ni mrithi?..Kumbuka FALME NA MATAIFA YA DUNIA YOTE YATAPITA…Lakini UFALME WA MBINGUNI UTADUMU MILELE..NA RAIA WAKE WATADUMU MILELE!!.
Yapo mengi ya kujifunza juu ya ufalme huu wa mbinguni tukilinganisha na ufalme wa duniani..lakini Muda usingetosha kuyaandika yote hayo, lakini kwa haya machache, yatatupa chachu ya kuzidi kuutafuta ufalme wa mbinguni kila siku kwa bidii.
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAP
Tafadhali share na wengine.
Maran atha!
Mada Nyinginezo:
Mbona Mungu anaruhusu watu wapate shida, ilhali ana uwezo wa kutuepusha?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/12/04/mwananchi/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.