MAANA YA RANGI KIBIBLIA.

by Admin | 11 January 2020 08:46 am01

Utangulizi:

Wakati mwingine Mungu anaweza kutumia rangi kutufikishia sisi ujumbe fulani, mfano mara baada ya Nuhu kutoka katika Safina Mungu alimpa agano la upinde wa mvua kama ishara kuwa hatateketeza tena kwa maji, ambalo lilikuwa na mkusanyiko wa rangi saba..Jiulize ni kwanini auvike upinde ule rangi nyingi, na si kitu kingine? Angeweza tu kuweka kitu fulani chenye mfano wa picha au wingu, lakini hakufanya hivyo ilimpendeza Mungu kutumia upinde wa rangi kusimamisha agano lake. Ni wazi kuwa mkusanyiko wa rangi zote zile saba, ziliwakilisha Neema, kuwa Mungu hataangamiza tena dunia kwa maji.

Hivyo tutaangazia tafsiri ya rangi katika biblia, na maana zake rohoni. Lakini awali ya yote ni vizuri kufahamu kuwa hakuna rangi yoyote iliyo bora Zaidi ya nyingine, wala yenye uwezo fulani wa ki-ungu Zaidi ya nyingine..Kwasababu wapo watu wameshafundishwa na manabii wa uongo na waganga wa kienyeji, elimu za mashetani zinazowaambia, ukivaa nguo ya rangi fulani au ukinunua kitu cha rangi fulani kinawakilisha laana au baraka fulani, kwamfano ukivaa nguo nyeusi roho ya misiba inakuandama, mimi mwenyewe binafsi nimeshakutana na watu wa namna hiyo, Na wengine wanasema ukivaa nguo nyeupe roho ya Mungu inakaa juu yako n.k… 

Lakini hawajui kuwa biblia inasema shetani naye hujigeuza na kuwa mfano wa malaika wa Nuru.(ukisoma 2Wakorintho 11:14 utaona), Vivyo hivyo na watumishi wake wote. Hivyo hata yeye kutumuia rangi zinazoonekana zina utukufu kama nyeupe si jambo la kushangaza, anafanya sana tu, Ili kuthibitisha hilo ukisoma  kitabu cha Ufunuo sura ya 6:2-3, utaona yule mpanda-farasi wa kwanza akiwa amepanda farasi mweupe..Lakini yule hakuwa anamwakilisha Mungu, bali mpinga-Kristo mwenyewe.

Hivyo hali hiyo ya kuangalia rangi ki-mwili ili kuamua hatma ya Maisha yao, imewafanya watu wengi wawe na hofu hata wanapokutana na mnyama wa rangi fulani tu labda tuseme, nyeusi wanawaogopa au wanakataa kuwafuga kwa kisingizio kuwa wanatumiwa na wachawi.

Ndugu jiepushe na mafundisho hayo, Na katika siku hizi za mwisho yamekuwa ni mengi sana. Unaweza kuona yana hekima na yamejaa mafunuo lakini kumbe ndivyo yanavyokupeleka mbali na Mungu.

Lengo letu ni kukusaidia wewe kuelewa tafsiri za rangi pale unaposoma biblia na kukutana na rangi fulani basi ujue zilimaanisha nini..Vilevile wakati Mwingine Mungu anaweza kusema na mtu kwa njia ya ndoto au maono, akamwonyesha rangi fulani na asijue maana yake.Lakini mfano akiwa na ufahamu wa kutosha wa kujua rangi zilisimama badala ya nini katika biblia itamsaidia kupata upambanuzi wa alichoonyeshwa au alichokisoma kirahisi.

Rangi zipo nyingi sana, lakini tatazigusia zile ambazo zinaonekana na kuzimetumika mara kwa mara katika biblia.

Rangi Nyeupe:rangi nyeupe

Hii ni rangi ya usafi, utakatifu, nuru, palipo na weupe hakuna chochote kinachoweza kusitirika, hata uchafu unaonekana kirahisi katika kitu cheupe, sehemu nyingi utaona Mungu anajitambulisha yeye kama mwenye mavazi meupe, kichwa cheupe na nywele nyeupe (Danieli 7:9, Ufunuo 1:14 ), na kiti chake cha enzi ni cheupe(Ufunuo 20:11), vilevile watakatifu watapewa mavazi meupe. (Ufunuo 3:5)

Mbingu pia ni nyeupe, Hivyo Mungu ukikutana na rangi hii, kwenye maandiko au kwenye maono sehemu kubwa ya ujumbe wake ni Utakatifu, au usafi war oho, au Uwepo wa Bwana.

Nyekundu:rangi nyekundu

Hii ni rangi ya mwadamu, Adamu alitolewa katika udongo mwekundu, hivyo Mungu akamwita Adamu, Rangi hii pia ni rangi ya uhai, na maangamizo, hatari. Hivyo jambo kama hili ukiliona. Ujue upo umwagaji damu mbeleni au hatari fulani, au maangamizo mbeleni..Ukisoma Ufunuo 17, utaona yule mwanamke kahaba, Babeli mkuu akiwa ameketi juu ya mnyama mwekundu sana, ikiashiria kuwa ni muuaji.

Ufunuo wa Yohana 17:1  “Akaja mmoja wa wale malaika saba, wenye vile vitasa saba, akanena nami, akisema, Njoo huku, nitakuonyesha hukumu ya yule kahaba mkuu aketiye juu ya maji mengi;

2  ambaye wafalme wa nchi wamezini naye, nao wakaao katika nchi wamelevywa kwa mvinyo ya uasherati wake. 

3  Akanichukua katika Roho hata jangwani, nikaona mwanamke, ameketi juu ya mnyama mwekundu sana, mwenye kujaa majina ya makufuru, mwenye vichwa saba na pembe kumi. 

4  Na mwanamke yule alikuwa amevikwa nguo ya rangi ya zambarau, na nyekundu, amepambwa kwa dhahabu, na kito cha thamani, na lulu, naye alikuwa na kikombe cha dhahabu mkononi mwake, kilichojawa na machukizo, na machafu ya uasherati wake. 

5  Na katika kipaji cha uso wake alikuwa na jina limeandikwa, la siri, BABELI MKUU, MAMA WA MAKAHABA NA MACHUKIZO YA NCHI. 

6  Nikamwona yule mwanamke amelewa kwa damu ya watakatifu, na kwa damu ya mashahidi wa Yesu. Nami nilipomwona nikastaajabu ajabu kuu”.

Unaona, ukisoma pia Ufunuo sura ya 6 utaona yule mpanda wa pili, akiwa amepanda farasi mwekundu sana, ikiashiria kuwa ataeleta mauaji vita n.k.

Ufunuo 6:3  “Na alipoifungua muhuri ya pili, nikamsikia yule mwenye uhai wa pili akisema, Njoo! 4  Akatoka farasi mwingine, mwekundu sana, na yeye aliyempanda alipewa kuiondoa amani katika nchi, ili watu wauane, naye akapewa upanga mkubwa.”

Hivyo ukiona rangi hii ukiona rangi hii nyekundu kwa sehemu kubwa imetumika kama hatari, umwagikaji damu, au dhiki, au machafuko yapo mbeleni.

Njano/Dhahabu:rangi ya njano

Hii ni rangi inayowakilisha thamani ya kitu kilichotakaswa, ukisoma kitabu cha ufunuo utaona Mji ule Yerusalemu mpya njia zake zikiwa ni za dhahabu tupu (Ufunuo 21:18,21). Vilevile katika agano la kale vyombo vya madhabahuni vilivyokuwa ni vya dhahabu. Rangi hii pia inawakilisha moto, Moto hutakasa, na kusafisha, moto unamwakilisha Roho Mtakatifu.

Hivyo Rangi hii inasimama kama utakaso..Kitu kilichotakaswa, kimewekwa wakfu kwa ajili ya kazi fulani maalumu ya Mungu. Ni ishara kwamba kuna utakaso utapita ambapo utakufanya au kumfanya mtu awe thabiti kiimani kama dhahabu.

Zambarau:rangi ya zambarau Rangi kifalme, rangi za kikuhani, mavazi ya Haruni yalikuwa yamenakshiwa na rangi za zambarau. Kutoka 26:1. Hata wale askari waliomsulibisha Bwana Yesu, waliyatwaa mavazi ya kifalme ya zambarau na kumvika ili wamdhihaki.(Marko 15:17). Hivyo rangi hii inawakilisha ukuu, utawala, au mamlaka fulani.. Hata tuliposoma hapo juu habari za yule Babeli mkuu mama wa makahaba tumeona alikuwa amevaa nguo za rangi ya zambarau, kuonyesha ameketi katika kiti cha kitawala, kama malkia,..

Hivyo ukikutana na rangi hii ujue inazungumzia Ufalme, au utawala fulani.

Nyeusi:  rangi nyeusi Hii ni Rangi ya giza, uovu, upotevu, uchafu, . Sikuzote giza ni jeusi..Na ndio maovu yote yanapofanyikia.(Yuda 1:13). Hivyo utakapokutana na rangi hii basi ujue inasimama kuonyesha ufalme wa giza na mamlaka ya shetani. Hivyo kama ni katika mazingira ya maono basi unapaswa umuulize Mungu ushindane vipi na hali hiyo, kwasababu zipo nguvu za shetani mbeleni.

Kijani: rangi ya kijani kibibliaRangi ya uhai,ustawi, ubichi, palipo na uhai pana ukijani, mvua ikinyesha juu ya nchi, majani yanayochipuka huonekana katika rangi ya kijani..na hivyo ni rangi inayoashiria  neema na baraka kutoka kwa Mungu.

Mwanzo 1:11 “Mungu akasema, Nchi na itoe majani, mche utoao mbegu, na mti wa matunda uzaao matunda kwa jinsi yake, ambao mbegu zake zimo ndani yake, juu ya nchi; ikawa hivyo. 

12 Nchi ikatoa majani, mche utoao mbegu kwa jinsi yake, na mti uzaao matunda, ambao mbegu zake zimo ndani yake, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.

Hivyo ukikutana na rangi hiyo katika maandiko au katika maono basi ujue neema ipo mbeleni.

Bluu: maana ya rangi ya bluu kibibliaHii ni rangi ya utukufu wa Mungu..nikiziangalia mbingu ni kazi ya vidole vyako (Zaburi 8:3)…Milima japo kwa karibu utaiona na rangi tofauti tofauti lakini ukiitazama kwa mbali utaona yote inabadilika na kuwa rangi moja ya bluu, vivyo hivyo hata na vyanzo vikubwa vya maji kama vile maziwa na bahari, ukiyatazama kwa mbali muonekana wao unabadilika na kuwa wa bluu..

Hivyo hii ni rangi ya utukufu wa Mungu.. Mungu kukuonyesha rangi hii basi ujue, Mungu anataka uuone utukufu wake. Usipoipenda rangi hii basi hii dunia itakuwa ya-kuboa sana kwako kwasababu popote utakapoutazama ukuu wa Mungu rangi hii utaiona.

Rangi nyingine ni kijivu jivu:rangi ya kijivujivu kibiblia

Hii inafunua mauti na kuzimu.

Ufunuo 6:7  “Na alipoifungua muhuri ya nne, nikasikia sauti ya yule mwenye uhai wa nne akisema, Njoo!

8  Nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu akafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga na kwa njaa na kwa tauni na kwa hayawani wa nchi”.

Hivyo ikiwa utakutana na rangi kama hizi basi ujue hizo ndio maana zake kibiblia, Na kama tulivyosema, hakuna rangi iliyobora Zaidi ya nyingine tukizungumza kwa namna ya kawaida, usiache kuvaa nguo yako ya rangi nyeusi kwa hofu kuwa mapepo yatakuvamia, au rangi ya kijivujivu, hilo jambo halipo. Mungu akikuonyesha rangi fulani katika ndoto au maono au katika Neno lake basi ujue kuwa analengo la kukufundisha jambo fulani rohoni na sio mwilini.

Ubarikiwe.

Je! Umeokoka? Je unafahamu kuwa tunaishi katika siku za mwisho za kurudi kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwamba UNYAKUO siku yeyote unaweza kupita? Unajua kuwa hili ndilo kanisa la mwisho lijulinalo kama Laodikia na kwamba hakutakuwa na kanisa lingine Zaidi ya hili? Je unafahamu kuwa Neema hii ya injili hatutakuwa nayo milele, hivi karibuni itaondoka na kurudi Israeli?. Na ikishaondoka huku kwetu ni basi tena, hakutakuwa na neema?..Dalili zote zimeshatimia, tazama manabii wa uongo wengi walivyo duniani, tazama maovu yalivyokithiri, ni uthibitisho tosha kuwa dunia hii imeshafikia ukomo wake.

Unasubiri nini usimpe Kristo Maisha yako?

Ikiwa utasema siku ya leo sitaki inipite bado nipo katika vifungo vya shetani Basi uamuzi unaoufanya ni wa busara sana ambao hautakaa uujutie maisha yako yote kama ilivyokuwa hata kwetu sisi. Unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU  MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

Bwana akubariki.

   Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

 

Mada Nyinginezo:

HADITHI ZA KIZEE.

ZIFAHAMU NAMBA KATIKA BIBLIA NA MAANA ZAKE.

UMUHIMU WA YESU KWETU.

UWEPO WA BWANA HATA KATIKATI YA MATESO.

ALIKUWAKO NAYE HAYUKO, NAYE YU TAYARI KUPANDA KUTOKA KUZIMU.

LOLOTE ATAKALOWAAMBIA FANYENI.

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/01/11/maana-ya-rangi-kibiblia/