ZIFAHAMU NAMBA KATIKA BIBLIA NA MAANA ZAKE.

ZIFAHAMU NAMBA KATIKA BIBLIA NA MAANA ZAKE.

Zifahamu namba katika biblia na maana zake.


Tafsiri ya namba kibiblia.

Shalom, Jina la Bwana Yesu libarikiwe.

Kabla hatujaenda moja kwa moja katika tafsiri ya namba kibiblia, awali ya yote tunapaswa tufahamu kuwa hatuishi kwa kuangalia namba, hatutumii kigezo cha namba kuamua hatma ya Maisha yetu, au kutumia hizo kuunda siku fulani maalumu ya kuabudu, au kuifanya namba Fulani kuwa takatifu Zaidi ya nyingine. Lengo la kutoa tafsiri hizi ni kukusaidia wewe msomaji wa biblia kupata uelewa mpana zaidi jinsi namba hizi zilivyotumika na zinavyomaanisha rohoni.

Wakati mwingine Mungu anaweza kusema nawe kupitia namba, pengine kwa ndoto au maono au kwa kusoma. Hivyo ukipata uelewa wa kutosha juu tafsiri ya namba hizo kibiblia itakuwa rahisi kwako wewe kuielewa sauti ya Mungu.. 

NAMBA MOJA KIBIBLIA (1):

Hii ni namba ya Mungu, inayoeleza utoshelevu. Mungu yupo peke yake yeye ni mmoja tu, na anajitosheleza yeye kama yeye. Hakuna mwanadamu au kiumbe kingine chochote kinachoweza kujitosheleza chenyewe isipokuwa Mungu peke yake..  Ni hiyo inayotupa ujasiri wa kumwabudu Mungu kwa amani yote tukijua kuwa hakuna mwingine yoyote pembeni yake anayeweza kuchukua nafasi yake au kumpindua.

Kumbukumbu 6:4 “Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja.  5 Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.

 

NAMBA MBILI KIBIBLIA (2):

Hii ni namba ya Ushahidi: Kristo alipowachagua wanafunzi wake wengine wale wasabini aliwatuma wawili wawili(Luka 10:1).  Manabii  wawili tunaowasoma katika kitabu cha Ufunuo sura ya 11, ambao biblia inasema watatoa unabii wao siku 1260 yaani miezi 42, pale Yerusalemu wakiwa wamevaa nguo za magunia siku za mwisho haiwataji tu kama manabii bali inawataja kama  Mashahidi ni kwasababu gani?   Ni kwasababu wapo wawili.. Angekuwa ni mmoja, wasingeitwa mashahidi.

Hivyo na sisi unabii wowote au ndoto yoyote inaposemwa kwetu, kabla ya kuipokea ni lazima tupate uthibitisho wa Ushahidi Zaidi ya mara moja, Hata Farao alipoota ndoto, ilijirudia mara mbili ndipo alipofahamu kuwa Ndoto ile inatoka kwa Mungu..(Mwanzo 41:32)

Vile vile namba 2 inasimama kama namba ya muunganiko. Ndoa ni muunganiko wa watu wawili (Mwanzo 2:23-24). Vilevile muunganiko katika ya Kristo na kanisa lake. (1Wakorintho 12). Biblia takatifu ni muunganiko wa maagano mawili, la kale na jipya.

Hivyo na sisi tunapotembea wawili katika Imani tunapata nguvu  Zaidi kuliko tukiwa mmoja mmoja.

Mhubiri 4: 11 “Tena, wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kuona moto?  12 Hata ikiwa mtu aweza kumshinda yule aliye peke yake, wawili watampinga…”

Usipende kupigana vita ya kiroho peke yako.

 

NAMBA TATU KIBIBLIA (3):

Ni namba ya uthibitisho na uhakiki, mashahidi wanapokuwa watatu kila Neno linathibitika. Mungu alijidhirisha kama Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Kristo aliuonyesha utukufu wake katika ule mlima mrefu akiwa na wanafunzi wake watatu yaani Petro, Yohana na Yakobo, kama mashahidi walioshuhudia na kuona.

Halikadhalika hata katika kutoa hukumu, biblia inasema.

Mathayo 18:15  Na ndugu yako akikukosa, enenda ukamwonye, wewe na yeye peke yenu; akikusikia, umempata nduguyo. 16  La, kama hasikii, chukua pamoja nawe tena mtu mmoja au wawili, ili kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno lithibitike.

Vilevile, Mungu naye amethitika kwetu kati ofisi zake kuu tatu: Yaani Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Hii ni namba timilifu ya Mungu kwetu sisi wanadamu. Kama Mungu asingejifunua kwetu kupitia ofisi zake hizi kuu  tatu leo hii tusingekaa aidha tumwelewe au tuokolewe au tumkaribie kwa namna yoyote ile. Pale tunapookolewa ni sharti tupite hatua tatu, ya kwanza ni utakaso wa Damu ya Yesu, ya pili ni ubatizo wa maji, na ya tatu ni ubatizo wa Roho Mtakatifu.

Hivyo tunapopata Ushahidi wa tatu katika mambo yote Tunathibitika Zaidi, kuliko tunapopata mbili. Vilevile tunapozingatia hatua hizo tatu za utakaso bila kuacha hata moja,. Ndipo tunapothibitika ipasavyo kwa Mungu.

 

NAMBA NNE KIBIBLIA (4):

Hii ni namba ya kueneza kwa jambo fulani au tukio Fulani sehemu zote. Pale Edeni, Mungu aliutokeza mto kupita bustanini na baada ya pale akaugawanya katika vichwa vinne (Mwanzo 2:4).Kama vile biblia inavyosema pembe nne za nchi (Ufunuo 7:1, Isaya 11:12,). Vilevile Bwana akiiadhibu dunia au nchi huwa anatumia fimbo zake nne nazo ni, njaa, tauni, upanga, na hawayani wa mwituni,Soma.

Ezekieli 14:21 Maana Bwana MUNGU asema hivi; Je! U zaidi sana nitakapoleta hukumu zangu nne zilizo kali juu ya Yerusalemu, yaani, upanga, na njaa, na wanyama wabaya, na tauni, niwakatilie mbali nayo wanadamu na wanyama?

 Sehemu nyingine anatumia parare, tunutu, nzige, na madumadu..(soma Yoeli 2:25-27).

Lakini shetani naye vilevile anatumia namba hii, kuleta mafuriko yake ya uovu  duniani. Ukisoma Ufunuo kuanzia sura ya 5 utaona  wale wapanda farasi 4 ambao wanafunua roho ya mpinga-kristo inayofanya kazi duniani kote, wa kwanza akiwa mweupe, wa pili mwekundu, wa tatu wa mweusi na wanne ni wa kijivu..

Lakini ashukuriwe Mungu naye aliachilia roho 4 za kudhibiti hizo roho 4 za ibilisi duniani katika kanisa la Mungu..ndio wale wenye uhai wanne tunaowasoma katika Ufunuo 4:6

Hivyo kwa kuhitimisha namba nne ni namba  ya kutekeleza kusudi fulani au  kueneza jambo,  sehemu zote. 

 

NAMBA SITA KIBIBLIA (6):

Hii ni namba ya mwanadamu. Mwanadamu aliumbwa siku ya sita. Na vilevile inasimama kama mwisho wa kazi..Mungu alisitisha kazi yake yote aliyoifanya katika siku ya 6. Mwisho wa kazi ya mtu inaonekana katika  namba 6. Hata katika Maisha ya kawaida umri wa kustaafu ni miaka 60, ambayo ni sawa na 10×6, baada ya hapo unaingia katika pumziko lako.

Rohoni kila mmoja wetu amepewa siku sita za kutumika. Hivyo tumia muda wako vizuri. Bwana anasema Je! Siku za mchana si 12?, yaani 6×2..Imetupasa kuifanya  kazi maadamu ni mchana, usiku waja mtu asiweze kuitenda kazi.(Yohana 9:4).

Hivyo wakati wako ulionao hapa duniani, kibiblia upo chini wa namba hii 6,

NAMBA SABA KIBIBLIA (7):

Hii ni namba ya utimilifu. Kwamfano wana wa Israeli walipokuwa wanaingia katika nchi yao ya ahadi waliagizwa wauzunguke ukuta wa Yeriko mara 7 kisha utaanguka. Nebukadneza alikaa maporini kwa muda wa miaka 7 kabla ya kurudishiwa ufahamu wake na kuwa mfalme tena wa Babeli.  Makanisa ya Kristo yapo saba. Na wajumbe wake saba..Vilevile mapigo ya mwisho ambayo Mungu atayamwaga duniani kote kumaliza kazi zote mbovu za ulimwengu huu yatakuwa saba.

Lakini pamoja na hayo yote hii namba katika biblia inasimama kama namba ya pumziko. Mungu aliumba dunia kwa siku sita na siku ya saba akapumzika. Sabato ya Bwana.

Hivyo na sisi pia Watoto wa Mungu tumeundiwa sabato yetu na Mungu ambayo tutapumzika naye. Nayo itakuwa katika ule utawala wa miaka 1000

Waebrania 4: 8  “Maana kama Yoshua angaliwapa raha, asingaliinena siku nyingine baadaye. 9  Basi, imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu”

Hivyo siku tutakapoanza kutawala na Kristo katika ule utawala wa miaka 1000 katika roho tutakuwa katika namba hii 7 ya Mungu.

 

NAMBA KUMI KIBIBLIA (10)

Inawakilisha jumla, tunaona Amri kumi za Mungu, Jumla yake zilikuwa ni 10, wale wanawali ambao waliokuwa wanamsubiria Bwana wao aje kuwachukua waingie karamuni, walikuwa 10, ambao nusu yao walikuwa werevu na nusu yao wapumbavu. Soma tena Luka 19:13.

Hivyo hii namba katika biblia  inawakilisha jumla kamili.

NAMBA KUMI NA MBILI KIBIBLIA (12)

Hii ni namba ya msingi na ya malango. Taifa la Israeli limenyanyuka kutokana na Watoto 12 wa Israeli. Vilevile Kanisa la Mataifa limezaliwa kutoka katika injili ya mitume 12 wa Kristo. Wakristo tumejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, namba 12.  Mji ule, Mtakatifu Yerusalemu mpya utakaoshuka kutoka mbinguni, utakuwa na misingi 12 na malango 12 ambao ni wale mitume 12 wa Bwana, na makabila 12 ya Israeli. (Ufunuo 21)

Hivyo, palipo na msingi wowote wa rohoni, au malango yoyote ya mbinguni basi fahamu yameundwa kwa namba hii 12

 

NAMBA ISHIRINI NA MOJA KIBIBLIA (21):

Namba ya maombolezo. Danieli alifunga siku 21,akiomboleza.

Danieli 10:2 “Katika siku zile mimi, Danielii, nalikuwa nikiomboleza muda wa majuma matatu kamili.

3 Sikula chakula kitamu, wala nyama wala divai haikuingia kinywani mwangu, wala sikujipaka mafuta kabisa, hata majuma matatu kamili yalipotimia.

4 Na siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kwanza, nilipokuwa kando ya ule mto mkubwa, Hidekeli;

5 naliinua macho yangu, nikatazama, na kumbe, mtu aliyevikwa nguo za kitani, viuno vyake vimefungwa dhahabu safi ya Ufazi;

Siku za kuomboleza kwetu, rohoni zinatimizwa kwa namba hiyo 21. Mungu anaweza kukupitisha katika maombolezo mfano wa Yeremia akiiombolezea Yerusalemu. Ukiona hivyo ujue upo katika siku hizi 21 rohoni,..upo wakati utafika yatakoma na Mungu atakujibu dua zako.

 

NAMBA AROBAINI KIBIBLIA (40):

Namba ya kumaliza jaribu. Wana wa Israeli walizunguka nyikani kwa miaka 39 na mwaka wa 40 waliingia nchi yao ya ahadi, Musa, alikaa nyikani miaka 40 baada ya kuikimbia Misri, na mwisho wa miaka hiyo akarudishwa tena kwa ajili ya utumishi wa kuwaokoa wana wa Israeli. Kristo alijaribiwa nyikani siku 40.

Hata wewe kama ni mtoto wa Mungu, jiandae na 40 zako, kupitishwa jangwani. Kabla ya kufanywa kuwa chombo kiteule cha Mungu. Mtoto yeyote wa Mungu ni lazima apitishwe katika 40 zake ili amtengenezee Mungu Njia.. Isaya 40.

 

NAMBA AROBAINI NA MBILI KIBIBLIA (42)

Hii ni namba ya kutekeleza hukumu. Mpinga-Kristo siku mwisho atapewa mamlaka ya kufanya kazi miezi 42, ambayo ni sawa na miaka mitatu na nusu..Vilevile wale mashahidi wawili wa Bwana watapewa nao ruhusu ya kutoa unabii wao miezi 42, huduma yao itafuatana na mapigo yale kama Musa na Eliya waliyokuwa wanayatekeleza Misri na Israeli. Kwa kufahamu zaidi soma kitabu cha Ufunuo sura ya 11.

 

NAMBA HAMSINI KIBIBLIA (50):

Maachilio, kufanywa huru au wa kuanza upya tena. Mwaka wa 50 kwa wana wa Israeli uliitwa mwaka wa YUBILEE. (Walawi 25:8-13)Ni mwaka wa kuachwa uhuru kwa watumwa wote,.Katika agano jipya Roho Mtakatifu aliachiliwa katika siku ya Pentekoste ambayo ilikuwa ni siku ya 50 baada ya kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo.

Hivyo na wewe siku unapompokea Roho Mtakatifu rohoni, unahesabika upo katika namba hii ya maachilio yaani namba ya 50.

 

NAMBA SABINI KIBIBLIA (70):

Ni namba ya utumishi: Bwana Yesu awachagua tena wanafunzi wake 70 wengine, kwa lengo la kuwatuma waende kuitenda kazi ya Mungu. (Luka 10:1). Utaona pia Musa aliwachagua wazee wengine 70 kwa ajili ya kumsaidia kazi ya kuwahukumu watu.(Hesabu 11:16).

Vilevile hii namba katika biblia inasimama kama idadi kamili ya kumaliza jambo fulani…Kwamfano wana wa Israeli walipopelekwa Babeli Mungu alimwambia Yeremia kuwa watakaa kule Babeli kwa muda wa miaka 70..

Ukisoma tena Danieli 9 utaona Mungu akimwonyesha idadi ya majuma yaliyobakia kwa taifa la Israeli mpaka mwisho wa dunia utakapofika, akaambiwa yatakuwepo majuma 70.

Hivyo na wewe siku utakapoona hii dunia imeisha basi ujue namba hii imetimia, vilevile utakapoona Kazi ya Mungu inahubiriwa kwa kasi tena, yaani utumishi wa Mungu umeamka tena, basi ufahamu watumishi hao wapo katika idadi ya hii namba 70 katika ulimwengu wa roho.

 

NAMBA MIA SITA SITINI NA SITA KIBIBLIA (666).

Hii ni mamba ya mpinga-Kristo. Soma Ufunuo 13 inamueleza yule mnyama na hesabu ya jina lake ambayo ni 666. Kimsingi, yule mpinga Kristo atakaponyanyuka, na kazi zake kuonekana basi rohoni atakuwa katika namba hii, na uthibitisho kuwa atakuwa katika namba hii, ni kuwa hata jina lake litakuwa na hesabu ya namba hii 666.

Hadi sasa tumeshafahamu mpinga-Kristo atatokea wapi..Atatokea si pengine zaidi ya kanisa la Rumi, katika  kile kiti cha juu kabisa cha kipapa.

Leo hii mtu yeyote anayekalia kiti cha kipapa anajulikana kama VICARIVS FILII DEI.. Yaani tafsiri yake kwa kiswahili  ni BADALA YA MWANA WA MUNGU.

Hivyo ukihesabu hizo namba za kirumi, utaona idadi yake inakuja moja kwa moja katika namba 666.

Jina hili lipo katika kofia ile ya mapapa yenye ngazi tatu. Hivyo pamoja na ishara nyingine nyingi zilizonazo kanisa hili, ambazo zinamuhusu mpinga kristo katika kanisa hili. Tunaojasiri wa kimaandiko kusema kuwa mpinga-Kristo atatokea katika kanisa hili la Rumi.

Hivyo ndugu hizi ni nyakati za mwisho, Dunia imeisha, hizi ni saa za majeruhi, ikiwa unadhani hii dunia itakuwa na miaka mingi tena mbeleni jiangalie mara mbili. 

Je! Umeokoka?

Kama hujaokoka, Muda ndio huu, saa ya wokovu ndio sasa, usisubiri kesho. Hapo ulipo chukua muda mchache, jitenge binafsi piga magoti ukiwa peke yako, lia mbele za Mungu wako, mwambie nimekosa nisamehe Baba yangu. Maanisha kufanya hivyo kwasababu hapo ulipo yupo karibu na wewe kukusikia na kukusamehe. 

Ukishatubu dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha, basi ufahamu kuwa Damu ya Yesu imeshakusafisha moyo wako, uthihirisho kuwa utasikia amani au utulivu wa ajabu ndani ya moyo wako kuanzia huo wakati. unachopaswa kufanya bila kupoteza muda, ni kuacha kwa vitendo vile vitu viovu ulivyokuwa unavifanya kabla..kama ulikuwa na miziki ya kidunia kwenye siku yako ni unaifuta, kama ulikuwa na una picha za ngono kwenye siku yako unafuta zote, kama ulikuwa mzinifu, unazidi na mtu ambaye si mke wako, unaacha mara moja..

Sasa Kristo akishaona Imani yako iliyo katika matendo, ataingia ndani yako kufanya makao kwako na kukupa nguvu ya kushinda vile vilivyosalia. Pia baada ya kuokoka kwako, bila kupoteza muda nenda katafute mahali utakapobatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamwishwa katika maji mengi,  na Kwa jina la YESU KRISTO sawasawa na Matendo 2:38. Ili kuukamilisha wokovu wako.

Na baada ya hapo Mungu mwenyewe atakupa kiwapa cha Roho wake mtakatifu.

Ubarikiwe sana.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

    

Mada Nyinginezo:

ZIFAHAMU HUDUMA KUU (10) ZA SHETANI DUNIANI.

Tofuati kati ya Myahudi, Mwisraeli na Muebrania ni ipi?

NENO NI LILE LILE, LAKINI UJUMBE NI TOFAUTI.

MKUU WA ANGA.

NGUVU ILIYOPO KATIKA MAAMUZI.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
7 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
10 months ago

Namba 5, 8 na 9 umeiruka Mtumishi wa Mungu.

arch raymond
arch raymond
8 months ago
Reply to  Anonymous

amina tumelipata somo weka na maana ya rangi kibiblia

Bishops Daniel Maritim
Bishops Daniel Maritim
1 year ago

Asante Sana na mungu akubariki sana

Anonymous
Anonymous
2 years ago

Ameeeen Mtumishi Ubarikiwe kwa masomo mazuri ya kiroho.

Anonymous
Anonymous
2 years ago

mbona hujafafanua namba 8